richiemc6
New Member
- Jul 16, 2021
- 1
- 2
MAZINGIRA SIO MGODI
Ikisiri (Abstract)
Uwezo wa mazingira wa kutimiza mahitaji ya mwanadamu, wanyama na mimea unaendelea kupungua. Kutoweka kwa viumbe, mimea na mabadiliko ya hali ya hewa na tabia nchi ni viashiria vilivyo dhahiri katika upungufu wa uwezo wake. Shughuli za kibinadamu haswa zile za kimaendeleo zikiongozwa na utekelezaji wa sera za uchumi wa viwanda zimepelekea hali ya swala la “uchimbaji mazingira.” Ikisiri (Abstract)
Makala hii inadhamiria kutafsiri na kudadavua dhana ya uchimbaji mazingira katika nchi zilizoendelea na zile zinazoendelea kama Tanzania. Dhumuni nyongeza la hii makala ni kujaribu kuonyesha na kutoa ushauri juu ya uchimbaji mazingira nchini Tanzania na kwa namna gani raia wa nchi wanaweza kukabiliana na athari za uchimbaji huo haswa ukitegemea kuwa asilimia kubwa ya nguvu kazi ya nchi inajihusisha na kilimo.
Utangulizi
Wengi wetu tunachukulia swala la athari kwa mazingira “poa,” kana kwamba mazingira ni kwa ajili ya kutimiza mahitaji yetu kwanza alafu ndiyo mahitaji ya viumbe vinginevyo na vizazi vijavyo vitafuata. Shughuli za kibinadamu za maendeleo kuanzia nusu ya karne ya 20 na kuendelea zimekuwa zikitumia mazingira kama mgodi usiyoisha madini yake. Kwa kuyatumia mazingira kama mgodi, madini yake kama vile hewa, vyanzo vya maji, rutuba ya ardhi, uwepo wa mimea, viumbe na uoto asilia vinaendelea kuathiriwa kwa kiasi kikubwa na kupelekea kupungua kwa uwezo wa mazingira kutoa madini haya kwa kiwango stahiki.
Kwanza kabisa, ifahamike na kueleweka kuwa hakuna mgodi usiyoisha madini. Kwa mfano, Idara ya Utafiti ya Statista ilitoa ripoti mwaka 2013 ikionyesha kuwa mgodi wa shaba unaweza ukavunwa kwa miaka 5-70 tu, huku ule wa chuma ukivunwa kwa miaka 6-24, na wa almasi ukitoa madini hayo kwa miaka takribani 4-27 pekee. Vivyo hivyo, katika tafiti ya British Petroleum ya mwaka 2013, ilikadiriwa kuwa kiasi cha mafuta ghafi yaliyoko ardhini ni mapipa trilioni 1.688 ambayo yatamalizwa kuchimbwa baada ya takribani miaka 54.
Hivyo basi ifikapo mwaka 2067, kama hapatokuwa na mbadala wa mafuta, tutaishia kupaki magari yetu nyumbani na kurejea usafiri wa miguu na wanyama. Mwanadamu akiendelea kuyatumia mazingira kama mgodi, uwezo wa mazingira kumuhudumia yatafika ukingoni.
Tofauti na migodi tuliyoizoea, mazingira yana uwezo wa kuzalisha huku yakitumika lakini tukiyatumia kwa mantiki ya “uchimbaji mazingira,” tutakuwa tunaelekea kusikojulikana. Yamkini tumeshasikia kuwa mahitaji ya kawaida ya mwanadamu ni endelevu, tukiongeza hapo mahitaji ya kimaendeleo ambayo ni maradufu na zaidi ya yale ya kawaida, basi tunayapa presha zaidi mazingira. Kwa kawaida, mgodi ukichimbwa mpaka mwisho, wachimbaji huhamia kwenye mgodi mwingine au hutafuta shughuli nyingine ya kufanya. Je, ‘tukiyachimba mazingira’ mpaka kuyamaliza, tutahamia sayari gani? Kipengele kifuatacho kinaeleza kuhusu dhana ya uchimbaji mazingira.
Dhana ya Uchimbaji Mazingira
Uchimbaji mazingira unaweza kufafanuliwa kama matumizi ya rasilimali za mazingira haswa kwa shughuli za kibinadamu za kujikimu na kimaendeleo pasipo kuzingatia matumizi wala mahitaji ya viumbe wengine pamoja na vizazi vijavyo vya wanadamu. Kama ambavyo uchimbaji wa mgodi usiyozingatia kifuatacho baada ya akiba ya madini kuisha, vivyo ndivyo uchimbaji mazingira usivyochukua tahadhari za mbeleni pale ambapo athari kwa mazingira zitakuwa kubwa sana.
