ben martin
New Member
- Aug 2, 2022
- 3
- 2
MAZINGIRA NI UHAI WETU
Mazingira yanatengenzwa na vitu vingi sana. Vitu hivyo vinaonekana na vingine havionekani, vipo vilivyo hai na vingine haviko hai. Mfano wa vitu hivyo ni pamoja uoto ukihusisha majani vichaka, miti na misitu minene. Pia kuna hewa katika anga mfano Oksijeni, Kaboni, Nitrojeni, Salfa n.k. Vitu vingine ni vyanzo vya maji kama mito, maziwa, bahari, chemchem n.k. bila kusahau ardhi, miamba, wanyama wa kila aina, wadudu wa kila aina na vitu vitu vingine vingi vya kila aina katika uso wa dunia.Kwa ujumla mazingira maana yake ni vitu vyote vinavyomzunguka binadamu vionekavyo na visivyoonekana, vilivyo hai na visivyo hai. Kwa kuangalia na kutathmini vitu vyote hivi, Mungu aliviumba ili vitupatie uhai sisi pamoja na viumbe wengine katika uso wa dunia.
Kama ambavyo uhai wetu unategemea mazingira hivyo hatuna budi kuyatunza na kuayalinda ili yaweze kututunza na sisi. Kutokana na mazingira tunapata mahitaji yetu ya kila siku kama chakula kitokanacho na mimea mbalimbali, nyama inayotokana na wanyama tofautofauti wanaoliwa pamoja na samaki. Pia mimea mingi hutumika kutengeneza dawa za aina tofautitofauti ili kutibu magonjwa mbalimbali yanayomsibu mwanadamu.
Aidha malighafi nyingi zinapatikana kwenye mazingira yetu. Mfano mchanga, mawe, udongo n.k hutokana na miamba mbalimbali. Pia magogo na mbao za kila aina hutokana na miti iliyopo katika mazingira yetu ambavyo vyote kwa pamoja hutuwezesha kujengea makazi yetu. Madini ya kila aina yanapatikana kwenye ardhi. Mfano Dhahabu, Almasi, Shaba, Rubi, Tanzanite n.k. Yote haya hutumika kutengeneza vito na vitu mbalimbali vinavyohitajika katika maisha yetu, kama mapambo ya mwili na nyumba, kutengeneza mashine na teknolojia mbalimbali.
Hivyo basi kulingana na faida nyingi zitokanazo na mazingira, binadamu na viumbe hai wengine tunaendelea kuwa hai na kustawi. Kukithiri kwa uharibifu wa mazingira kunaweka uhai na ustawi wetu hatarini zaidi hivyo kuifanya dunia isiendelee kuwa sehemu salama.
Uharibifu wa mazingira umesababishwa na biandamu mwenyewe kwa kujihusisha na shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii. Shughuli hizi zimepelekea uharibifu wa mazingira. Mfano kukata miti na misitu kwa ajili ya kuvuna mbao, magogo, na mkaa. Pamoja na hayo shughuli za uchimbaji wa madini, viwanda na usafirishaji wa majini na nchi kavu zote hizi zimehusika kwa kiasi kikubwa kuharibu mazingira.
Shughuli hizi zimepelekea kuongezeka kwa majanga mbalimbali ya kidunia yanayotokana na uharibifu wa mazigira. Mfano ongezeko la joto katika uso wa dunia( Global Warming), mmomonyoko wa udongo, ukame, mafuriko n.k vyote hivi vinasababishwa na ukataji wa miti na misitu hovyo bila kupanda mingine. Uchomaji mkaa, gesi chafu kutoka viwandani, nyenzo za usafirishaji kama treni, magari, meli na ndege. Vyote hivi huzalisha hewa chafu kama kaboni, sulfadioksaidi,methane n.k ambazo zimerundikana katika tabaka la hewa hivyo kusababisha ongezeko la joto duniani.
Ongezeko la joto katika uso wadunia limesababisha madhara mengi sana mfano kuyeyuka kwa barafu katika maeneo yayolifunikwa na barafu kama milima mirefu zaidi mfano mlima Kilimanjaro barafu yake imepungua kutokana na kuyeyuka. Pia barafu inapungua sana katika ncha za dunia za kusini na kaskazini. Kuyeyuka kwa barafu kumeleteleza kutokea kwa mafuriko katika maeneo mbalimbali na kuongezeka kwa kina cha maji katika bahari na maziwa.
