Suley2019
JF-Expert Member
- Oct 7, 2019
- 2,203
- 5,610
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mkoa wa Mbeya kimewaasa wananchi kutosusia uchaguzi wa Serikali za Mitaa, vitongoji na vijiji kwa kuwa kura zao ndizo zitakazoamua aina ya viongozi na mustakabali wa maisha yao kwa kipindi cha miaka mitano ijayo (2024-2029).
Mwenyekiti wa CHADEMA mkoa wa Mbeya, Masaga Pius Kaloli, ametoa wito huo alipokuwa akizungumza kwenye mkutano wa hadhara na wananchi wa Chunya mjini, mkoani Mbeya, katika mwendelezo wa mikutano ya hadhara inayoendelea wilayani humo.
Masaga amesisitiza kuwa wananchi wanayo nafasi ya kihistoria ya kuchagua viongozi watakaowatumikia kwa kipindi cha miaka mitano ijayo. Amesema Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imeshindwa kuwaletea wananchi maendeleo ya kweli, akidai kuwa maendeleo yanayosemwa hayaendani na uongozi wenye dhamira safi kwa zaidi ya miaka sitini tangu uhuru.
"Ndugu zangu wa Chunya na Watanzania kwa ujumla, hatupaswi kususia uchaguzi huu wa Serikali za Mitaa. Hatuwezi kukiondoa Chama Cha Mapinduzi madarakani kwa bunduki kwa sababu ni za kwao. Hatutafanya hivyo kwa maneno, bali tutawaondoa kupitia sanduku la kura," amesema Masaga.
Ameongeza kuwa wananchi wa Chunya wanaendelea kuteseka na matatizo lukuki, kama vile upungufu wa maji hata katika maeneo ya mjini, huduma za afya za chini ya kiwango, huku akihimiza kuwa lazima wananchi wachukue hatua kwa kutumia kura zao kuleta mabadiliko.
Mwenyekiti wa CHADEMA jimbo la Vwawa, mkoani Songwe, Mch. Amoni Tuloline Mwashitete, amewaonya wasimamizi wa uchaguzi watakaohujumu uchaguzi huo, akisema hawatovumiliwa, pamoja na mipango ya baadhi ya wagombea kupita bila kupingwa.
Katibu wa CHADEMA jimbo la Lupa wilayani Chunya, Yohana Mpamba (Mcotton), amesisitiza kuwa Chunya ni jimbo lililodumaa kimaendeleo na kuwataka wananchi kuhakikisha wanawachagua viongozi bora katika uchaguzi ujao, ambao utakuwa sauti yao.
Zoezi la uandikishaji wapiga kura katika daftari la makazi kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa, vitongoji na vijiji linatarajiwa kufungwa hivi karibuni, huku uchaguzi ukitarajiwa kufanyika tarehe 27 Novemba 2024 kote nchini.