WAKATI watu wengi wakijitosa kuzungumzia kashfa ya ubadhirifu wa mabilioni ya shilingi katika Benki Kuu (BoT), Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, ameonekana kusita kuungana nao.
Mwinyi aliweka bayana msimamo wake huo, nyumbani kwake Mikocheni jijini Dar es Salaam juzi, muda mfupi tu baada ya kukamilika kwa hafla ya ufunguaji wa akaunti katika Benki ya NMB, kwa ajili ya michuano ya soka ya Kombe la Ali Hassan Mwinyi Orphans.
Rais huyo mstaafu ambaye alikuwa akijibu swali aliloulizwa na mwandishi wa gazeti hili, alisema ni mapema mno kwa sasa kueleza msimamo wake kuhusu jambo hilo na akaahidi kufanya hivyo wakati muafaka utakapowadia. "Suala la BoT… aahaaa…, siwezi kuzungumzia, ni mapema mno ………(kicheko), wakati ukifika nitalizungumzia," alisema rais huyo mstaafu huku akiingia nyumbani kwake.
Mwinyi anaweka bayana uamuzi wake huo ikiwa ni takriban wiki mbili sasa tangu Rais Jakaya Kikwete alipochukua uamuzi wa kutengua uteuzi wa aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu, Daudi Ballali, siku chache tu baada ya kupokea taarifa ya ukaguzi wa hesabu za taasisi hiyo nyeti, kazi iliyofanywa na Kampuni ya kimataifa ya Ernst & Young.
Ballali aliyeko nchini Marekani anakoaminika kuwa alikwenda kutibiwa tangu katikati ya mwaka jana, ndiye ofisa pekee wa juu wa serikali ambaye tayari amehusishwa kwa namna moja au nyingine na ufujaji wa shilingi bilioni 133, fedha za umma kupitia Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA).
Mbali ya Ballali, viongozi wengine kadhaa wakiwamo Basil Mramba, aliyekuwa Waziri wa Fedha wakati fedha hizo zikichotwa mwaka 2005 na Gray Mgonja aliyekuwa Katibu Mkuu Hazina wakati huo, ni miongoni mwa viongozi ambao majina yao yanatajwatajwa kuwa miongoni mwa watu wanaostahili kuwajibika au kuwajibishwa kutokana na ubadhirifu huo.
Tangu Kikwete atoe uamuzi huo, kumekuwa na maoni tofauti kutoka kwa watu kadhaa binafsi na taasisi za kijamii na kidini zilizoeleza kushtushwa na kugundulika kwa ubadhirifu huo mkubwa wa kwanza kuwekwa hadharani hapa nchini. Katika hatua ya hivi karibuni, Mwenyekiti wa Chama cha siasa cha PPT-Maendeleo, Peter Mziray, ameitaka kamati iliyoteuliwa na Rais Kikwete, kuacha kufanya uchunguzi zaidi, na badala yake iwakamate viongozi wa taasisi za serikali, makampuni binafsi na wafanyabiashara ambao wametajwa katika ripoti ya Kampuni ya ukaguzi wa hesabu ya Ernst & Young kuhusika katika uchotaji wa fedha katika akaunti ya madeni ya nje (EPA).
Mziray aliyasema hayo jana alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO), jijini Dar es Salaam. Alisema kuwa kitendo cha wanasheria kuomba wapewe taarifa kutoka kwa wananchi ni kupoteza muda, kwani masuala mengi ya msingi ambayo yanaweza kutumika kama ushahidi mahakamani, yalishabainishwa na kampuni hiyo.
Alisema kilichotakiwa kwa timu hiyo ni kutafuta vielelezo zaidi kutokana na maelezo yaliyotolewa na Ernst & Young kama vile kutafuta kumbukumbu za makampuni hayo katika ofisi za wakala wa usajili wa makampuni - BRELA.
Kwa upande mwingine, Mziray alisisitiza kuwa, anauona uhusiano wa kisayansi kati ya uchotaji wa fedha kutoka BoT na ushindi wa kishindo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005. "Mwaka 2004 magazeti humu nchini yaliandika kwamba NEC ya CCM ilimwomba mwenyekiti wake wa wakati huo kuziongezea uwezo wa kifedha, magari na vitendea kazi ofisi za chama hicho nchini pote.
Na baada ya muda mfupi, CCM ilimwaga magari ya kuzinufaisha ofisi za wilaya zote pamoja na kugawa kanga, fulana na kofia nchi nzima. Tunahoji walipata wapi pesa kwa muda huo mfupi? "Mimi sioni lolote la kumpongeza Rais Kikwete eti kwa kutengua ajira ya aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu kwani ni sehemu ya utendaji wake," alisema.
Alisema yeye ataridhika iwapo waliotajwa kuhusika na upoteaji wa fedha hizo wakichukuliwa hatua stahili kama vile kukamatwa na kuhojiwa, kwani ukiacha Dk. Ballali ambaye yupo nje ya nchi, wengi wa waliotajwa wamo humuhumu nchini.
Alisema kuwa bila ya jambo hili kuchukuliwa hatua kwa umakini, uamuzi wa kuzirejesha fedha hizo unaweza usitekelezeke. Aidha, Mziray alimtaka aliyekuwa waziri wa fedha wakati wizi huo ulipotokea, Basil Mramba, na Waziri wa Fedha wa sasa, Zakia Meghji, kujiuzulu, si kwa kuwa wanahusika na wizi huo, bali ili kulinda heshima zao.
Habari Mpya | Kitaifa | Dar | Mikoani | Tahariri | Makala | Michezo | Matangazo | Webmaster
Copyright 2008 © FreeMedia Ltd. Free media limited
mtaa wa Mkwepu na Makunganya, jengo la Bilicanas, gorofa ya kwanza, SLP 15261, Dar es salaam, Tanzania
simu +255-22-2126233 • faksi +255-22-2126234 • Selula 0713 296570