SoC03 Mbunge kuwa waziri kunalegeza utendaji

SoC03 Mbunge kuwa waziri kunalegeza utendaji

Stories of Change - 2023 Competition

Thom issa

New Member
Joined
Jul 15, 2023
Posts
2
Reaction score
2
Habari wana jamiiForums, naitwa Thom nimekuja mbele ya jukwaa hili kuelezea ufanisi na mapungufu yanayojitokeza ikiwa Mbunge wa jimbo flani nchini kwetu Tanzania wakati huo pia akateuliwa kuwa waziri wa wizara flani.

Tunajua kuwa wabunge wana chaguliwa na Wananchi kwenye majimbo mbalimbali Nchini ili wakawakilishe maoni na mawazo ya wananchi wa jimbo husika kwa sababu watu wote hawawezi kwenda Bungeni bali kwa kupitia wawakilishi hao kwa mjibu wa katiba.

Hivyo kwa njia hiyo ndipo wabunge wanavyopatikana Nchini Tanzania kwa ajili ya kuwakilisha mahitaji ya wananchi ikiwa ni pamoja na huduma za kijamii kama maji,umeme ,Hospitali,Barabara pamoja na miundo mbinu mingine.

Hoja zangu za Mbunge kuchaguliwa kuwa waziri inaweza kuwa ni njia rahisi kwa serikali kuweza kuchagua mtu ambaye tayari wanajua utendaji wa kazi zake pamoja na misimamo yake katika kutekeleza majukumu yake ya kila siku, Lakini haya ni miongoni mwa madhaifu yanayo onekana moja kwa moja kwa mbunge kuteuliwa kuwa Waziri.

Utendaji hafifu Jimboni kwake,Nimeshaona mara kadhaa Mbunge akiteuliwa kuwa Waziri utendaji wa kazi zake kama Mbunge anayewakilisha wananchi wa jimbo flani huwa yanafifia,kwa sababu muda mwingi ataanza kufanya ziara kwenye mikoa mbalimbali kukagua na kuangalia maendeleo ya miradi iliyopo chini ya wizara yake,hivyo nguvu inapungua ya kusimamia jimbo lake.

Mbunge kuwa Waziri inapunguza uwajibikaji hasa kwenye kushauri serikali ifanye kitu gani ili isonge mbele,mfano Mbunge Juma Aweso ni Mbunge pia ni mteule wa Rais kwenye wizara ya maji,kwa upande huo yeye atashindwa kuikosoa serikali endapo kama kuna miradi itakuwa inasuasua hasa kwenye uidhinishaji wa fedha za miradi hiyo.

Mbunge kuwa Waziri inapelekea yeye Mbunge kufanya kazi bila uoga wa kukosolewa hivyo kusababisha miradi ya wizara kutokuendelea mbele kwa msukumo wa wabunge wenzake hayo yote yanasababishwa na urafiki pamoja na ujamaa uliopo kati yao Mbunge flani hataki kumkosoa Mbunge flani ambaye ni Waziri kwa sababu ni rafiki yake.

Mbunge kuwa Waziri, inasababisha kuwepo kwa uchawa ambao kwa sasa hivi umekithiri ndani ya Tanzania, hii ni kwa sababu mpaka sasa karibia kila Waziri akiwa kwenye ziara au mradi flani wa maendeleo lazima amshukuru Rais hata kama mradi huo umefadhiliwa na watu au Taasisi ya nje ya Nchi, hali ya kumtaja Rais kila sehemu wanaona ndiyo njia nzuri ya kubaki kwenye uteuzi wakati huo Utendaji unakuwa mbovu.

Mbunge kuwa Waziri inapelekea miradi mingi kuendelea kuendeshwa kisiasa badala iendeshwe kwa mikakati maalum na inayoleta tija,hii ni kwa sababu Mbunge anakuwa mzuri akiwa sio Waziri anaweza kushauri serikali,kukosoa na kuweka mijadala yenye suluhisho,mfano Hussein Bashe alipokuwa Mbunge aliwakilisha vizuri mawazo yake bungeni lakini kwa sasa amepunguza mijadala yenye tija ametulia kwa sababu hawezi kukosoa serikali maana yeye pia ni sehemu ya serikali.

Kitu cha kufanya kwenye katiba na kanuni zingine ambazo zimetoa baraka kwa wabunge kuteuliwa kuwa mawaziri zifikie hatua sasa zibadilishwe ili serikali ipate mawaziri ambao sio wabunge ili kufanya kazi kwa ufanisi na kuepuka siasa katika utendaji na kuharakisha maendeleo kwa wananchi wa Tanzania kwa sababu bado kuna matatizo mengi sana kwenye Nchi yetu kama uhaba wa ajira,uhaba wa maji,Hospitali,ubovu wa barabara na mengine mengi,hivyo kupitia andiko hili likawaguse wasomaji wote na lifike sehemu husika tupate muafaka.

(Haya ni mawazo yangu sijakopa sehemu yoyote)
 
Upvote 1
Back
Top Bottom