KIAPO CHA SULTANI.
Hapo zamani sana katika nchi za Uajemi , china na hindi kulitokea sultani aliyefahamika kwa kuwa na upendo kwa watu wake na nguvu pia ya kijeshi na kiutawala. Watu wake walimpenda sana na yeye aliwapenda. Sultani huyu alikuwa na watoto wawili ambao ni Shahriyar ambaye ndiye mkubwa na mwingine ni Shahzanam ambaye ndiye mdogo.
Watoto hawa pia walitambulika kwa ushujaa walio nao na uhodari katika mambo mbalimbali, hususani katika fani ya kupanda farasi. Sultani huyu alipofariki utawala wake akamwachia mwanaye mkubwa ashike madaraka yake. Na mwanae mdogo akabakia anatawala maeneo mengine katika utawala wa baba yake. Huyu mdogo akaelekea maeneo ya Samarkand na huyu mkubwa akabaki palepale.
Sultan Shahriyar alikuwa na mke wake aliyempenda sana kwa muda mrefu. Hakuwahi kuamini kama itaweza kutokea siku moja akamsaliti. Ilitokea siku moja akamkuta mke wake anazini na mtumwa wake. Kitendo hiki kilimuuma sana na akamuuwa mkewe na yule mtumwa. Kutokea hapo akaapa kutokumwamini mwanamke yeyote duniani. Na kitendo hiki kilimfanya ajiwekee utaratibu mpya wa maisha nao ni kuoa kila siku mke mpya na kisha humuua ifikapo asubuhi.
Hivyo mambo yakawa kama hivi kila siku jioni bibi harusi mpya mwanamwali huolewa na na ikifika asubuhi huuliwa. Kitendo hiki kiliendelea kwa muda mpaka watu wakawa wanaogopa. Ikiwa nyumba moja watu wanalia kwa kufiwa na binti yao nyumba nyingine hufanyika arusi. Sultani alikuwa na waziri wake maalum ambaye alikuwa amepewa kazi hii ya kumletea mfalme wanawali na kutekeleza amri ya kuwauwa kila ifikapo asubuhi.
Waziri huyu aliyepewa kazi hii alikuwa na watoto wawili aliyewapenda sana, mmoja aliitwa Schehrazade ambaye ndiye mkubwa na Dinarzade ambaye ndiye mdogo. Schehra-zade alipata upendo mkubwa kutoka kwa baba yake. Alipewa taaluma mbalimbali za matibabu, sanaa, kuandika, masimulizi , kazi za mikono na nyingine nyingi. Ukiacha mbali na taaluma hizi pia alijulikana kwa uzuri wake ulioaminika kuwashinda wanawake wote katika nchi hiyo. Mabinti wawili hawa walipendana zaidi kila mmoja.
Ilitokea siku moja katika mazungumzo waziri mkuu akiwa na mabinti zake wanaongea Schehra-zade alitowa ombi kutoka kwa baba yake ambalo lilionekana kumshangaza sana. “Baba ninaombi ila niahidi kwanza kuwa utanitekelezea,” alizungumza Schehra-zade kumwambia baba yake. “ Naahidi nitalitekeleza kama lipo chini ya uwezo wangu,” alisikika waziri mkuu akimjibu binti yake.
“Ninataka kukomesha tabia ya kikatili ya sultani kuua mabinti.” “Mmmhhh mwanangu kipenzi, vipi utaweza kumaliza tabia hii ya sultani wetu?” Ni maneno yaliyokuwa yakizungumzwa kati ya waziri na mwanawe. “Baba ninataka unipeleke mimi kwa sultani niwe mkewe.” Alizungumza Schehra-zade. “Mwanangu unafahamu fika kuwa ukiolewa punde tu ifikapo asubuhi nitaamriwa nikuue,” alizungumza waziri kwa masikitiko makubwa.
