SoC02 Mbinu hii inaweza kupunguza tatizo la ajira kwa Watanzania

SoC02 Mbinu hii inaweza kupunguza tatizo la ajira kwa Watanzania

Stories of Change - 2022 Competition

Abeida

Member
Joined
Jul 14, 2022
Posts
13
Reaction score
7
Abeid Abubakar

Katuni ya Kipanya katika gazeti la Mwananchi Julai 21 mwaka huu ukurasa wa 10, inafikirisha. Ni tafakuri tunduizi.

Katuni inamuonyesha kipanya mdogo akisema: Msitusahau kwenye utumishi wa umma. Kisha kipanya mkubwa akamjibu kwa swali: Wana eksipiriensi? akimaanisha wana uzoefu wa kazi?

Ni katuni yenye ujumbe unaofikirisha hasa katika kipindi hiki, ambacho idadi kubwa ya wahitimu katika ngazi mbalimbali za elimu na wananchi wengine katika jamii wakilia uhaba wa ajira.

Tatizo ni kubwa kiasi gani? Hebu turejee tukio la mwaka 2014 ambapo Idara ya Uhamiaji ilitangaza ajira ya watu 70, lakini waliofika kwa ajili ya usaili ni watu zaidi 10,000 .

Aidha, kwa mujibu wa takwimu zilizomo kwenye kitabu My Life, My Purpose (Maisha Yangu, Kusudi Langu) kilichoandikwa na hayati Benjamin Mkapa, mwaka 2017 Mamlaka ya Mapato ilitangaza nafasi 400, lakini waliojitokeza kuomba walikuwa 56,000.

Mwaka huohuo watu 6740 walijitokeza kuomba ajira 47 zilizotangazwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS). Takwimu hizi alizotoa Mkapa ni kielelezo cha kutosha kuwa tatizo la ajira lipo na si la leo wala la jana.

Katika mazingira kama haya, tulitatarajia kuwapo kwa mikakati thabiti ya kuongeza nafasi ya ajira hasa zile chache zinazopatikana, lakini cha ajabu mgawo wa ajira umekuwa ukiwarudia walewale ambao tayari kimaisha wako vizuri.

Uteuzi wajumbe wa bodi

Kuna huu utaratibu wa mamlaka za uteuzi kuwateua wastaafu na watumishi walio kazini kuongoza au kuwa wajumbe wa bodi za mashirika na taasisi za kiserikali, nafasi ambazo tungewapa vijana wetu waliohitimu, lakini kama anavyosema Kipanya labda wanakosa uzoefu. Sasa watapataje uzoefu ikiwa hawapewi nafasi?

Ninapoangalia utitiri wa vyombo na taasisi hizi na idadi ya wajumbe katika vyombo hivyo, naona kabisa namna ambavyo nafasi hizo zinavyoweza kujazwa na vijana na kisha tukapunguza kwa namna fulani tatizo la ajira.

Kibaya zaidi ni pale unapoona hao wanaoteuliwa kuwa wajumbe ni watu ambao hata weledi katika fani husika au chombo husika, unaleta ukakasi.

Utaona tunatangziwa kuwa fulani na fulani wameteuliwa kuwa wajumbe wa bodi kama vile ya utalii, lakini wanaotajwa ni wanajeshi, maprofesa wa elimu ya siasa na wengine ambao ukiangalia CV zao hazihusiani na utalii.

Haya yanafanyika wakati vyuo vinazalisha wahitimu wa stashahada na shahada mbalimbali za utali, tena wapo wanaosomea kwa ngazi za uboboezi wa taaluma yaani shahada za uzamili na uzamifu.

Hawa hawapewi nafasi badala yale wanapewa nafasi wastaafu na watu ambao tayari wamo kwenye utumishi na zaidi mambo yao yakiwa yameshanyooka!

Hebu tuone mfano wa hivi karibuni kuhusu uteuzi wa bodi ya wakurugenzi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, kama ninavyoinukuu kutoka katika tovuti ya www.maliasili.go.tz kwa taarifa yenye kichwa cha habari: Uteuzi wa wajumbe wa Bodi ya Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA)

Bodi hiyo inaongozwa na Mwenyekiti Jenerali mstaafu wa Jeshi la Wananchi na aliyekuwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Venance Mabeyo, huku wajumbe wake wakiwa hawa wafuatao na taaluma zao kwenye mabano;

Moja, Benson Obdiel Kibonde (mhifadhi wanyamapori mkuu (Mstaafu) Pori la Akiba Selous.

