Nimeshtushwa na thamani ya mali zisizohamishika ambazo Mh. Yona na Mwenzake Mramba, waliziwekana kama rehani dhidi ya uhuru wao katika kesi inayowakabili ya matumizi mabaya ya madaraka yao.
Kilichinishtua sio uwezekano wa Mtanzania kuwa na mali nyingi kiasi hiki, la! Ila haijaniingia akilini namna gani mtumishi wa umma anaweza kupata mali nyingi kiasi hiki kutoka katika mshahara ama posho.
Je, walikuwa wafanyabiashara kabla ya kuwa mawaziri au kushika nyadhifa mbalimbali za uongozi wa umma? Kuna mwenye kujua hilo?.....Naambatanisha.
Yona ajidhamini Wazomewa na kadamsanina waandishi wetu WAZIRI wa zamani wa Madini na Nishati, Daniel Yona, jana Jumanne, alikuwa kivutio na gumzo kubwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, alipojidhamini kwa mali zake mwenyewe zenye thamani ya Sh. bilioni 3.69 ili kuepukana na adha ya kurejea rumande ya Keko.
Wakati Yona alijidhamini kwa mali zake mwenyewe, Basil Mramba ambaye anashitakiwa naye kwa makosa ya kutumia vibaya madaraka yao na kuisababishia Serikali hasara ya zaidi ya Sh. bilioni 11, alijidhamini kwa mali zake, kampuni na mali za watu wengine wawili, Hatibu Senkoro na Harun Mohammed zinazofikia Sh. bilioni 3,146,660,000.
Mmoja wa wadhamini hao wa Mramba, Senkoro sasa anafanya kazi katika kampuni ya Barrick ya Canada lakini yenye kuendesha migodi duniani kote ukiwamo wa dhahabu wa Geita aliko Senkoro. Kabla ya kujiunga na Barrick aliongoza kwa miaka mingi kampuni ya TDFL iliyokuwa ikuhusika na masuala ya fedha.
Mbele ya Hakimu Mkazi Hezron Mwankenja, Yona ambaye ni mshitakiwa wa pili kupitia mawakili wake, Stanslaus Boniface na Frederick Manyanda, aliwasilisha hati ya kwanza ya nyumba yenye namba 57467 yenye thamani ya Sh. milioni 443.
Hati ya pili iliyowasilishwa na waziri huyo wa zamani ilikuwa ya nyumba yenye namba 59935 yenye thamani ya Sh. bilioni 2.2 na ya tatu yenye namba 57230 yenye thamani ya Sh. 420,300,000. Nyumba zote hizo ziko Makongo Juu, Dar es Salaam.
Mapema kupitia kwa mawakili hao hao, Mramba ambaye ni mshitakiwa wa kwanza katika kesi hiyo, aliwasilisha hati ya nyumba yenye namba 42578 iliyoridhiwa na Senkoro yenye thamani ya Sh. milioni 397.
Aliwasilisha hati nyingine yenye namba 44755 Kitalu namba 138 Kitalu C ya Harun Mohammed yenye thamani ya Sh. bilioni 1,226,200,000.
Mramba pia aliwasilisha hati namba 7217 ya Kitalu 53 Msasani mali ya kampuni ya Kilimanjaro Mine Limited yenye thamani ya Sh. 976,420,000 na hati ya nyumba yake mwenyewe namba 40268 Kitalu namba 446 iliyopo Kawe, Dar es Salaam yenye thamani ya Sh. 547,400, 000.
Baada ya kupokea hati zote za washitakiwa zilizowasilishwa kupitia kwa mawakili wao, Hakimu Mwankenja alisema kwamba washitakiwa baada ya kushindwa kutimiza sharti la awali la kila mshitakiwa kulipa fedha taslimu Sh bilioni 3.9 walikwenda kwenye mahakama ya juu (Mahakama Kuu) kuomba kulegezwa kwa sharti hilo.
Sharti hilo lililegezwa kwa kutakiwa kila mshitakiwa kutoa hati za mali zenye thamani ya Sh bilioni 2.9, sharti ambalo washitakiwa walikuwa wametimiza kwa kuwasilisha hati hizo.
