The Sheriff
JF-Expert Member
- Oct 10, 2019
- 747
- 2,112
Mabadiliko ya tabianchi yamekuwa changamoto kubwa duniani, na Tanzania imeathirika pakubwa kutokana na kuongezeka kwa matukio ya hali mbaya ya hewa kama mafuriko, ukame, na kupungua kwa rasilimali muhimu kama vile maji. Hali hii imeathiri sekta nyingi muhimu kama kilimo, nishati, na afya, na kuleta athari za kiuchumi na kijamii.
Kama wawakilishi wa wananchi, wabunge wanatakiwa kuwa mstari wa mbele katika kutengeneza sera zinazolenga kupambana na mabadiliko ya tabianchi na kulinda ustawi wa taifa kwa ujumla. Lakini je, ni wabunge wangapi wameweka suala hili kama kipaumbele katika ajenda zao za maendeleo? Ikiwa wapo, ni hatua gani wamechukua katika majimbo yao kukabiliana na athari za moja kwa moja za mabadiliko haya?
Kwa mfano, matukio ya ukame katika mikoa ya Kaskazini, kama vile wilayani Longido, yameleta maafa makubwa ambapo mifugo zaidi ya 556 ilikufa mwaka 2022 na kupelekea wananchi kukabiliwa na upungufu wa chakula na kutetereka kiuchumi. Hii inaonesha hitaji kubwa la wabunge kushughulikia kwa haraka suala la uhifadhi wa mazingira, ujenzi wa miundombinu ya uvunaji maji, na uwekezaji katika teknolojia za kilimo cha umwagiliaji ili kupunguza utegemezi wa mvua.
Katika maeneo yaliyoathirika sana na mafuriko hivi karibuni kama vile Katesh, wilayani Hanang, ambapo takribani watu 80 walifariki na wengine 133 kujeruhiwa mwaka 2023 kutokana na mafuriko, wananchi wanapaswa kujiuliza je, mbunge wetu amechukua hatua gani kuhakikisha majanga kama haya hayagharimu maisha ya watu kwakuwa tu pamekosekana miundombinu ya kukabilana na matokeo ya mabadiliko ya tabianchi? Je, ametengeneza mikakati gani shirikishi ya utunzaji wa mazingira utakaoepusha majanga mengine? Haya ni maswali ya msingi kwa wananchi wanaotaka kiongozi anayejali masuala ya mazingira na maendeleo endelevu.
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) lilieza wakati fulani kuwa mgao wa umeme ulioikuwa ukiikumba nchi wakati ule ulisababishwa na ukame. Hii ni ishara tosha ya jinsi ambavyo mabadiliko ya tabianchi yanavyoweza kuharibu uchumi wa nchi. Na hii ndiyo sababu wabunge wanapaswa kuwa na jukumu la kuhakikisha kuwa miundombinu ya nishati mbadala kama nishati ya jua na upepo inawekezwa kwa nguvu zaidi. Lakini pia wanapaswa kuhimiza serikali kuweka bajeti inayojitosheleza kwa ajili ya kukabiliana na majanga yanayotokana na hali mbaya ya hewa. Lakini je, wako wapi wabunge wenye mikakati ya muda mrefu kuhusu nishati safi na mbadala?
Wakati nchi ikielekea kwenye uchaguzi mkuu wa 2025, wananchi wanapaswa kujiuliza kwa kina kuhusu mchango wa wabunge wao katika kukabiliana na changamoto hizi. Ni muhimu kuhoji wabunge wao wamekuwa wakifanya nini kuhakikisha kwamba unajengwa uwezo wa kitaifa wa kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Lakini inapotokea kwamba mbunge hana dhamira au hajachukua hatua zozote za kushughulikia changamoto hizi, ni nini wananchi wanaweza kufanya? Kwanza, mimi binafsi nadhani ni muhimu kuzingatia ukweli kwamba mabadiliko ya tabianchi si jambo la kisiasa pekee bali ni suala la maisha na vifo. Hivyo, wananchi wanaoathirika na athari za moja kwa moja za mabadiliko ya tabianchi wanapaswa kuwawajibisha viongozi wao kwa kutaka uwazi kuhusu mipango ya muda mrefu ya kukabiliana na changamoto hizi.
Katika mazingira ya kidemokrasia, uchaguzi ndiyo silaha kuu ya wananchi. Ikiwa mbunge haoneshi nia ya kushughulikia masuala yanayogusa maisha yao, basi ni wajibu wa wananchi kumtafuta mbunge mwingine anayeweka mbele maslahi yao na kuhakikisha kwamba mazingira yao yanaimarika.
Kingine ni kwamba, wananchi wanaweza kutumia majukwaa ya kiraia, kama vile mashirika yasiyo ya kiserikali yanayoshughulika na masuala ya mazingira, kuhamasisha na kushinikiza serikali kuchukua hatua madhubuti zaidi. Vilevile, kwa kutumia mitandao ya kijamii na majukwaa kama JamiiForums, wananchi wanaweza kufikisha sauti zao kwa viongozi wao na kuweka shinikizo la kisiasa kwa wabunge kuchukua hatua za haraka.
Wapiga kura wanapaswa kuwa tayari kuwawajibisha viongozi wao kwa kushindwa kuchukua hatua kuhusu masuala ya mazingira kwa ujumla wake. Kwa mfano, katika uchaguzi wa 2025, wapiga kura wanapaswa kuwauliza wagombea maswali haya magumu: Je, una mipango gani ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi katika jimbo hili? Je, umewahi kushiriki katika kuanzisha sera za mazingira bungeni? Je, una mkakati gani wa muda mrefu wa kuhakikisha tunapunguza utegemezi wa kilimo cha mvua na kuhamasisha nishati mbadala?
Ni wazi kuwa mabadiliko ya tabianchi ni tishio kubwa, lakini pia yanatoa fursa ya kipekee kwa viongozi wanaoelewa uzito wake. Tanzania inahitaji wabunge wenye uwezo wa kufikiria mbali, ambao wako tayari kuchukua hatua za kisera za muda mrefu kuhakikisha kuwa vizazi vijavyo vinakuwa na mazingira salama na endelevu. Wananchi wanapaswa kutumia nafasi hii katika uchaguzi ujao 2025 kuchagua viongozi ambao wanatambua umuhimu wa kupambana na mabadiliko ya tabianchi na kuchukua hatua stahiki za kuhakikisha taifa linakuwa salama.
Kwa hivyo, mbunge wako anafanya nini kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi? Na kama hajafanya lolote, unachukua hatua gani kuhakikisha unapata mbunge anayejali mustakabali wa taifa?