Herbalist Dr MziziMkavu
JF-Expert Member
- Feb 3, 2009
- 42,872
- 34,363
Chanzo cha picha, Getty Images
Magazeti ya Uingereza na Kiarabu bado yametawaliwa kwa kiasi kikubwa na taarifa za milipuko ya vifaa vya mawasiliano vya 'pager' nchini Lebanon, huku yakijadili athari za mashambulizi haya kwa sura na sifa ya Hezbollah, na uwezo wa shirika la ujasusi la kigeni la Israeli (Mossad), ambalo linaaminika kuwa nyuma ya shambulio hilo, ingawa Israel haijadai kuhusika.
Magazeti pia yalijadili sababu za uwezekano wa shambulio hilo.
Tunaanza uchambuzi wetu wa magazeti na ukurasa wa maoni wa Guardian na makala ya Lina Khatib yenye kichwa cha habari :"Je, Hezbollah waliojeruhiwa na kudhalilishwa watafanya nini baada ya mashambulizi ya Pager?"
Mwandishi anasema kuwa shambulio la kipekee dhidi ya pager nchini Lebanon mnamo Septemba 17, likifuatiwa na shambulio dhidi ya simu za upepo siku moja baadaye, ni ukiukaji mkubwa wa usalama ambao Hezbollah imekabiliana nao katika historia yake.
Mashambulizi hayo, ambayo yanahusishwa sana na ujasusi wa Israel (Mossad) ingawa Israel haijadai rasmi kuhusika, yanaleta mtafaruku mkubwa kwa Hezbollah, na kusababisha pigo kwa maadili ya chama na uaminifu kama kundi lenye silaha ambalo linadai kuwa na viwango vya juu vya usalama, na kuiweka chini ya shinikizo kubwa la kulipiza kisasi, wakati huo huo ikipunguza chaguzi zake za hatua ya kijeshi.
Lina Khatib anaongeza kuwa chama hicho daima kimekuwa na usiri mkubwa katika kuendesha shughuli zake kwani mawasiliano yake yamekuwa ni muhimu katika kusaidia ulinzi wa Lebanon, kuunda mtandao wa mawasiliano tofauti kabisa na mtandao wa kitaifa, na kufanya shughuli za siri katika bandari ya Beirut na uwanja wa ndege, bila usimamizi wowote au kuingiliwa na mamlaka ya serikali, na kuimarisha hali ya usalama ndani ya jimbo la Lebanon. Lakini leo, Hezbollah haiwezi tena kudai kuwa na kinga linapokuja suala la usalama wake.
Mwandishi anaamini kuwa mashambulizi ya vifaa vya mawasiliano vya pager na ya simu za upepo yameharibu taswira ya usalama ya chama hicho, na kwamba kinalazimika kuhesabu kwa makini hatua zake zinazofuata dhidi ya Israel.
Anasema kutakuwa na shaka kubwa ndani ya chama kuhusu kile ambacho Israel inaweza kukipiga pia, ambacho kitasababisha kupungua kwa ari miongoni mwa taasisi za Hezbollah.
Kwa mujibu wa makala hiyo, ingawa Israel ina fursa ya kutumia muda huu kufanya operesheni kubwa ya kijeshi kusini mwa Lebanon, haitafanya hivyo, kwa sababu inaweza kuwa haina faida; Hezbollah imezoea kupigana dhidi ya Israel na inaweza kuhimili hasara kubwa, na baadaye inaweza kujenga upya silaha zake, kama ilivyofanya baada ya vita vya mwisho vya mwaka 2006.
Mwandishi anaamini kuwa mafanikio ya mashambulizi hayo yatamnufaisha Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kisiasa, ambaye amekuwa akikabiliwa na shinikizo kubwa la umma la kulinda mpaka wa kaskazini wa Israel na Lebanon, kwani anaweza kudai kuwa mashambulizi haya ni hatua inayoonekana kuelekea kufikia lengo hili, na kuendelea na operesheni za kijeshi bila mabadiliko ya kimkakati.
