sulphadoxine
JF-Expert Member
- Nov 1, 2010
- 2,257
- 649
JUZI Ijumaa, Askofu Mkuu Mstaafu wa Kanisa la Anglikana Afrika Kusini, Desmond Tutu, aliyewahi kuwa shabiki maridadi wa chama tawala ANC, aliyekiunga mkono dhidi ya serikali dhalimu ya makaburu, alitoa kauli nzito iliyowaudhi viongozi wa ANC na watawala wa nchi hiyo.
Alisema: "Nimekuwa napigia kura chama cha ANC, lakini kwa masikitiko makubwa sitaweza kuwapigia kura tena, kwani sikubaliani na jinsi mambo yanavyokwenda."
Alitoa kauli hiyo katika makala aliyoandika kwenye Jarida la Prospect, ambayo imechapishwa pia kwenye gazeti la Mail & Guardian. Anasisitiza kuwa hana kadi ya chama chochote cha siasa, na anakiri kwamba ANC ilifanya kazi nzuri ya kupigania uhuru. Lakini sasa haoni kama kikundi hiki cha wapigania uhuru kimefanikiwa kujigeuza kuwa chama cha siasa kinachopigania maslahi ya wananchi walio wengi.
Kama vyama vyote vikongwe Afrika, ANC nayo imechoka. Matumaini waliyokuwa nayo wananchi mwaka 1994 wakati chama hicho kinaingia madarakani yameanza kufifia.
Baadhi ya watu waliokipigania, wameanza kukipinga. Baadhi ya waliokishabikia wameanza kufikiria jinsi ya kukiwekea upinzani imara. Baadhi ya waliokiweka madarakani wameanza kutamani kiondoke madarakani. Wengine wameanza mipango ya kukiondoa.
Ndivyo siasa ilivyo. Popote ambapo wananchi wanajua maana ya demokrasia, hiki ndicho kinachotarajiwa. Uongozi ni dhamana, kama alivyosema Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Wanaotawala wanaposhindwa kukidhi maratajio ya watawaliwa, wanachostahili kufanyiwa kwa haki kabisa, ni kuondolewa madarakani.
Yawezekana baadhi ya watu wakashangaa iweje ANC iliyoingia madarakani 1994 ianze kuchukiwa na wananchi, hata watamani kuiondoa, huku vyama kama ZANU-PF (Zimbabwe) na CCM vikiwa bado madarakani.
Ukweli ni kwamba ANC ni kikongwe kuliko vyote hivyo. Kilianzishwa mwaka 1912. Malengo yake yalikuwa yale yale kama ya vyama vingine vya ukombozi barani Afrika, kikiwamo TANU. Vilishamaliza kazi.
Kinachogomba sasa ni kwamba vimejikuta katika kutekeleza jukumu la pili, ambalo ni gumu - kuongoza serikali kidemokrasia na kuleta maendeleo kwa wananchi.
Haidhuru chama kimekaa madarakani kwa muda mrefu au mfupi kiasi gani. Ikishapita miaka 10, kwa siasa za kisasa, inatosha kwa wananchi kutoa hukumu ya haki.
Na mara nyingi watawala wanakuwa wameanza kuchoka na kuishiwa mawazo mapya na mipango mipya.
Baada ya miaka 10, watawala wanakuwa wameanza kunyemelewa na ufisadi. Wanakuwa wameshaanza kuona na kuhisi kwamba wananchi wana maswali mengi na magumu kuliko majibu ya serikali.
Watawala, badala ya kutimiza ahadi zao na kuweka mipango mipya ya kimaendeleo, wanaanza kujikita katika mikakati ya kujilinda wasiondolewe. Ndicho kipindi cha watawala kuasisi siasa za vitisho na ukatili dhidi ya wapinzani wao.
Ni kipindi cha uharibifu na ulevi wa madaraka. Na kwa sababu hiyo, ni kipindi cha mabadiliko ya watu na mifumo ya utawala.
Inasikitisha kwamba Watanzania tumechelewa kutambua ukweli huu. Katika Afrika, tumebaki sisi na Wazimbabwe (kama kumbukumbu zangu zipo sahihi) ambao tunaongozwa na serikali zinazoundwa na vyama vya wapigania uhuru wa miaka 50 iliyopita.
Tumegeuka mataifa ya watu wanaoongozwa na watawala wanaotamani "kufia Ikulu" ili wasije wakahojiwa kwa ufisadi waliotenda wakiwa madarakani.
