KLABU za Gor Mahia inayoshiriki Ligi Kuu ya Kenya na St. George ya Ethiopia, zinatajwa kumwania mshambuliaji wa kimataifa wa Simba kutoka Burundi, Laudit Mavugo, imeelezwa.
Hata hivyo, Akizungumza na gazeti hili jana, Kaimu Rais wa Simba, Salim Abdallah "Try Again" amesema kuwa hakuna mchezaji hata mmoja atakayeachwa na hiyo inatokana na ripoti ya kiufundi waliyokabidhiwa na Kocha Mkuu, Joseph Omog.
Salim alisema jana kuwa chini ya uongozi wake, hakutakuwa na kiongozi atakayesajili mchezaji au atakayependekeza nyota kuachwa, kwa sababu jukumu hilo liko chini ya Omog na wasaidizi wake tu.
"Kila kitu kinaendeshwa kwa kufuata kanuni na taratibu, Simba ni taasisi na ni kubwa kuliko mchezaji au kiongozi, ni lazima hilo liheshimiwe," alisema kiongozi huyo ambaye anakaimu nafasi iliyoachwa na Evans Aveva, anatuhumiwa kutumia vibaya fedha za klabu.
Taarifa zilizopatikana jijini zinasema kuwa kuna mazungumzo yasiyo rasmi yanaendelea na lengo la kufanya hivyo ni kutaka kushawishi mshambuliaji huyo aachwe kwa ajili ya kukwepa kulipa ada ya uhamisho kwa sababu mshambuliaji huyo bado ana mkataba na Simba.
"Mimi najua St. George ndiyo wanamtaka, na hawakuanza sasa, ila wanaonyesha wanataka kumsajili kupitia mlango wa nyuma, na hili haliwezekani," alisema kiongozi mmoja wa Simba.
Wakati huo huo mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya Simba na Lupuli FC kutoka Iringa iliyopangwa kufanyika kwenye Uwanja wa Azam Complex sasa itachezwa kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania, Boniface Wambura, alisema uamuzi wa kuirejesha mechi hiyo kwenye Uwanja wa Uhuru umetokana na kupata taarifa kuwa uwanja huo utakuwa huru siku hiyo huku akiongeza kuwa mechi kati ya Yanga dhidi ya Prisons itachezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi jijini.
Chanzo: Nipashe