Aidha ongezeko la joto limesababisha kutokea kwa moto wa nyika katika maeneo mabalimbali katika uso wa dunia hasa huko Ulaya, Asia na Amerika, ambapo watu wengi aidha wamekufa, kuhama makazi au kupoteza mali zao. Mbali na hayo pia misitu inateketea , wanyama wanakufa na wengine kuhama kabisa kutoka maeneo hayo hatarishi hivyo baadhi ya nchi kupoteza vivutio vya utalii.
Hata hivyo uharibifu na uchafuzi wa mazingira umesabaisha kuibuka kwa magojwa mengi ikiwa ni pamoja na kansa ya ngozi kutokana na joto kali,Monkey pox kutokana na wanyama kuvamia makazi na mashamba ya wanadamu na kuchangamana nao kwa namna moja au nyingine.
Kwa ujumla madhara ya uharibifu wa mazingira ni mengi mno ukilinganisha na nyakati zilizopita. Siku hizi uzalishaji katika kilimo umekuwa hauridhishi kutokana na kupungua kwa rutuba kwenye udongo, mpaka inawalazimu wakulima kuongeza mbolea za viwandani na madawa mengine ili angalau wapate mavuno mazuri.
Kutokana na madhara hayo sisi kama binadamu tunapaswa kufanya jambo ili kulinda mazingira yetu pamoja na uhai wetu na wa viumbe wengine. Je tufanye nini ili kulinda uhai wetu?
Kwa swali hilo kila mmoja wetu aliye hai katika uso huu wa dunia anapaswa kutafakari kwa kina na kupata suluhu ya kuepukana na madhara yatokanayo na uchafuzi na uharibifu wa mazingira.
Ingawa kuna watu na mataifa mabalimbali duniani walishakaa na ujadili namna ya kuyalinda mazingira kwa kutunga sheria za mazingira na mashirika na mbalimbali duniani yakaundwa kama UNEP( United Nations Environmental Programme) na kwa Tanzania tukaunda NEMC (National Environment Management Council) na mengine mengi ili kupambana na kuendeleza harakati za utunzaji wa mazingira. Lakini mbali na hayo yote bado uchafuzi na uharibifu unaendelea hivyo kuifanya dunia kuendelea kuwa hatarini.
Ushauri wangu
1. Sheria za mazingira zirejelewe na mpya zitungwe kuwalazimisha watu kutunza mazingira kwa kuacha kutupa taka hovyo kwenye mazingira na kupanda miti kuanzia ngazi ya familia, mtaa, wilaya na taifa. Mfano sheria itungwe kuilazimisha kila familia kupanda miti isiyopungua mitano na iongezwe kulingana na ukubwa wa eneo la familia husika.
2. Serikali za dunia ziingie gharama, kuvumbua, kutengeneza na kununua teknolojia zitakazowezesha kutunza, kuchakata, na kusindika taka zote hatari zinazozalishwa kwenye mazingira.
3. Wazalishaji wote wa nishati rafiki wa mazingira mfano gesi asilia, nishati za jua, upepo na maji wapewe ruzuku, mikopo rahisi na serikali ziweke nguvu na kutoa motisha zaidi na kuhakikisha wazalishaji wanakidhi mahitaji ya dunia.
4. Nishati rafiki wa mazingira ziuzwe kwa bei nafuu zaidi ili kuwawezesha watumiaji kumudu.mfano gesi ya kupikia iuzwe kwa bei rahisi zaidi ilikuwawezesha wtumiaji kuepukana na matumizi ya kuni na mkaa ambavyo ni vyanzo vikuu zaidi vya ukataji wa miti na misitu.
Kwa kuhitimisha naweza kusema kuwa Mungu alipoiumba dunia aliifanya eneo salama na paradiso kwa ajili ya viumbe wake. Sisi tunaiharibu paradiso yetu, tunaitengezeza kuwa jehanamu itakayotuangamiza wote. Tubadilike, tuache kuharibu mazingira, tujifunze, tutafute njia bora zaidi za kuilinda dunia yetu na sisi kujilinda wenyewe. "TUIFANYE DUNIA KUWA KIJANI ZAIDI".
Upvote
3