Stephano Mgendanyi
JF-Expert Member
- May 16, 2020
- 2,833
- 1,301
MBUNGE JANETH MAHAWANGA AITAKA SERIKALI KUWEKEZA KWENYE MAJUKWAA YA UWEZESHAJI WANAWAKE KIUCHUMI
Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Tisha Mama Foundation Mhe. Janeth Elias Mahawanga amechangia Bajeti ya Shilingi Bilioni 74.22 ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum iliyosomwa na Waziri Mhe. Dorothy Gwajima
Mhe. Janeth Mahawanga ameipongeza Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa kazi nzuri inayofanya lakini amempongeza pia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ndiye muasisi wa Majukwaa ya uwezeshaji Wanawake Kiuchumi kwa kuona changamoto wanazopitia Wanawake Wajasiriamali katika harakati zao za kujikwamua kiuchumi.
Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan alikuwa na maono haya akiwa Makamu wa Rais mwaka 2016 na mwaka 2022 Majukwaa haya yalirasimishwa rasmi.
Mhe. Mahawanga ameitaka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kufanya kazi kwa kushirikiana na Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara na kuhakikisha Majukwaa haya yanakuwa imara na yenye tija kwa Vikundi vya akina Mama ambao wamehamasika sana kujiunga vikundi kupitia majukwaa haya kwa kuhakikisha wanaratibu utoaji wa mafunzo kwa watekelezaji wa majukwaa, wanaratibu upatikanaji wa mitaji, wanawaunganisha na fursa mbalimbali za kiuchumi, wanashauri mbinu bora za kuendeleza shuguli zao za kiuchumi na kuwaunganisha na wadau muhimu hasa kwenye masuala ya upatikanaji wa mitaji.
Aidha, Mhe. Mahawanga ameitaka Wizara kuhakikisha inazingatia mambo muhimu matatu katika kuwakomboa Wajasiriamali hao ambayo ni Elimu, Fursa na Mitaji kwani hivi ni vitu muhimu sana unapoamua kumsaidia mjasiriamali.
Mhe. Mahawanga ameomba elimu hiyo ihusishe Vikundi vyote vya majukwaa ngazi zote isiwe ngazi ya Mkoa tu bali ifike mpaka ngazi ya Kata, Mitaa na Vijiji kwani huko ndiko kwenye watu na vikundi vingi lakini pia Madiwani wa Viti Maalum washirikishwe kwani wao ni wadau wakubwa katika kusimamia vikundi hivi huko kwenye majimbo katika kuwasimamia kwenye kupata mikopo na kuwapa semina mbalimbali za ujasiriamali.
Mhe. Mahawanga ameiomba Wizara kuhakikisha Waratibu wa Majukwaa wavisaidie vikundi kwa kuwakutanisha kwenye vikao vyao vyao na wadau muhimu kama Sido, TBS, Kampuni za Bima, Taasisi za Kifedha, Brella, Maafisa Biashara wa Halmashauri na Wataalam wa Masoko ili kuwapa uelewa mpana Wajasiriamali hao.
Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum katika bajeti yake ya mwaka 2023/2024 imeomba jumla ya Shilingi 74,223,193,000 ili kutekeleza majukumu yake ya Maendeleo na Ustawi wa Jamii.