Schehra-zade aliendelea kusisitiza ombi lake la kutaka kuolewa na sultani ili akamalize tabia yake ya kuua mabinti. Waziri nae hakuacha kumsihi mwanae asithubutu kujiingiza kwenye matatizo haya makubwa. Waziri akawa anamwambia mwanae, “ Hivi mwanangu unataka nikufanyie kitu gani mpaka uachane na msimamo wako huo? Au unataka yakupate yalompata mke wa mfugaji?” Kwa shauku Schehra-zade akauliza, “Kwani baba ni kitu gani kilimpata mke wa mfugaji.” “Mmmmhh.. Ni habari ndefu lakini nitatakusimulia hadithi yake,” alizungumza waziri na kuanza kusimulia hadithi hii:
KISA CHA MFUGAJI NA MKEWE
Hapo zamani kulikuwa na mfugaji maarufu sana na alikuwa ni tajiri na mfanyabiashara aliyekuwa na mafanikio makubwa. Alikuwa anaelewa lugha za wanyama. Alipata tunu hii kwa sharti kuwa asisimulie kwa yeyote mazungumzo ya wanyama na pindi tu akisimulia alichokisikia atakufa hapohapo. Alikuwa akifurahia sana kuwaona wanyama wake na kujua nini wanazungumza. Alikuwa na banda lake la wanyama ambapo ndani kulikuwa na ng’ombe na punda, ambapo kazi ya kuwasimamia wanyama hawa alimpa mtumwa wake.
Sikumoja alipokuwa amekaa pembeni mwa banda hilo akasikia mazungumzo ya kustaajabisha kati ya punda na ngo’mbe. Ngombe akamwambia punda, “Nakuonea wivu kwa raha unayoipata. Wakati mimi ninashinda juani kulima shamba la bwana wetu wewe mwenzangu unaogeshwa na kupambwa na kazi yako ni kumbeba bwana wetu, wananipiga, wananifunga majembe yao shingoni. Nakuonea wivu, natamani ningekuwa wewe.” Punda akamwambia ng’ombe, “Usijali nitakueleza jambo ukilifanya katu hautalimishwa tena. Kesho akija mfanyakazi mpige mateke na mtishe kwa pembe zako na umfukuze. Kataa kula chakula chao. Ukifanya hivi katu hawatakulimisha tena.”
Siku iliyofuata ng’ombe akafanya kama alivyoshauriwa na punda, akamtisha mfanyakazi na akamkimbiza akataka kumchoma kwa pembe zake. Alikataa kula chakula. Siku iliyofuata mfanyakazi akakuta kile chakula alichokileta jana kipo vilevile hivyo akatoa taarifa kwa bwana wake. Mfugaji akamuamuru mfanyakazi wake amchukue punda kwenda kulima. Hivyo siku ile punda akafungwa jembe la kulimia na kwenda kulimishwa. Jioni ile akarudi bandani akiwa amechoka sana.
Kufika hapa waziri akamwambia mtoto wake Schehra-zade “Binti yangu, hivi unataka kuangamia kama punda alivyomshauri mwenzie vibaya na akaumia mwenyewe?” Schehra-zade akamwambia baba yake, “Baba bado msimamo wangu upo pale pale nipeleke kwa sultani nikakomeshe tabia yake. Lakini baba bado sijajua kilichompata mke wa mfugaji ?” alizungumza Schehra-zade kutaka hadithi iendelee. Waziri akaendelea kumsimulia Schehra-zade hadithi hii:
Siki moja mfugaji akiwa na mkewe wameketi karibu na banda la wanyama hawa ili kujua nini punda atamshauri mwenzie. Akamsikia punda akimwambia ng’ombe, “Rafiki yangu nakupa ushauri unisikilize vizuri. Nimemsikia bwana wetu akimwambia mfanya kazi kuwa kama hali yako utaendelea nayo basi uchinjwe na upelekwe ukauzwe nyama. Hivyo nakushauri kesho utii amri ya mfanya kazi hivyo atadhani kuwa ulikuwa umeumwa na sasa umepona.” Ng’ombe alionekana kutii ushauri huu. Hapo mfugaji akacheka sana. Kicheko hiki kilimstaajabisha hata mkewe. Mkewe akataka kujua kinachomchekesha, akamjibu ni siri na nikikwambia nitakufa ila naweza kusema kuwa ninacheka kwa sababu ya mazungumzo kati ya punda na ng’ombe.
Mke huyu alionekana kuwa na msimamo wa kutaka kujua nini hasa kilisemwa mpaka akacheka. Akaahidi kama asipomwambia atarudi kwao. Ugomvi ukawa mkubwa ikafikia hatua ya kuita ndugu waje kusuluhisha. Mfugaji akabaki na msimamo wake kuwa kama atasema atakufa paohapo na mke akafikia kusema kama asiponiambia na mimi nitajiua. Hali hii iliendelea kwa muda mpaka kufikia kuwa mbaya zaidi. Mfugaji akiwaza nimwambie ili nife kwa kumridhisha mke wangu au nisimwambie. Na nisipomwambia atajiua. Ni mawazo ya mfugaji. Ugomvi uliendelea kwa siku kadhaa bila ya maelewano pale ndani.
