SoC03 Matamko hayatamaliza matumizi ya mkaa, kuni

SoC03 Matamko hayatamaliza matumizi ya mkaa, kuni

Stories of Change - 2023 Competition

achaniseme2

New Member
Joined
Jul 27, 2023
Posts
2
Reaction score
2
DHAMIRA ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kutaka kumaliza matumizi ya kupikia Kuni na mkaa, inaonyesha wazi haitafanikiwa kwa muda waliojipa wa hadi kufikia mwaka 2032 iwapo hawatabadilisha mbinu wanazotumia.
Dhamira hiyo ya serikali iliwekwa wazi na Rais Samia Suluhu Hassan, mwaka Jana, jijini Dar es salaam, kwenye kongamano la kuhamasisha umuhimu wa kupikia chakula kwa kutumia nishati safi.

Lakini dhamira hiyo inaweza kugonga mwamba kutokana na matumizi ya nishati ya mkaa na kuni kuonekana kukua kwa kasi, na hilo limethibitishwa na Takwimu zilizotolewa Juni mwaka huu na shirika la kimataifa linalojihusisha na masuala ya kupikia nishati safi la Clean Cooking Aliance, Juni, mwaka huu.
Takwimu hizo zinaonesha kuwa watumiaji wa nishati za Kuni na Mkaa kwa sasa wapo milioni 950 kutoka nchi za kusini mwa jangwa la Sahara na Tanzania ni miongoni mwa nchi hizo lakini inakadiliwa kufikia mwaka 2050 itaongezeka na kufikia hadi bilioni 1.67.

SABABU YA ONGEZEKO LA MATUMIZI
Tafsiri ya ongezeko hilo linaonyesha wazi sio kazi rahisi kumaliza janga hili kwa matamko bali njia sahihi kwa kuwa watumiaji wengi wanakabiliwa na umasikini.

Ingawa baadhi ya watumiaji wanatambua matumizi hayo husababisha maradhi ya mapafu, moyo na magonjwa ya macho ikiwemo na kuwa chanzo cha uharibifu wa misitu, lakini wanatumia kutokana na kushindwa kumudu gharama za kupikia nishati safi za majiko ya umeme na gesi.

Wapo baadhi ya wananchi wanaoishi kwenye nyumba zenye umeme lakini hawautumii kwa kupikia majiko ya umeme kwa madai kwamba yanatumia umeme mwingi, hivyo wanakwepa kulipa gharama kubwa.
Suala la gharama kubwa pia linatajwa kukwamisha matumizi ya gesi kwa familia kubwa, ambapo ili ipate mtungi mkubwa wa gesi wa kilo 28 ambao unaweza kutumika kwa mwezi mmoja, kama utapikia vyakula vyepesi tu, unauzwa kwa Sh. 50,000.

Mwajuma Kitomori wa Kiromo, Bagamoyo, Pwani anasema, "Nikinunua gunia la mkaa la Sh. 30,000 natumia miezi miwili. Hii ni nafuu zaidi kwangu.

Gesi ya Petroli iliyoyeyuka (LPG) ya kilo 15 inayouzwa Sh. 50,000 inadumu kwa miezi miwili na nusu bado nalazimika kuwa na mkaa nyumbani kwangu lakini maharage au makande hadi yaive yanatumia gesi nyingi tofauti na Mkaa."

Naye Janeth Igalula wa Kimbiji, Kigamboni anasema, "Ingawa kuna wafanyabiashara wanaotengeneza mitungi midogo ya gesi ya kuanzia kilo mbili inayouzwa Sh. 6,000 lakini bado gharama yake ni kubwa kwa watu wa hali ya chini kutokana na kuwa gesi ni chache."

NINI KIFANYIKE
Ili kufanikisha kumaliza matumizi ya mkaa na kuni; kwanza ni kuhakikisha mitungi ya gesi inapunguzwa bei zaidi ya ile ya mkaa au ifikie mkaa.

Ili kupunguzwa lazima serikali iingilie kati kwa kuondoa au kupunguza kodi katika mitungi ya gesi ili wananchi wengi wa kawaida waweze kumudu kununua.

Wale walio na umeme serikali itazame namna ya kupunguza bei ya 'unit' ili iwavutie wengi kutumia majiko ya umeme kupikia vyakula hata vile vigumu kama Maharage au Makande.

Jambo jingine ni kutoa elimu ya umuhimu wa kupikia nishati safi na madhara ya kutumia nishati chafu, kwa Wananchi hasa wale wanaopata Kuni bure kwa kuzifuata porini na mashambani.

Pia Serikali iongeze juhudi za kuunganisha mabomba maalumu ya gesi kuingia majumbani kwa kuwa inakwenda taratibu sana hadi sasa na maeneo yaliyounganishwa ni Madimba (Mtwara), Songo Songo (Lindi), Pamoja na Bomba la kusafirisha gesi asilia hiyo kutoka Mtwara, kupitia Somanga Fungu mkoani Lindi, Pwani hadi Dar es Salaam.

Kwa jijini Dar es Salaam, wakazi waliofaidika ni wachache wa maeneo ya Ubungo, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Survey, Makongo Juu, Sam Nujoma, Shekilango, Sinza, Mikocheni – Coca-Cola na Mwenge.

Picha: mwanamama akipika chakula kwa Kuni, picha kwa hisani ya mtandao wa Majiraonline.
Screenshot_20230727-100541.jpg
 
Upvote 2
Back
Top Bottom