Mbili, Bakari Nampenya Kalembo (mshauri wa masuala ya fedha)

Tatu, Agnes Kisaka Meena (Mkurugenzi wa Uendelezaji Sera, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora)

Nne, Prof. Esther William Dungumaro (Mkuu wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu, Mkwawa (MUCE).

Tano, Prof. Herrieth Godwin Mtae (Mtaalamu wa Maendeleo ya Uchumi wa Jamii, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT).

Sita, Prof. Henry Chalu, (Profesa Mshiriki, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam)

Saba, Simon Vedastus Ntobbi, Ofisa tawala mkuu Daraja la I, Ofisi ya Rais - Utumishi)

Tazama mwenyewe aina ya watu walioteuliwa katika nafasi hizo na kitu wanachokwenda kukisimamia. Kama wajumbe wa bodi ni washauri wa chombo husika, pengine tulitarajia orodha hii kujaa watu wenye taaluma za uhifadhi, utalii, maendeleo ya jamii na vijiji na fani zinazofanana na majukumu ya chombo husika.

Watu wenye fani za uhifadhi na utalii wapo na pengine wamejaa mtaani wanalia ajira. Lakini mifumo yetu haiwafikirii, labda kwa kigezo cha kukosa uzoefu.

Tuwe wakweli, shirika kwa mfano linalohusika na maji; kati ya kumteua kwenye ujumbe wa bodi mhitimu mhandisi wa maji asiye na kazi na mstaafu wa jeshi ambaye fani yake ni upigaji mizinga, au profesa wa saikolojia ya elimu, kipi bora kwa manufaa na mustakbali wa chombo hicho? Hii ndio hoja ninayoijenga. Kidogo kilichopo tugawane sote, kuliko kidogo hicho kuliwa na walewale siku zote

Mimi naamini kuwa kama mashirika yote ya Serikali na vyombo vingine, yatawapa nafasi vijana wasomi wasio na kazi katika bodi zao, tutasaidia kupunguza tatizo.

Natambua kuwa baadhi ya bodi, hazina mishahara lakini si mbaya, vijana hawa wakiwa huko hata hizo posho zinawatosha kuliko kukosa kabisa, Inauma kuona posho hizo ‘ zilizonona’ wakipewa watu ambao chambilecho msemo wa vijana kuwa ‘wameshatoka kimaisha’.

Ushauri wa makala haya ni kuwa katika mazingira ambayo ajira ni tatizo, kunapotokea fursa tungefikiria kuanza na wale wasio na ajira ikizingatiwa hizi nafasi za bodi aghalabu ni za ushauri, hivyo ushauri ukitoka kwa mtu wa fani husika, huwa bora zaidi kuliko hata busara za mstaafu japo sidunishi kuwa wastaafu hawana kitu cha kuchangia.

Kama hatuna ajira za kudumu kwa sababu mbalimbali , basi tusishindwe japo kuwasaidia baadhi ya vijana kwa kuwapa nafasi hizi zenye ukomo wa muda wa kazi.

Kwa mfano, mchakato wa kuwapata wasimamizi wa sensa, nadhani haukupaswa kuwashirikisha watu wenye ajira za kudumu kama walimu. Hii ingekuwa fursa tosha kwa hawa maelfu ya wahitimu wasio na ajira.

Kioja zaidi, wakati tunalia na ajira unaweza kushangaa kuwa kuna mashirika kibao ambayo huwa kuna wakati yanakosa wajumbe wa bodi. Mfano mzuri ni ripoti ya Mkaguzi na Mdhbiti Mkuu wa Hesabu za Serikali aliyoitoa mwaka 2020 na habari yake kuwekwa katika tovuti ya www.mwananchi.co.tz ya Aprili 8 mwaka huo. Taarifa ilitaja mashirika 43 ya Serikali kutokuwa na wajumbe hivyo kuzorotesha utendaji.

Hizi zote ni fursa ambazo zingeweza kuwasaidia wahitimu wetu na wananchi wengine wasio na ajira.

Mwandishi ni mkazi wa Dar es Salaam. Anapatikana kwa barua pepe: abeidothman@gmail.com
 
Upvote 0
Back
Top Bottom