Matangazo yaongeza watalii nchini
habarileo
Oscar Mbuza
Wednesday,July 02, 2008 @00:04
Idadi ya watalii wanaotembelea Tanzania inaongezeka siku hadi siku kutokana na Mkakati wa serikali kujitangaza kupitia vyombo vya habari vya kimataifa kama Kituo cha Televisheni cha CNN na magazeti ya Marekani.
Ofisa Mfawidhi wa Idara ya Utalii katika Wizara ya Maliasili na Utalii, Philip Chitaunga, aliyasema hayo jana kwenye Maonyesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam.
Chitaunga alisema mkakati wa serikali wa kuvitumia vyombo vya habari vya Marekani, umefanya watalii wengi kutoka Marekani kuja nchini kutembelea maeneo mbalimbali ya kitalii. "Zamani watalii wengi walikuwa wanatoka Uingereza lakini sasa soko la utalii limebadilika na watalii wengi sasa wanatoka Marekani," alisema Chitaunga.
Katika hatua nyingine, alisema pamoja na nia ya Tanzania ya kuongeza idadi ya hoteli za kitalii ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, lakini mpango huo unafanyika wakati kuna tahadhari muhimu kuhusu mazingira na uhai wa wanyama.
Alisema ingawa Tanzania imepania kuona Hifadhi ya Serengeti inakuwa na hoteli nyingi za kitalii kama ilivyo kwa upande wa pili wa Mbuga ya Masai Mara nchini Kenya, ili kuongeza mapato yatokanayo na utalii, lakini suala la mazingira halijafumbiwa macho.
"Lengo letu ni kuwa na watalii wachache watakaotuingizia fedha nyingi na si kuwa na watalii wengi kupita uwezo wetu wa kuweza kuwahudumia kwa viwango vinavyotakiwa," alisema. Alisema mkakati uliopo hivi sasa ni kutangaza utalii wa asili utakaoiwezesha Tanzania kuwa na utalii wa aina tofauti na hivyo kuwafanya watalii kuona ulazima wa kuja kujionea utalii huu.