Japokuwa mwanadamu mamboleo ana silaha ya teknolojia katika kupambana na uchimbaji mazingira, bado anaendelea kupuuza matumizi ya silaha hii. Hili linadhihirika kwa kuendelea kutegemea mafuta ghafi kama chanzo cha umeme wakati nguvu za umeme wa jua na upepo zipo bwerere. Nchi zilizoendelea zinajitahidi kupunguza na hatimaye kusitisha athari za ‘uchimbaji mazingira’ ulizozifanya kuanzia mwaka 1950 kupitia kutumia tena (reuse), kurejea bidhaa walizokwisha zitumia (recycle), na kubadili vyanzo vyao vya umeme wa magari na viwanda (using greener energy sources). Utekelezaji ndiyo unaendelea kuwa changamoto kutokana na hitaji la kuendelea mbele zaidi na kujiimarisha kiuchumi.
Sababu za Uchimbaji Mazingira
Kuna sababu kama mbili za uchimbaji mazingira zitakazoelezewa kwa kina nazo ni: tabia ya ubinafsi na tamaduni ya matumizi.
Kuna tabia fulani ya mwanadamu ambayo huambatana na kujua kuwa kitu fulani kina mwisho wake. Tabia hii ni ya ‘kukimaliza kile kitu kwa haraka zaidi’ badala ya kukitunza kwa ajili ya matumizi ya ulazima au matumizi ya mtu mwingine. Kama ilivyo kwenye migodi ambapo makampuni ya uchimbaji hutafuta mbinu za kuchimba kwa haraka zaidi ili kunufaika haraka, kwenye mazingira mwanadamu hutumia njia zozote kuendelea na kunufaika kabla hajafika mwisho wake (kifo).
Katika kutafuta maendeleo, viwanda vimekuwa chanzo kikubwa kwenye kuyafanya mazingira kuwa kama mgodi. Uchumi wa viwanda haswa baada ya Vita Vikuu vya Dunia II ulijikita katika kufufua chumi za Ulaya, Urusi, Japani na Marekani ambazo ziliathirika na vita hiyo kwa kiasi kikubwa. Wakati nchi za barani Asia kama China, Korea ya Kusini, Malaysia, na Taiwan zikijiimarisha kwenye uchumi wa viwanda kuanzia miaka ya 1970, uchumi wa aina hii umeleta athari kubwa sana kwa mazingira kiasi cha kupelekea mabadiliko ya zama kutoka zama za Holocene mpaka zama mpya ya Anthropocene (Zama za mwanadamu mpya-tafsiri kutoka maneno ya Kigiriki).
Zama za Anthropocene kijiolojia zinatafsiriwa kama zama zilizoanza aidha mwaka 1800 wakati wa mapinduzi ya awali ya viwanda au mwaka 1950 ambapo palitokea kasi ya ongezeko la shughuli za kibinadamu ikiwemo mapinduzi ya pili ya viwanda na majaribio ya silaha za kinyuklia. Zama hizi za mwanadamu mpya zinaonyesha jinsi gani shughuli zake zimepelekea mabadiliko ya viungo vya hewa, udongo na ikolojia kwa ujumla. Kama vile mgodi unavyobadili muundo wa mandhari ya eneo husika kwa kulibugudhi, ndivyo mwanadamu mamboleo (new/neo man) anavyoyabugudhi mazingira kwa shughuli zake za maendeleo haswa viwanda.
Utamaduni wa viwanda huambatana na utamaduni wa utumiaji/matumizi (consumerism) ambapo viwanda na wateja, vyote haviridhiki. Kiwanda kinatafuta njia ya kuzalisha zaidi kila kukicha huku mteja akitafuta vitu vipya kila kukipambazuka. Tuchukulie mfano kwa wiwanda vya simu kama Samsung na iPhone ambavyo huzalisha matoleo mapya ya bidhaa kila wakati kwa ajili ya wateja wao.
Nchi za wenzetu huwa tunashuhudia wateja wakilala nje ya maduka ya simu wakingoja kwa hamu matoleo mapya ya vifaa hivyo vya kisasa ili mradi tu waendane na ile dhana ya usasa au upya. Yamkini kwenye toleo jipya la simu vinaongezeka vitu vichache sana lakini kutokana ili kuendana na mwenendo (trend), mwanadamu wa kisasa naye hataki apitwe.
