Mbunge wa Jimbo la Bukoba Mjini mkoani Kagera, Stephen Byabato, amesema ujenzi wa soko kuu la kisasa la Manispaa ya Bukoba ni miongoni mwa miradi minne iliyopo katika miradi mikubwa ya TACTIC, ambayo itagharimu zaidi ya shilingi bilioni 47, ambapo wafanyabiashara 1,200 watahama kupisha ujenzi wa soko hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutembelea na kukagua miradi hiyo ambayo inatekelezwa katika Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera kupitia mradi wa TACTIC, Mbunge Byabato amesema kuwa anaipongeza serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa bilioni 47 ili kutekeleza miradi hiyo ambayo inaenda kuibadilisha Manispaa ya Bukoba na mkoa kwa jumla.
Aidha, ameongeza kuwa ili ujenzi wa soko kuu la Bukoba ukamilike kwa wakati, wafanyabiashara wapato 1,200 waliopo katika soko hilo wanatakiwa kuhamia sehemu nyingine ambazo zimeandaliwa na Manispaa ya Bukoba ili ujenzi wa soko hilo uanze mara moja.
Miradi mingine ambayo itatekelezwa katika Manispaa ya Bukoba kupitia TACTIC ni pamoja na ujenzi wa stendi, kingo za Mto Kanoni pamoja na ujenzi wa barabara zaidi ya kilometa 10 katikati ya mji.