Hakimu Mwankenja alisema baada ya hati hizo kuhakikiwa na waendesha mashitaka, mawakili wa utetezi na Mahakama yenyewe na kwa kuwa hakukuwa na upande wowote uliowasilisha pingamizi kuhusiana na hati hizo, Mahakama iliridhia washitakiwa, ambao walikuwa chini ya ulinzi, waachiwe kwa dhamana hadi kesi itakapotajwa tena.
Baada ya kutoka kwa dhamana, washitakiwa hao watatakiwa kurejea mahakamani Januari 2 mwakani wakati kesi yao itakapotajwa. Kabla ya tarehe hiyo kuafikiwa na Hakimu Mwankenja, mawakili wa utetezi walijaribu bila mafanikio kuishawishi Mahakama ipange kesi hiyo itajwe Januari 5 mwakani.
Mbali na sharti la kila mmoja kuwasilisha hati za mali zenye thamani ya Sh bilioni 2.9, washitakiwa hao kila mmoja alitakiwa kusalimisha mahakamani hati zake za kusafiria na asitoke nje ya mkoa wa Dar es Salaam bila ya kibali cha Mahakama.
Kwa kupata dhamana jana ilikuwa ni furaha kubwa kwa mawaziri hao waandamizi wa zamani katika serikali ya Awamu ya Tatu, chini ya Rais Benjamin Mkapa. Dhamana hiyo ilitolewa wakati juzi watuhumiwa hao walikuwa wamekwama kuipata kutokana na Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu kusema kwamba haikutoa hati ya watuhumiwa hao kuletwa mahakamani.
Kutokana na sababu hiyo Mahakama hiyo ilishindwa kushughulikia suala la kukamilisha dhamana yao iliyolegezwa masharti na Mahakama Kuu mwishoni mwa wiki iliyopita.
Jaji Njengafibili Mwaikugile wa Mahakama Kuu, Dar es Salaam Ijumaa iliyopita alitoa amri ya kurekebishwa mara moja kwa sharti lililokuwa likiwataka watuhumiwa hao kila mmoja kutoa fedha taslimu Sh bilioni 2.9 ili wapate dhamana badala yake alisema kisheria mtuhumiwa anatakiwa apate dhamana kwa kutoa kiasi cha fedha au kuwasilisha hati ya mali yenye thamani sawa na kiwango hicho.
Baada ya amri hiyo ndipo juzi Jumatatu walipofikishwa Mahakama ya Kisutu ambako waligonga mwamba kwa kuwa Mahakama hiyo haikuwa na taarifa ya kuletwa kwao. Ilisema ilikuwa na taarifa ya kuletwa kwao jana Jumanne.
Hali haikuwa ya kawaida mahakamani hapo jana Jumanne baada ya washitakiwa hao kuletwa na kupata dhamana kwani pilika pilika za watu wa kawaida na wapiga picha wa vyombo mbalimbali za kutaka kushuhudia jinsi wanavyorudi uraiani vilifanya eneo la Mahakama kuwa na vituko vya kukimbia hapa na pale.
Kwa takriban saa moja watu hao na wapiga picha walikimbia kutoka sehemu ya mbele ya Mahakama hadi ya nyuma kutafuta ni sehemu ipi kati ya hizo watakapotokea baada ya kutolewa kwenye chumba cha Mahakama walikopatiwa dhamana.
Hatimaye walitolewa kupitia mlango wa mbele. Patashika ya wapiga picha ilikuwa kubwa na washitakiwa hao walimulikwa na taa za kamera mfululizo kiasi cha Mramba ambaye kipindi chote cha kesi akiwa nje ya Mahakama alikuwa bubu akiwa chini ya ulinzi, jana sauti yake ilisikika kwa mara ya kwanza akiwa huru.
Pigeni zote, pigeni zote, alisema Mramba akiwahimiza wapiga picha kuendelea kupata picha zake zinazomuonyesha anatoka mahakamani baada ya kupata dhamana.
Alikuwa akihimiza hivyo wakati anaelekea kupanda kwenye gari la kifahari lililokuwa limeegeshwa mbele ya lango kuu la Mahakama. Bila shaka gari hilo lilikuwa tayari kumpeleka nyumbani kuungana na familia yake iliyomkosa kwa wiki nzima baada ya kulazimika kulala mapema kila siku akiwa rumande ya Keko.
Kama ilivyokuwa Jumanne ya wiki iliyopita wakati waliposhindwa sharti la kuwasilisha kila mmoja fedha taslimu bilioni 2.9 hivyo kulazimika kwenda Keko, kulikuwa na kundi la watu lililoonyesha hasira za wazi dhidi yao licha ya kuwapo askari na makachero mahakamani hapo.
