Mohamed Said
JF-Expert Member
- Nov 2, 2008
- 21,967
- 32,074
JULIUS NYERERE ALIPOSIMAMA JUKWAANI KUDAI UHURU WA TANGANYIKA 1955
Nimezungumza na Maggid Mjengwa kuhusu historia ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kama ilivyoandikwa.
Hebu turudi nyuma hadi mwaka wa 1955 tumwangalia Nyerere kijana mdogo yuko Mnazi Mmoja anahutubia wananchi kuhusu uhuru:
"Katika mikutano ya TANU ile miaka ya mwanzoni walikuwa wanajenga kijukwaa kidogo cha miti.
Mikutano hii ikifanyika Mnazi Mmoja karibu na Kidongo Chekundu In Shaa Allah nitaweka picha yake.
Kabla ya mkutano pale kwenye jukwaa kulikuwa na gramophone inapiga nyimbo ya Frank Humplink inayosema, ''Tanganyika ikichakaruka Kenya na Uganda zitaumana.''
Nyimbo hii ikawa kama ndiyo nyimbo ya TANU na Waingereza walipoona nyimbo hii imependwa inaimbwa mitaani wananchi wakihamasishana ikapigwa marufuku na polisi wakiingia nyumba hadi nyumba wakikuta santuri hii inavunjwa.
Akifika Nyerere ndiyo sasa akina Hawa bint Maftah, Bi. Titi, Bi. Tatu bint Mzee na wenzake ndiyo wanamkaribisha kwa nyimbo za lelemama.
Hapo uwanja mzima unazizima kwa shamrashamra na Bantu Group wamelizunguka jukwaa wamevaa lubega xa kamiki wamebeba mashoka na mikuki.
Lakini mipango yote ya mkutano inakuwa imefanyika nyumbani kwa Abdul Sykes jana yake kuwa ni vipi akina mama wataletwa mkutanoni kuja kuhamasisha na kuongeza umma kujaza uwanja.
Haikuwa kitu rahisi kukifanya kwani Dar es Salaam ulikuwa mji wa Waislam na wanawake wasingeweza kujitoa vile hadharani kwa urahisi.
Mama Sakina, Bi. Chiku bint Said Kisusa, mke wa Shariff Abdallah Attas alisaidia sana katika hili na mjukuu wake ndiye aliyemvisha shada la maua Nyerere mwaka wa 1955 aliporejea kutoka UNO. Yapo mengi.
Sheikh Takadir atasoma dua na hapo atamtambulisha Nyerere na Nyerere atawahutubia wana TANU na wananchi kuhusu kudai uhuru wa Tanganyika.
Nyerere alikuwa anaanza hotuba zake kwa kuwaambia Watamganyika kuwa kutawaliwa ni fedheha.
Turudi kwa Frank Humplink.
Waingereza wakamkamata Frank Humplink Moshi alipokuwa anaishi.
Frank Humplink akaachiwa baada ya Chief Thomas Marealle kuingilia kati.
Pale Mnazi Mmoja nyuma ya umma ule Abdul Sykes kasimama pembeni, kalamu mkononi alikuwa akiandika hotuba ya Nyerere katika hati mkato."
Picha ya kwanza Bantu Group katika shamrashamra za kuhamasisha, Frank Humplink, Uwanja wa Mnazi Mmoja mkutano wa TANU, Frank Humplink na Mwandishi nyumbani kwake Lushoto na picha ya mwisho ni Paramount Chief Thomas Marealle.
Bantu Group katika shamrashamra za kuhamasisha
Frank Humplink
Uwanja wa Mnazi Mmoja mkutano wa TANU
Frank Humplink na Mwandishi nyumbani kwake Lushoto