Sildenafil Citrate
JF-Expert Member
- Jan 29, 2021
- 577
- 2,595
Picha: Maxence Melo
Mkurugenzi Mtendaji wa Jamiiforums Maxence Melo amesema taasisi hiyo kwa kushirikiana na Wizara ya Habari na Mawasiliano wapo kwenye hatua za mwisho za kuiandikia barua kampuni ya Google ili iweze kuitambua lugha ya Kiswahili katika utoaji wa maudhui.
Amesema kwa sasa waandaji wa maudhui kwa lugha ya Kiswahili hawapati malipo ya kutosha ikilinganishwa na lugha zingine hasa Kiingereza kwa kuwa haipo kwenye orodha ya lugha zilizo kwenye mpango wa kulipiwa matangazo ya mtandaoni maarufu kama Google ads.
Melo ameyasema haya leo Septemba 16, 2022 wakati wa Warsha ya Kuhamasisha Uandaaji, na Uzalishaji wa Maudhui ya Ndani iliyoandaliwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ambapo Waziri wa Habari na Mawasiliano Nape Nnauye alikuwa mgeni rasmi.
Katika hatua nyingine, ameshauri uwepo wa ubunifu katika kutengeneza maudhui yenye asili na upekee bila kunakili kutoka sehemu zingine kwani itawafanya wahusika wakose haki zao.
Katika mazingira ya sasa yenye ushindani mkubwa, ameonesha wasiwasi wake kuwa kitendo cha Serikali kuamua kuwalipa watoa maudhui kitasababisha kufa kwa ubunifu kwa kuwa watu wanapaswa kwanza wao wenyewe kutoka nje ya maeneo yanayo wafanya wajisikie huru na salama (comfort zone).
“Kabla hamjaanza kuisumbua Serikali kuwalipa kwa maudhui (content) unayotengeneza, jiulize kwanza umeleta kitu kipi chenye tija ambacho kina thamani ya wewe kulipwa” amesema.
Ametolea mfano wa Taasisi ya Jamii Forums kuwa haijafanikiwa kwenda nje ya mipaka ya Tanzania kwa kuwa ina chaneli ya Youtube, au kwa kuwa inapata matangazo ya biashara bali upekee na thamani ya maudhui yake ndiyo vimefanikisha jambo hilo kutokea.