nngu007
JF-Expert Member
- Aug 2, 2010
- 15,860
- 5,801
- Sunday, May 15, 2011, 9:12
- Habari za Mikoani, Mtanzania
Na Mwandishi Wetu, Mwanza
MBUNGE wa Ilemela Jijini Mwanza, Highness Kiwia (CHADEMA),amewaonya wafanyabiashara na wamiliki wa viwanda vya samaki jijini hapa, kwa vitendo vyao vya kubana mizani na kuwapunja wavuvi wadogo mali zao halali.
Alisema, kitendo cha wafanyabiashara hao kuwaibia wavuvi wadogo mali zao, inapaswa kukomeshwa haraka sana, kwani ni kinyume cha sheria za nchi.
Kutokana na hali hiyo, mbunge huyo ametoa muda wa siku saba kuhakikisha hali hiyo,inakomeshwa la sivyo hatua za kisheria zitaanza kuchukuliwa dhidi ya wahusika.
Kiwia, aliyasema hayo juzi wakati alipofanya ziara ya kushtukiza
kwenye mialo ya uvuvi iliyopo Igombe na Kayenze jimboni Ilemela.
Tumeona sote wizi huu, kwenye kilo 100 mvuvi mdogo anapunjwa kuanzia kilo 20. Hii ni hatari sana kwa maendeleo na mimi nitalifuatilia hili hadi kieleweke, alisema Kiwia.
Kwa mujibu wa Kiwia, Sheria ya vipimo namba 20 ya mwaka 1982, iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002, inakataza wafanyabiashara kutumia mizani isiyo sahihi wala vipimo visivyoruhusiwa kisheria, hivyo adhabu yake ni faini, kifungo cha mwaka mmoja hadi miaka mitano.
Kwa upande wao, wafanyabiashara wa samaki katika mialo hiyo ya Igombena Kayenze, walimweleza mbunge huyo, kwamba wanabana mizani yao kwa sababu nao wanapopeleka samaki viwandani hukuta mizani imebanwa, hivyo hupoteza kilo nyingi.