Mauaji ya vikongwe sasa yakomeshwe

Mauaji ya vikongwe sasa yakomeshwe

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Joined
Feb 3, 2009
Posts
42,872
Reaction score
34,363
Kumekuwepo na taarifa zinazojirudia rudia zihusuzo mauaji ya vikongwe hususan wanawake katika mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Mara nyingi mauaji haya huhusishwa na imani za kishirikina na kwa bahati mbaya, walengwa zaidi ni akina mama wenye umri mkubwa ingawa hata wanaume wazee nao pia huuawa lakini si kama ilivyo kwa akina mama vikongwe.

Kwa mfano, katika toleo letu jana ukurasa wa nane, kulikuwa na taarifa za kuuawa kinyama kwa wajane wawili ndugu wakazi wa kijiji cha Ilirika wilayani Geita.

Habari zilieleza kuwa wajane hao waliuawa usiku wa kuamkia juzi baada ya watu wasiofahamika kuvamia nyumba zao kwa nyakati tofauti na kuvunja kwa kutumia mawe maarufu kama `Fatuma.'

Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Ilirika, Fabian Mugetha, aliwataja waliouawa kuwa ni Chausiku Lukombe (60), aliyekatwa katwa sehemu kadhaa za mwili na kuchinjwa shingoni na kuachwa kichwa chake kikishikiliwa na ngozi nyembamba.

Mwingine ni Zuhura Lukombe (55), ambaye licha ya kukatwa katwa sehemu kadhaa za mwili, pia mkono wake wa kulia ulitenganishwa na kiwiliwili chake.

Licha ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Geita, Leonard Paulo, kuthibitisha kuwapo kwa mauaji hayo, lakini hakueleza kama kuna watuhumiwa waliokamatwa kuhusiana na tukio hilo la kusikitisha.

Mauaji haya ni mfululizo wa mauaji mengine kama haya ambayo sasa yamekuwa kama ni jambo la kawaida katika mikoa ya Kanda ya Ziwa hasa mikoa ya Mwanza, Shinyanga na Geita.

Mathalani, mwaka jana, gazeti hili pia liliandika habari za kuuawa kwa mpigo kwa vikongwe wanne katika kitongoji cha Chenzumla kijiji cha Lwenzera wilayani Geita Mei 10, mwaka jana kutokana na imani za kishirikina kisha nyumba pamoja na mali zao zote kuteketezwa kwa moto.

Vikongwe waliokumbwa na mkasa huo walikuwa ni Esther Konya (55), Lolensia Bangili (70), Kulwa Mashana (65) na Roza Masebu (65).

Pamoja na mauaji hayo, hakukuwa na taarifa za kuaminika kama waliohusika na mauaji hao walikamatwa na kushughulikuwa kwa mujibu wa sheria za nchi.

Mauaji kama haya yamekuwa yakisababisha huzuni kubwa kwa familia husika na na kulitia aibu taifa katika jamii ya kimataifa na ikumbukwe kwamba wanaouawa ni wazee ambao bila shaka huacha familia zao zikiteseka.

Kwa mfano, katika mauaji dhidi ya vikongwe hao wanne, mmoja wao, Esther Konya, alimwacha binti yake, Tatu Michael (19), akiwa anasoma kidato cha nne.

Tatu, alikuwa akimtegemea kwa asilimia 100 mama yake kuanzia ada ya shule, mavazi pamoja na chakula.

Baada ya kifo hicho cha mama yake, msichana huyo alilazimika kuomba msaada kwa wasamaria wema mbalimbali kupitia vyombo vya habari wamsaidie ili angalau afanye mtihani wake wa kuhitimu kidato cha nne uliokuwa uko mbele yake.

Tunawashukuru wasamaria wema waliotikia kilio cha msichana huyo na hatimaye kufanikiwa kufanya mtihani huo.

Lakini yatupasa kuelewa kwamba wapo watoto wengine kama Tatu ambao wazazi wao waliuawa kwa njia kama hiyo na hivi sasa wamebaki yatima na wanaishi maisha ya tabu na shida tupu.

Sisi tunadhani kwamba, wakati sasa umefika kwa serikali kukaa chini na kutafakari kwa kina jinsi ya kulikabili tatizo hilo ili kuleta amani katika mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Haiwezakani watu waendeshe mauaji dhidi ya vikongwe kwa miaka yote hiyo na wakaachwa wakitanua tu mitaani pasipo kukamatwa na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria.

Kila binadamu anayo haki ya kuishi na kwa msingi huo hakuna mtu yeyote mwenye haki ya kutoa uhai wa mwenzake na inapotokea hivyo, basi anapaswa ashughulikiwe kikamilifu kulingana na sheria za nchi.

Tunatoa wito kwa vyombo vya usalama kujipanga ipasavyo kuhakikisha kwamba mauaji ya vikongwe katika mikoa ya Kanda ya Ziwa yanakomeshwa haraka iwezekanavyo ili watu wanaofanya unyama huo watambue kwamba Tanzania inajali na kuheshimu uhai wa kila mtu.






CHANZO: NIPASHE

 
Ni dhambi kubwa kuua binadamu mwenzio kwa makusudi kisa unatafuta mali.
 
Back
Top Bottom