Siku moja alikaa nyumbani kwake ghafla akamuona mbwa wake aliyempenda sana anamkimbilia jogoo la kuku. Kisha akamuelezea mambo yote yaliyompata bwana wake yaani mfugaji na mkewe. Hapo jogoo akacheka sana kisha akamwambia, “Bwana wako ni mpumbavu kweli, hivi haunioni mimi nina wake zaidi ya hamsini hapa na ninafanya ninalotaka, lakini yeye ana mke mmoja tuu lakini anampa waka timgumu hivi. Akieleza siri atakufa hapa dawa ni ndogo tu. Achukue fimbo nzuri kisha amtandike kisawasawa, bila shaka atarudisha akili yake.” Baada ya maneno haya jogoo likawika na kuondoka zake kwa mwendo wa madaha.
Mfugaji alifikiri atumie ule ushauri wa jogoo, asubuhi ya siku iliyofuata mke wa mfugaji aliendelea na vurumai lake. Mfugaji akaagiza aletewe bakora nzuri na kutekeleza ushauri wa jogoo. Mambo yakatulia nyumbani na hakuleta vurumai lile tena.
Baada ya kumaliza kusimulia hadithi hii waziri akamwambia Schehra-zade, “Binti yangu, je unataka na mimi nitumie uamuzi wa jogoo?” Schehra-zade akamwambia baba yake, “Hapana baba ila mi nadhani hadithi hii hainitoshelezi kubadili uamuzi wangu.” Basi waziri baada ya mazungumzo marefu akakubaliana na maamuzi ya mwanae na kukubali kumpeleka kuwa bibi harusi kwa sultan kwa usiku uliofuata.
Siku ile waziri akaenda kwa sultani kwa masikitiko na majonzi, akamweleza sultan kile ambacho kilitokea kati ya yeye na binti yake. “Sultani; Schehra-zade anataka kwa heshima yako awe mkeo japo kwa usiku mmoja tu. Nimejaribu kumnasihi na kumkataza kwa hali zote nilizoziweza lakini imeshindikana.” Ni maneno ya waziri alomwambia sultani. “Unajua fika kuwa asubuhi baada ya harusi itabidi uchukuwe amri ya kumuua, na ukishindwa na wewe pia utauliwa na kichwa chako kutundikwa.” Ni maneno ya Sultani akisikika anamwambia waziri. Baaada ya mazungumzo marefu Waziri akarudi nyumbani kwa majonzi na kumueleza binti yake ajiandae kwa harusi jioni inayofuata.
Schehra-zade akamueleza mdogo wake Dinar-zade, “Mdogo wangu nina kitu naomba unifanyie, huenda likawa ombi la mwisho kabla sijauliwa au likanusuru maisha yangu na maisha ya mabinti wengine wa nchi hii.” Ni ombi gani hilo dada?” Dinar-zade alimuuliza dada yake. Schehra-zade akaendelea kumweleza “Nitakapokuwa nimeingia kwa mfalme nitamwomba ruhusa ya kuwa na wewe katika chumba kile ili nipate kukuaga kabla sijauliwa. Hivyo nikipewa ruhusa hiyo itakapofika saa kumi na moja alfajiri niamshe kisha uniombe nikusimulie hadithi nzuri iwe kama furaha ya kuagana.” Mdogo wake akakubaliana na wazo hilo la dada yake.
Hali ilikuwa kama hivyo na harusi ikafanyika kati ya sultani na binti wa waziri mkuu. Bibi harusi akaingia kwenye jumba la kifalme huko akakutana na sura ya sultani. Kwa madaha na manjinjo akamuomba ombi lake la kuruhisiwa kuwa na mdogo wake usiki ule katika chumba kimoja ili aweze kumuaga kesho asubuhi kabla ya kuuliwa. Sultani akakubali ombi lile na kuamuru Dinar-zade aletwe na chumba maalumu kikaandaliwa ndani pale.
Mambo yakawa kama hivyo usiku haukuwa mrefu kati ya mabinti wawili hawa. Ilipobaki saa moja kabla ya kupambazuka Dinar-zade akamwambia dada yake, “Dada yangu kipenzi, naomba unifurahishe kwa kunisimulia hadithi nzuri iwe kama furaha ya mwisho ya kuagana kabla ya kuuliwa.” Schehra-zade kabla ya kumjibu mdogo wake akaomba ruhusa kwa sultani ili amruhusu aweze kutimiza matakwa ya mdogo wake kipenzi. “Hakuna shida msimulie tuu ….” Alisema Sultani. Hapo Schehra-zade akaanza kusimulia hadithi kama ifuatavyo.