Utamaduni wa utumiaji (consumerism) hauendani na uwezo za mazingira kuzalisha kwa ajili ya mahitaji yasiyo kifani ya mwanadamu. Vile vile mazingira huwahudumia viumbe vingine ambavyo viwekuwa vikitoweka kutokana na athari za mazingira zinazosababishwa na mwanadamu.
Tofauti na sisi, viumbe vinginevyo havijabadili mifumo yao ya kuishi wala mahusiano na mazingira. Kwa viumbe hivi mazingira siyo mgodi bali ni mlezi wa kuheshimiwa na kutokubugudhiwa. Japo viumbe wengine wameendelea kuyaheshimu na kuyathamini mazingira, shughuli za binadamu zilizopelekea ‘uchimbaji mazingira’ zimesababisha viumbe hivi kuwa kama kafara inayotumika kugharamikia uchafuzi wa mazingira unaoletwa na mwanadamu.
Uchimbaji Mazingira Nchini Tanzania
Tanzania kama zilivyo nchi zote zinazoendelea, matamanio ya kufikia viwango vya maendeleo vya nchi za Magharibi ni kipaumbele. Kupitia nchi tajiri, Tanzania imejifunza kuwa uchumi wa viwanda ndiyo njia ya kufikia maendeleo. Sera za kufanikisha uchumi wa viwanda zilizoanza kutekelezwa kwa kasi zaidi chini ya aliyekuwa Raisi wa awamu ya tano, Dkt. John Pombe Magufuli zinaendelezwa na mrithi wake Raisi Samia Suluhu Hassan. Utekelezaji wa sera hizi nchini Tanzania ni wa tofauti haswa ukizingatia kuwa ni nchi inayotegemea utalii vile vile na hivyo kulazimika kuwa na jicho la uangalifu zaidi kwenye swala la mazingira.
Kutokuwa na viwanda vingi kwa nchi zinazoendelea kumefanya nchi hizi zisiwe za kisasa kama zile za Magharibi na hivyo hali na athari za ‘uchimbaji mazingira’ kuwa ndogo ukilinganisha na nchi za Magharibi. Wanadamu wa hizi nchi zinazoendelea huzingatia mazingira kwa kiasi kikubwa japo huathirika na mabadiliko ya hali ya hewa, mabadiliko ya tabia nchi ambayo kwa kiasi kikubwa husababishwa na chumi zilizoendelea.
Hii haimaanishi kwamba uchimbaji mazingira haupo Tanzania, upo na unapatikana kupitia ukataji miti kwa ajili ya mkaa na utengenezaji wa samani, matumizi ya mafuta kwenye vyombo vya usafiri na viwanda vichache vipatikanavyo nchini.
Hali duni ya raia wengi wa kitanzania kumesaidia kupunguza tamaduni ya utumiaji (consumerism) ambapo nguo na viatu rejea (mitumba) ambayo huagizwa na hutumika kwa wingi kumepelekea kutokuwepo kwa idadi kubwa ya viwanda vikubwa vya nguo nchini au hata viwanda vya kuchakata bidhaa za nguo kama vile pamba ambayo hulimwa nchini. Raia wa Kitanzania sio wa mamboleo kama wale wa Ulaya, Japani, Marekani, Kanada na Australia kutokana na hali ya chini ya kiuchumi ambayo inawafanya wasiwe na tamaduni ya kutumia (consumerism) kwa kiasi kikubwa.
Kiwango cha ujuzi, uthubutu pamoja na mitaji ya raia wa Kitanzania walio wengi hairidhishi na hivyo kupelekea kasi ndogo kwenye uanzishwaji wa viwanda nchini. Japo kuwa haya sio mazuri kwenye swala zima la kupiga hatua za kimaendeleo kupitia uchumi wa viwanda, kwenye swala la uchimbaji mazingira yamekuwa tumaini.
Uhitaji uliyokithiri wa malighafi kwa ajili ya kulisha viwanda nchini Tanzania sio kama ule wa uliopo kwenye nchi zilizoendelea au zile ambazo zinaendelea kwa kasi. Hii hali imepelekea kuwepo kwa upatikanaji wa uoto asilia kwa kiasi kikubwa nchini. Lakini, bado athari zitokanazo na uchimbaji mazingira ziliotokea awali na ambazo zinaendelea kutokea zinazikumba nchini zinazoendelea kama Tanzania.
