Mbunge Lidia Thorpe wa Australia ametolewa nje ya Bunge la Nchi hiyo baada ya kupiga kelele na kumfokea Mfalme wa Uingereza, Charles III alipolitembelea Bunge hilo jana Jumatatu.
Thorpe alisindikizwa nje na Walinzi baada ya kupiga kelele akisema hamtambui Mfalme huyo kama Mfalme wake na kwamba Serikali ya kifalme (Wakoloni) ya Uingereza imechukua ardhi na mifupa ya Wenyeji wa Nchi hiyo.
“Ulifanya mauaji ya kimbari dhidi ya Watu wetu, utupe ulichotuibia, mifupa yetu, mafuvu yetu, Watoto wetu, Watu wetu, uliharibu ardhi yetu” alisikika Mbunge huyo akipiga kelele na kudai kuwa hakuna mkataba uliowahi kufikiwa kati ya Wakoloni wa Uingereza na Wenyeji wa Australia.
Tukio hili limetokea wakati vuguvugu la Jamhuri la Australia likiwa limeshika kasi likitaka Australia kufuta uhusiano wake wa kikatiba na Uingereza ambapo waliandika barua wakitaka kujitenga na Uongozi wa kifalme wa Uingereza.
Raia wa Australia waliamua katika kura ya maoni ya mwaka 1999 kumbakisha Malkia Elizabeth II kama Mkuu wa Nchi hiyo jambo ambalo limekua likipingwa katika siku za hivi karibuni na baadhi ya Viongozi ambao wanataka Australia isiwe tena chini ya uongozi wa Kifalme wa Uingereza. #MillardAyoUPDATES