Maulidi Shein: Mwanamapinduzi, 'Trade Unionist' na mwana-ASP. Ushamsikia?

Maulidi Shein: Mwanamapinduzi, 'Trade Unionist' na mwana-ASP. Ushamsikia?

Mohamed Said

JF-Expert Member
Joined
Nov 2, 2008
Posts
21,967
Reaction score
32,074
MAULIDI SHEIN MWANAMAPINDUZI, ''TRADE UNIONIST'' NA MWANA-ASP...USHAMSIKIA?

Mazishi yana hulka ya kuwakutanisha watu waliopoteana kwa miaka.

Leo nimebahatika kukutana na Mzee Maulidi Sheni sasa ana umri wa miaka 93.

Mara ya mwisho kukutana na Maulid Shein ilikuwa mwaka wa 2008 niko na Dr. Harith Ghassany ndiyo kaja Tanga katika siku zake za mwisho kukamilisha utafiti wake wa historia ya Zanzibar uliopelekea kuandika kitabu, ''Kwaheri Ukoloni Kwaheri Uhuru,'' ambayo ni historia ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka wa 1964 ambayo kabla yake hakupata kutokea mwandishi kuandika kwa namna alivyofanya Dr. Ghassany.

Ikutoshe kuwa kitabu kina kurasa 497 kiasi cha kumuogopesha yeyote aliye mvivu wa kusoma lakini kumtia hamu yule apendae kusoma.

Wakati wa utafiti wa kitabu hiki kwa upande wa Tanganyika na hasa mjini Tanga na Dar es Salaam sehemu muhimu za mipango ya mapinduzi nilikuwa mara nyingi niko pembeni ya Daktari kama dereva wake wa kumkimbiza huku na kule.

Kwa ajili hii basi nimemfaidi sana Dr. Ghassany kwa kushuhudia nyakati zake za furaha na wakati mwingine akiwa na huzuni kubwa kwa yale aliyosikia yamepitika katika mapinduzi ya Zanzibar alipoelezwa na wale walioshiriki katika kuiangusha serikali ya Sheikh Mohamed Shamte .

Nimemwona Daktari kwa mara ya kwanza akiwa katika simanzi mchana kwa mara ya kwanza Kisosora Tanga nyumbani kwa Mzee Mohamed Omari Mkwawa nilipompeleka kumkutanishanae.

Mzee Mkwawa jina lake lingine maarufu ni ''Tindo'' alilopewa na Mzee Karume wakati wa kupigania uhuru wa Zanzibar.

Mkwawa siku ile katika kikao chao cha kwanza alikuwa kamfungulia Daktari yale ambayo hakuwa amepata kuyasikia popote au kusoma kokote si katika maktaba kubwa za Marekani kama Library of Congress au Uingereza Rhodes House Oxford.

Aliyosikia kutoka kwa Mzee Mkwawa yalimyong'onyeza kiasi Dr. Ghassany alikuwa na dua yake akipenda kisoma kila mara, ''Mola wangu ikiwa kitabu hiki kitaleta maelewano kwa Wazanzibari kijaalie kikamilike lau kama si hivyo na kipotelee mbali.''

Nimemuona Daktari akiwa katika furaha kubwa akiwa pembeni ya Mzee Mkwawa Kipumbwi maili chake kutoka Tanga asubuhi moja Mzee Mkwawa alipompeleka hapo kumuonyesha sehemu ilipokuwa kambi ya Wamakonde kutoka mashamba ya mkonge ya Sakura.

Hawa Wamakonde walikuwa msaada mkubwa katika kuipindua serikali ya Sheikh Mohamed Shamte.

Siku ile na asubuhi ile TIndo alimwonyesha Daktari pango kubwa lililofunikwa na kichaka kikubwa ambako chini ya kichaka kile pangoni vyombo viliegeshwa mchangani na kutolewa kiza kikiingia kuanza safari kwenda Zanzibar yeye Mkwawa na jeshi lake wakiwa abiria ndani ya chombo.

Furaha ya Daktari ilikuwa furaha ya mwanasayansi yeyote katika maabara anapofikia tamati ya kupata ufumbuzi wa tatizo lilikuwa likiwahangaisha wanasayansi wote.

Turejee kwa Mzee Maulidi Sheni.

Safari ya kumtafuta Maulidi Sheni ilifungwa Tanga na kiongozi wa msafara kuja Dar es Salaam alikuwa Mzee Mkwawa mimi nikiwa dereva.

Kituo chetu cha kwanza ulikuwa Msikiti wa Mzee Mwinjuma Mwinyikambi, Mwananyamala na haukuchukua muda mrefu tukampata Mzee Maulidi Sheni.

Maulidi Sheni na Mzee Mkwawa walikuwa hawajaonana miaka mingi sana.

Wanamapinduzi hawa mnyororo wao uliokuwa ukiwaunganisha ulikatika baada ya kifo cha Mzee Karume mwaka wa 1972.

Maulidi Sheni ndiye mtu wa kwanza kumfahamisha Mzee Mkwawa kuhusu kambi ya Sakura kama sehemu ya kutayarisha Mapinduzi ya Zanzibar.

Safari hii ya kumtafuta Mzee Maulidi Sheni ilikuwa kupata na yeye kauli yake kuhusu Kipumbwi na Sakura.

Daktari hakuwa anapenda taarifa nusu nusu za upande mmoja.

Vipi leo nimebahatika kukutana na Mzee Maulidi Sheni?