Wakati Jumanne iliyopita Mramba na Yona walisindikizwa kwa kelele za wezi hao, wezi, jana kila mmoja kwa wakati wake alisindikizwa kwa kelele za mwizi huyo, mwizi huyo, gari lake lilipoondoka kwa kasi katika eneo la Mahakama.
Gari la kwanza kuondoka lilikuwa ni lile lililombeba Yona na la pili lilikuwa lililombeba Mramba na kufuatia na mengine ambayo bila shaka yalikuwa ni ya wana familia wa familia za washitakiwa hao wawili.
Mramba na Yona wote kwa pamoja wameshitakiwa kwa kuibeba kampuni ya Alex Stewart (Assayers) Government Business Corporation ya Washington DC, Marekani ambayo ilikuwa ikifanya kazi ya uhakiki wa mapato ya madini ya dhahabu nchini.
Mawaziri hao wawili Jumanne ya wiki iliyopita walisomewa mashitaka yao na waendesha mashitaka kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kisutu, Hezron Mwankenja, kukiwa na ulinzi mkali wa makachero na askari magereza wenye silaha.
Pamoja na kutoa upendeleo wa kuongeza mkataba wa kampuni hiyo ya Alex Stewart (Assayers) Government Business Corporation, Mramba na Yona wakiwa Waziri wa Fedha na Waziri wa Nishati na Madini, ilidaiwa waliisababishia serikali hasara ya zaidi ya Sh. bilioni 11 kutokana na kusamehe kodi kampuni hiyo kinyume cha sheria.
Makosa hayo yalielezwa mahakamani hapo kutendwa katika kipindi cha mwaka 2002 na mwaka 2007, ambako Mramba aliandaa na kutoa matoleo ya Gazeti la Serikali (GN) yenye namba 423/2003, 424/2003, 497/2004, 498/2004, 377/2005 na 378/2005 ambayo yalilenga kutoa msamaha wa kodi kwa Alex Stewart (Assayers) Government BC uliofikia kiwango cha Sh 11,752,350,148/- bila kuzingatia sheria ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Kwa mamlaka yao na nafasi zao, Mramba na Yona walidaiwa mahakamani hapo kwamba bila kuzingatia wajibu wao waliokabidhiwa na serikali waliingia mkataba ulioisababishia serikali hasara ya Sh 11,752,350,148/- kutokana na kampuni hiyo ya uhakiki wa dhahabu.
Ilidaiwa kwamba Mramba kupitia matoleo mbalimbali ya Gazeti la Serikali amewezesha kutolewa kwa msamaha wa kodi ya mapato iliyopaswa kulipwa na kampuni hiyo ya Alex Stewart kinyume cha sheria ya Kodi ya Mapato.
Kwa mujibu wa maelezo ya waendesha mashitaka hao, Mramba anadaiwa alitumia vibaya madaraka yake kwa kudharau ushauri wa TRA waliomtaka kutokubali kutoa msamaha wa kodi ya mapato kwa kampuni hiyo ya kigeni ambayo ililalamikiwa sana kwa kumega mapato ya dhahabu nchini.
Mawaziri hao wa zamani walituhumiwa pia kudharau maelekezo ya kamati ya ushauri ya serikali ambayo ilipendekeza kupelekwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali mkataba wa Alex Stewarts na badala yake waliongeza muda wa mkataba wa kampuni hiyo bila kuzingatia suala la kupitia upya ada iliyokuwa ikilipwa kwa kampuni hiyo na hivyo kuiingizia serikali hasara.
Katika kuongeza mkataba huo, Mramba na Yona walidaiwa kutumia vibaya madaraka yao kwa kumshirikisha Dk. Enrique Segura wa Alex Stewarts katika kuingia naye mkataba wa nyongeza ya miaka miwili kuanzia Juni 14, 2005 hadi Juni 23, 2007 bila kuzingatia Sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2002 na Sheria ya Madini ya mwaka 2002.
Mashitaka dhidi ya watuhumiwa hao yalifuatia kibali kilichotolewa na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) Elieza Feleshi kutoa kibali kwamba viongozi hao waandamizi wametumia vibaya madaraka yao na wamesababisha hasara kwa mamlaka husika.