Lina Khatib anahitimisha kuwa changamoto hizi zote zinaiweka Hezbollah katika hali ya shinikizo lisilo la kawaida, kwani itataka kuokoa msimamo wake wa kisiasa nchini Lebanon na kudumisha uaminifu wake katika vita vyake dhidi ya Israeli.
"Hadithi ya ajabu na ya kutisha kutoka katika ulimwengu wa ujasusi"
Katika gazeti la Telegraph tunasoma ripoti ya Ed Cumming yenye kichwa cha habari "Siri ya kutisha ya sifa ya Mossad - iliyofunuliwa na maafisa wa zamani wa ujasusi wa Israel".Mwandishi anaelezea mlipuko wa vifaa vya mawasiliano vya pagers na simu za upepo nchini Lebanon kama hadithi ya ajabu na ya kutisha kutoka ulimwengu wa ujasusi, hadi kufikia kiwango cha zaidi ya uwezo wa kuonyeshwa katika sinema.
"Ukweli kwamba tulifaidika na matokeo haimaanishi kwamba tulipanga shambulio," anasema Avner Avraham, ambaye alihudumu katika Mossad kwa miaka 28-10 kati yake akihudumu nje ya nchi - na sasa anafanya kazi kama mshauri wa filamu za Hollywood kuhusu historia ya Mossad.
"Jambo ni kwamba operesheni hii ni ya kushangaza sana, ya ubunifu sana, kwa hivyo kwa kawaida ni mashirika ya ujasusi ya Marekani, Uingereza CIA, MI6 au Mossad tu ndio wangeweza kufanya kitu kama hiki. Kwa sababu utahitaji msaada wa serikali, ushawishi mwingi, na pesa kufanya kitu kama hiki."
Wakala huyo wa zamani wa Mossad Avraham anaongeza kuwa maisha ya Mossad ni magumu sana na sio kama James Bond. Kwa mtazamo wake, Mossad ana nguvu kuu mbili, ikilinganishwa na mashirika mengine ya kijasusi duniani.
- Ya kwanza ni kwamba "Wayahudi walikuja kutoka duniani kote, na kukulia katika maeneo tofauti, hivyo muonekano wao ni tofauti, na wanaweza kuzungumza lugha tofauti. Familia yangu ilitoka Iraq, na ninaweza kuzungumza Kiarabu na tunafanana na Waarabu wa Iraq, kwa hivyo nilifanya kazi na Mossad nchini Lebanon."
- Ya pili ni kwamba "vifaa maalum vya Mossad pia vilipigwa wakati wa miaka mingi ya vita... Kinachotufanya tuwe wazuri sana ni kwamba tulilazimika kupambana miaka yote hii ili kuishi katika nchi yetu."
Kama ilivyokuwa kwa huduma za ujasusi za Usovieti, Marekani na Uingereza katika kilele cha vita baridi, vikosi vya Israel kwa miongo kadhaa vimepata sifa ya ubunifu, kutafuta njia zisizotarajiwa za kufikia malengo yao, ambayo mara nyingi huwa ni ya siri na ya usalama, lakini mashambulizi ya hivi karibuni yamezidi hata makadirio ya juu ya uwezo wao, kulingana na mwandishi wa makala, Ed Cumming.
"Yote huanza kwa kutambua fursa," anasema afisa wa zamani wa Israeli katika kitengo siri kinachofahamika kama kigtengo cha 81, Eide anasema.
Aliongezakusema kuwa : "Hapa fursa ilijitokeza wakati Hezbollah ilipotaka vifaa vya mawasiliano ya jumbe vya pager kwa sababu walitaka kuepuka kutumia simu za mkononi ambazo zinaweza kudukuliwa na kufuatiliwa, lakini pia pager ni kifaa ambacho tunaweza kudukua kwa urahisi."
Makala hiyo inasema kuwa Hezbollah kiliamini kwamba pager zilikuwa salama, na kwamba haikutarajia uwezo wa vikosi vya Israeli kwa namna fulani kupenya kwenye maelfu ya vifaa kuanzia viwandani katika kile kinachoitwa shambulio la usambazaji wa bidhaa, kulingana na maelezo ya afisa wa Israeli ambaye alihudumu katika kikosi cha vifaru.