Tumefiwa na mzee wetu Ashraf Himidi na nilipofika msibani nikamuona Salim Msoma mmoja kati ya wasomi makini na bingwa wa lugha ya Kiingereza kukizungumza na kukiandika.

Salim kakaa na watu wengine na baada ya kusalimiana akanionyesha mtu mmoja mtu mzima sana, ''Unamjua huyu?''

Nimemtazama yule mzee lakini sikuweza kumtambua na yule mzee akawa ananiangalia lakini kwa ule mtazamo wake nikajua na yeye pia hakunitambua.

Lakini niliahidi pia kwa ajili ya utu uzima Maulidi Sheni hakuwa hadhir.

''Maulid Sheni huyo mwanamapinduzi, anayo mengi sana lakini hataki kusema. Sasa ana miaka 93,'' Salim alinifahamisha.

Hapo hapo sura ya Mauidi Sheni ikarejea katika kumbukumbu zangu.

Miaka 12 ilikuwa sasa imepita toka siku ile nilipomwendesha Daktari kutoka Tanga hadi Msikiti wa Mwinjuma Mwinyikambi, Mwananyamala kwenda kumtafuta tukiongozwa na Mzee Mohamed Omari Mkwawa.

Salim Msoma hakuwa anafahamu kuwa Maulidi Sheni alishazungumza na Dr. Harith Ghassany mazungumzo ambayo naamini ndiyo yalikuwa ya mwisho katika mstari mrefu wa wale walioeleza waliyoyajua kuhusu Mapinduzi ya Zanzibar.

Nilikuwepo siku Mzee Maulidi Sheni alipokuwa anahojiwa na Daktari tumekaa ufukweni Sea View Dar es Salaam na kwa utulivu mkubwa nilisikiliza mazungumzo yao.

Baadhi ya yale ambayo alieleza katika historia ya mapinduzi yalitufadhaisha sote.

Baada ya mahojiano haya nilipobaki na Daktari tulisema mengi kuhusu yale tuliyosikia.

Baada ya mahojiano haya Dr. Ghassany alirejea Washington DC kukamilisha kitabu.

Nimefurahi sana kukutana tena na Mzee Maulid Sheni na ingawa utu uzima umemtopea na hakuweza hata kuitikia salamu yangu na muda wote mfupi niliokuwa pale na Salim Msoma yeye alikuwa kama hayupo, kanzu yake nyeupe aliyovaa ilikuwa safi imemkaa vema pamoja na kofia yake ya Kiomani.

Allah atuhifadhie mzee wetu na amjaalie siha njema.

PICHA;
Kushoto Mohamed Omari Mkwawa, Maulidi Sheni na Mwandishi Tindo kakishika kitabu, ''Kwaheri Ukoloni Kwaheri Uhuru.''
 

Attachments

  • MAULIDI SHEIN.jpg
    MAULIDI SHEIN.jpg
    43 KB · Views: 2
  • KWAHERI MKOLONI NA TINDO.JPG
    KWAHERI MKOLONI NA TINDO.JPG
    28 KB · Views: 2
Asante kwa andiko lako limenifanya nitafute Kitabu cha Dr.Ghassany.Nimekipata naanza kukisoma
 
Hawa wazee wako waliua sana Wazanzibar kwenye mapinduzi ya kumtoa Shamte, Wapemba mpaka leo wanateseka kwa ajili yao. Mapinduzi yalikuwa batili.
 
Hawa wazee wako waliua sana Wazanzibar kwenye mapinduzi ya kumtoa Shamte, Wapemba mpaka leo wanateseka kwa ajili yao. Mapinduzi yalikuwa batili.
Laki...
Sijui kwa nini unakuja na lugha hii kuwa wazee wangu waliua sana Wazanzibari.

Hapa nadhani unawakusudia Mzee Mkwawa na Maulidi Sheni.

Ikiwa unachukulia kushiriki katika mipango ya kuivamia Zanzibar na kupindua serikali na mauaji kutokea ni kuua, hakika wameua lakini lawama hii itakuwa kwa wengi kwani mpango huu uliwahusisha wengi katika serikali ya Tanganyika iliyokuwapo madarakani mwaka wa 1964.

Lakini ukweli ni kuwa katika wale waliokuwa katika mpango huu walikuwapo wengi ambao hawakujua kuwa kuna kambi Kipumbwi itashiriki katika mapigano ndani ya ardhi ya Zanzibar.

Mauaji mengi yalifanywa mashamba na wale Wamakonde waliotoka Kipumbwi, kesi za Mzanzibari kumuua Mzanzibari nduguye ni chache sana.

Ilipokuja kujulikana yale mauaji yaliyotokea tena baada ya serikali imekwishaanguka wengi wa wale ambao kwa namna moja au nyingine walikuwa wameshiriki katika mipango ile, hawakutaka kabisa katika maisha yao kuhusishwa na mapinduzi.

Mmoja katika hawa waliokuwa hawataki kuhusishwa na mapinduzi alikuwa Ali Mwinyi Tambwe.

Unasema mapinduzi yalikuwa batili.

Ali Muhsin Barwani na Wazanzibari wengi wana fikra kama zako.

Hii ni moja ya sababu kwa nini CCM Zanzibar inapata tabu sana kushinda katika kila uchaguzi visiwani.

Ukisoma kitabu cha Ali Muhsin, "Conflict and Harmony in Zanzibar," utaelewa zaidi.

Yapo mengi.



Sent using Jamii Forums mobile app
 
Safi sana


Sent from my iPhone using JamiiForums
 
Back
Top Bottom