Tumekuwa mataifa yanayotawaliwa kwa vitisho vya dola; ambamo wananchi wake, hasa wanaokosoa serikali, huishi kwa wasiwasi, kwani wanawindwa kama swala.
Kauli ya Askofu Tutu inaakisi kilio cha wengi. Inabeba hofu ya wengi wetu kuhusu mustakabali wa taifa letu. Inabeba matumaini ya wengi wanaopigana kuleta mapinduzi mapya ya kimfumo.
Ingawa ameitolea Afrika Kusini, inabeba ujumbe ule ule ambao watu wote wenye kuheshimika hapa nchini wangependa kutoa. Tatizo la watu wetu ni woga.
Wakati mwingine ni zaidi ya woga. Ni unafiki. Watu wenye haiba ya Askofu Tutu katika jamii yetu ni wengi, lakini wengi wao wanapenda kujisogeza karibu na watawala.
Wamegeuka sehemu ya uovu wa watawala. Wanabembeleza maslahi, "urafiki wa Kaizari" wanasaliti wananchi maskini. Wanatafuta kupendwa na wakubwa, wanachukiwa na wananchi.
Ndio hawa ambao serikali inapofanya mchezo mchafu halafu ikagundua mambo yameanza kuharibika, inawaita Ikulu kunywa chai, kupoza makali, kupiga picha, na kuwataka wawe mawakala wa kusafisha uchafu uliosambazwa na viongozi wa serikali.
Hawa wanasutwa na kauli ya Askofu Tutu. Vile vile, wanasutwa na dhamiri zao. Maana hapa tulipofikia, hata wasio na macho wanaona; na wasio na masikio wanasikia kishindo cha mabadiliko.
Moja ya sababu za wananchi kutaka "kuondokana na watawala hawa" ni mienendo na kauli zao katika masuala yanayogusa maisha ya wananchi.
Wanachosema watawala wetu, hasa kwenye hotuba wanazoandikiwa, sicho wanachoamini. Walichoahidi sicho wanachotekeleza.
Ni mawili. Ama wametuchoka au wamechoka. Na kama hali ndiyo hiyo, tusiwalazimishe kuendelea kutawala.
Najua wapo watu wema, wenye uwezo mkubwa, ndani ya mifumo hii mibovu. Lakini kama hawapati fursa ya kuwa juu, kufanya uamuzi na kusimamia utendaji, wema wao ni sawa na uovu wa watawala wenyewe. Hauna faida kwa kuwa hautumikii wananchi.
Hatuhitaji wema au uwezo wa vitabuni. Tunataka wema unaotafsirika katika vitendo vya ukombozi. Tunataka wema na uwezo utakaosaidia kudhibiti mfumuko wa bei na kupunguza makali ya maisha ya wananchi.
Tunataka wema utakaotafsiriwa katika sera mwanana zinazogusa maisha ya wananchi. Tunataka uwezo utakaopunguza idadi ya watu wanaokosa chakula, dawa, maji safi na salama, elimu bora na huduma nyingine muhimu katika jamii.
Hiki ndicho anachopigania Askofu Tutu. Ndiyo maana aliunga mkono harakati za ANC kuondoa makaburu. Ndiyo maana leo ana ujasiri wa kutamka hadharani kwamba "sitaweza kuwapigia kura tena."
Msimamo wa Askofu Tutu umenikumbusha kauli ya bibi kizee mmoja aliyesema ana umri wa miaka 84, mkazi wa Nyakatanga, wilayani Muleba, ambaye mwezi Septemba mwaka jana (2012), baada ya kuhudhuria mkutano wa hadhara wa CHADEMA, na kushuhudia wanakijiji wenzake walivyokuwa wanajiengua CCM na kuingia CHADEMA kwa wingi, aliomba kipaza sauti akasema, "na mimi sitapiga tena kura yangu kwa CCM, kuanzia leo najiunga na CHADEMA, nisije nikakosa watu wa kunizika!"
Ni kweli, watu tuliowaamini kwa muda mrefu ndio wametuangusha. Kwa siasa za Tanzania ya sasa, watu wenye maoni kama haya wapo wengi.
Wengine ni jasiri wa kujitokeza na kusema hadharani. Wengine, hata wakisema hawasikiki kwa kuwa hawana majina makubwa kama Askofu Tutu.
Lakini wapo, na hawa ndio hasa wanapaswa kusema na kusikilizwa. Hawa ndio Watanzania tunaozungumzia.
Nina hakika kama Askofu Tutu angekuwa Mtanzania angesema maneno yale yale kuhusu CCM. Naamini ametusemea. Tumemsikia.