Afisa huyo wa zamani wa kitengo cha 81 anasema kuwa baadhi ya waajiriwa katika vitengo vya kiufundi vya Israeli wanaonekana wakiwa bado shuleni, na ana shaka kwamba maafisa wa ngazi ya juu wa jeshi walifikiria mpango wa pager. "Kijana mwenye umri wa miaka 25 lazima atoke na kusema, 'Angalia vifaa hivi, je, unadhani kuna kitu tunaweza kukifanya dhidi yake?'"
Makala hiyo inahitimisha kuwa wakati Hezbollah sasa inauguza majeraha yake, na dunia nzima inaangalia kwa mshtuko ubora wa teknolojia ya kutisha ya Israeli, raia nchini Israeli, Lebanon, na mahali pengine mbali zaidi wanashangaa mahambulio haya yanaweza kusababisha nini, kulingana na makala hiyo.
"Israel ilitaka shambulio kama hilo la Hezbollah dhidi ya Glilot"
Chanzo cha picha,Getty Images
Kwenye tovuti ya kituo cha Al-Mayadeen cha Lebanon - ambacho kiko karibu na
Hezbollah na Iran - tunasoma makala ya Ahmed Abdel Rahman yenye kichwa cha habari "Uhusiano kati ya shambulio la Pager nchini Lebanon na shambulio la Hezbollah dhidi ya Glilot ni nini?"
Mwandishi anasema kuwa mbali na athari za milipuko ya pager, kuna safu iliyofichwa katika tukio hili la uchungu ambalo huenda halijapokea sehemu yake ya uchambuzi, ambayo ni sababu za shambulio hili, ambalo analielezea kama la kijinga na hatari sana.
Abdul Rahman anaamini kuwa sababu za shambulio hilo zinaweza kuelezewa na matukio kadhaa:
Kwanza: Kuchochea upande wa kaskazini (kama matokeo ya mgogoro kati ya ngazi za kisiasa na kijeshi), na kupanua eneo la mapigano huko, ambayo yangelazimisha jeshi la Israeli kujiondoa kwa kiasi kikubwa kutoka Gaza,jambo ambalo hatimaye linaweza kumshinikiza Netanyahu kukubali kukomesha vita upande wa kusini.
Pili: Nia ya Israel kutuma ujumbe wa kuizuia Hezbollah na pande zote za mhimili wa upinzani, hasa baada ya shambulio la kombora la masafa marefu la Yemen mjini Tel Aviv siku chache zilizopita. Kwa hiyo, shambulio pana linalenga kukidhibiti chama na kukilazimisha kupunguza kiwango cha mashambulizi yanayotekelezwa.
Tatu: Kwa mtazamo wa mwandishi, kilicho karibu na ukweli ni kwamba shambulio hili kubwa lilikuja kujibu shambulio la Hezbollah kwenye kituo cha ujasusi cha "Glilot" mwishoni mwa Agosti mwaka uliopita, na athari kubwa lililoacha , baadhi ya siri ambazo zilionekana wazi zilizosababisha kujiuzulu kwa mkuu wa kitengo cha 8200, anasema Abdul Rahman.
Mwandishi anahitimisha kwamba Israeli "ilitaka kujibu operesheni hiyo ya kipekee na ngumu ambayo Hezbollah ilitegemea habari sahihi za kijasusi, na wakati huo iliamua kufanya operesheni ambazo ziliipa mwongozo wa usalama pamoja na mwelekeo wa kijeshi na uendeshaji, kupitia operesheni kama hiyo inayojulikana na mwelekeo wa usalama na ujasusi inahyotegemea sana uwezo wa kiufundi na kiteknolojia unaomilikiwa na serikali ya Kiebrania , ambayo inachukuliwa kuwa nchi yenye uwezo juu zaidi ulimwenguni katika Nyanja hii." chanzo.BBC