Kwa kuwa raia wa nchini wana mtazamo kuwa wao huchangia kwa asilimia kidogo sana katika athari hizo, muitikio wa utunzaji na kuyalea mazingira umekuwa mdogo. Ni kama vile raia wa nchi zinazoendelea wanakalia kimya swala la uchimbaji mazingira unaosababishwa kwa kiasi kikubwa na nchi zilizoendelea, huku nchi zinazoendelea zikikumbwa na athari za uchimbaji huo bila kubaguliwa.
Waathirika wa Uchimbaji Mazingira Tanzania
Yamkini hawachangii sana katika kuyaathiri mazingira, lakini wakulima ni wahanga wakubwa wa swala la 'mabadiliko ya tabia nchi,’ ambalo hujidhihirisha katika mabadiliko ya misimu pamoja na kiasi cha mvua ambayo hutegemewa na takribani asilimia 60 ya nguvu kazi ya Tanzania ambayo unapatikana kwenye sekta ya kilimo. Athari pia zimedhihirika kwenye udongo ambao unaendelea kupoteza rutuba na hivyo kumlazimu mkulima kuingia gharama kununua mbegu stahimilivu zaidi pamoja na pembejeo kila mwaka.
Japo kundi la wakulima linaonekana “kuisoma namba” zaidi, muitikio wao kwenye utunzaji wa mazingira sio wa kuridhisha. Unaweza kutafsiri muitikio wao kama uchimbaji mazingira wa kifikra ambao wakulima wanaufanya kwa kukalia kimya au kuchukulia mabadiliko ya tabia nchi kama sehemu ya changamoto za kila siku badala ya changamoto ambayo ina uwezo wa kuathiri sekta nzima ya upatikanaji wa chakula kwa sasa na hata baadae.
Uchimbaji mazingira wa kifikra una sifa nyingi kama kutokuwa na muitikio wa kushiriki kampeni za utunzaji, midahalo, kukalia kimya au kufumbia mambo uchafuzi wa mazingira unaotokea eneo lolote, pamoja na kuchukulia poa athari za uchimbaji mazingira kwa kuamini kwamba ni ‘Mpango wa Mungu’. Mtanzania wa kawaida huegemea sekta ya imani pale ambapo anapata changamoto ndogo au kubwa au hata pale anapoona uvivu kushupalia jambo.
Tunachukulia vitu poa, kwa mazoea mfano jua kuwa kali tunaona kama ni hali ya kawaida katika mipango ya Mungu, angali ni sisi wenyewe ndiyo tunaleta athari hizi aidha kupitia viwanda au kupitia kuchukulia poa athari za uchimbaji mazingira badala la kutekeleza mambo kama upandaji miti kwa wingi kwenye maeneo ya makazi, haswa mijini. Wakati ambapo nchi zilizoendelea zimepelekea uchimbaji mazingira kwa vitendo, nchi zinazoendelea kama Tanzania zinaongezea uchimbaji huo kwa nadharia ya kuchukulia poa au kawaida swala hili.
Hitimisho na Mapendekezo
Mazingira yamekuwa yakitumika kama mgodi, ndiyo maana leo hii tunazungumzia athari za mabadiliko ya hali ya hewa na tabia nchi, kutoweka kwa viumbe na uoto asilia, kuongezeka kwa matukio ya misitu kuungua n.k. Uchimbaji mazingira wa kifikra na matendo ni visababishi na inatupasa kuchukulia kuwa visababishi vyote viwili ni hatari.
Kwa mtazamo huu itasaidia kujumuisha raia wa nchi zinazoendelea kwenye mapambano dhidi ya uchimbaji mazingira pamoja na athari zake. Tukiendelea kuyatumia mazingira kama mgodi, uwezo wake wa kutoa madini kama hewa na maji safi, ardhi yenye rutuba, miti, mimea na viumbe kama nyuki ambavyo husaidia kusambaza mbegu za mimea na kutupatia asali utaendelea kupungua.
Jinsi upungufu huu unavyokithiri ndivyo jinsi tunavyojiweka hatarini pamoja na kuviweka viumbe na mimea mingi zaidi hatari kutoweka maana bila mazingira stahiki hakuna mwanadamu wala kiumbe kitakachosalimika. Maendeleo ni matamanio mazuri lakini maendeleo kupitia uchimbaji mazingira sio sahihi.
Upvote
2