SoC01 Mawazo barabara yanatoka wapi?

SoC01 Mawazo barabara yanatoka wapi?

Stories of Change - 2021 Competition

Jo Africa Tz

Member
Joined
Jul 23, 2019
Posts
10
Reaction score
10
Mawazo barabara yanatoka wapi? Jee yanaangukia kutoka mbinguni? La. Jee, yamo akilini tangu mtu kuzaliwa? La. Mawazo barabara yanatokana na vitendo vya mtu katika jamii tu. Mawazo barabara yanatokana na aina tatu za vitendo katika jamii:

1. Mapigano ya kuendeleza uchumi,
2. Mapigano ya kitabaka na
3. Majaribio ya kisayansi.

Ni hali ya mtu katika jamii ndio inayoamua fikra zake. Mara fikra barabara zinazowakilisha tabaka lililoendelea mbele zinapokamatwa na umma, basi fikra hizi hugeuka kuwa nguvu hasa zinazoibadilisha jamii na kuibadilisha dunia.

Katika vitendo vya kijamii, binadamu wanafanya kila aina ya mapigano na wanajipatia maarifa mengi kutokana na mafanikio yao na pia kushindwa kwao. Mambo mengi ya ulimwengu unaotuzunguka yanaingia kwenye akili ya binadamu kwa njia tano za fahamu:

1. Macho,
2. Masikio,
3. Pua,
4. Ulimi na
5. Mwili (uliofunikwa na ngozi).

Mwanzoni, ujuzi ni wa kuhisi. Baada ya kupatikana ujuzi wa kuhisi, panapatikana mchupo kuendea ujuzi wa kuwaza, na fikra zinapatikana. Huu ni mwenendo mmoja wa kulifahamu jambo. Hii ni daraja ya kwanza ambayo inatokana na vitu hasa (objective matter) kuendea ufahamu wa mtu, yaani kutokana na kuwepo kwa vitu (existence) kuendea fikra.

Katika daraja hii bado haiwezekani kuthibitisha kama ufahamu au fikra za mtu (pamoja na nadharia, siasa, mapigano au njia) zinamathilisha vyema kanuni za ulimwengu unaotuzunguka au la, kwani bado haiwezekani kuhakikisha kama ufahamu na fikra hizo ni barabara au la.

Daraja la pili ni ile inayoanza na ufahamu kurejea katika vitu, kutoka fikra kurejea kuwepo kwa vitu, ambamo ujuzi uliopatikana katika daraja ya kwanza unatumiwa katika vitendo vya mtu katika jamii ili kuhakikisha kama nadharia, siasa, mipango, njia na kadhalika za mtu zinapata mafanikio yaliyotumainiwa. Kwa jumla, zile fikra zilizofanikiwa ni sahihi, na zile zilizofeli si sahihi; jambo hili ni kweli hasa katika mapigano ya binadamu na maumbile.

Ujuzi wa binadamu unafanya mchupo mwengine kwa kupitia majaribio ya vitendo. Umuhimu wa mchupo huu ni mkubwa kuliko ule wa kabla. Kwani ni mchupo huu peke yake ndio unaoweza kuthibitisha usahihi au la wa mchupo wa kwanza, yaani fikra, nadharia, siasa, mipango, njia na kadhalika zilizotengenezwa katika mwenendo wa kumathilisha ulimwengu unaotuzunguka. Hapana njia yo yote nyengineo ya kuupima ukweli.

Mara nyingi ujuzi barabara huweza kupatikana baada ya kurudia rudia kwa mara kadha mwenendo wa kutoka vitu kuendea ufahamu na kurejea tena kwenye vitu, yaani kutoka vitendo kuendea ujuzi na kurejea tena kwenye vitendo. Hii ndiyo nadharia ya uyakinifu wa upembuzi kuhusu ujuzi.

Yeyote anayetaka kukijua kitu hana njia ya kufanya hivyo isipokuwa kufanya maingiliano na kitu hicho yaani kwa kuishi (kutenda) katika mastakimu yake.

Hivyo ili kupata mawazo barabara, kwanza pata hisia, halafu waza kuhusu hisia hizo ili kupata fikra, halafu geuza fikra hizo kuwa vitu kwa kufanya kwa vitendo na hapa ndipo utapata ujuzi, na ukishapata ujuzi rejea tena kwenye vitendo ili kupata vitu na hapo ndipo utapata mawazo barabara baada ya kurudia rudia kwa mara kadhaa ili kupata uhakika.

Kila hisia igeuze kuwa fikra, na kila fikra igeuze kuwa kitu kwa kufanya kwa vitendo, na kila kitendo kirudiwe ili kupata ujuzi. Fikra za kusoma kwenye vitabu au za kufundishwa darasani tu havijawahi kuzalisha watu wa maana katika dunia hii. Kama mwenendo mzima wa kihisia, kifikra na kivitendo utafanywa na wewe, basi utakuwa wa kipekee katika historia ya ulimwengu huu.

Elimu ya kweli ni ile inayomfanya mtu kuwa na uwezo wa kugeuza hisia zake mwenyewe kuwa fikra na kugeuza fikra hizo kuwa vitu kwa vitendo ili kupata ujuzi na si kukaririshwa vitu ambavyo haviwafanyi kuwa wagunduzi bali wasomi tu wa mawazo ya watu.

Kila kinachomkuta mtu katika maisha ni muhimu licha ya mabaya yanayoletwa na kitu hicho. Umuhimu utakuja endapo mtu ataamua kutengeneza fikra na kugeuza fikra hizo kuwa vitu kwa kufanya kwa vitendo. Je, unayo mawazo barabara?
_________________
GROUP%20TEKU.jpg
 
Upvote 1
Back
Top Bottom