Nimekutana na stori inadaiwa kuna Mbwa wa Urusi anayeitwa Laika ndiye kiumbe hai wa kwanza kusafiri nje ya dunia? Kuna ukweli kuhusu historia hii?
- Tunachokijua
- Laika alikuwa ni mbwa mdogo aliyepatikana huko Moscow, alichaguliwa kwa ajili ya majaribio ya kutuma chombo nje ya dunia, alikuwa ni mbwa wa mtaani asiye na makazi hivyo iliaminika kuwa angeyamudu mazingira ya njaa, baridi na mikiki mikiki ya huko anga la mbali.
credits: RCS Energia
JamiiCheck imefuatilia makala na tovuti za masuala ya anga na kubaini kuwa ni kweli mnyama wa kwanza kwenda anga za mbali kuzunguka dunia alikuwa mbwa aliyejulikana kwa jina la Laika. Mathalani makala iliyoandaliwa na Royal Museums Greenwich wanaeleza kuwa mnyama wa kwanza kufika anga za mbali kuizunguka dunia alikuwa ni mbwa aliyejulikana kwa jina Laika kwa kutumia chombo cha anga za juu cha Soviet Sputnik 2 tarehe 3/11/1957
Wakati wa majaribio Mbwa Laika alichaguliwa na mbwa wengine wawili waliojulikana kama (Albina na Mushka) ambao waliwekwa kweye vizimba vidogo zaidi kwa wiki kadhaa na mwisho kutokana na hali yake ya utulivu Laika akapata nafasi ya kuchaguliwa. Kiongozi wa mpango wa kisovieti wa anga za juu Vladimir Yazdovsky alieleza kuwa Laika alikuwa mtulivu na mwenye kupendeza.
Tovuti ya Space.com imeandika kuwa mbwa Laika alipokuwa kwenye chombo aliwekwa kwenye kichumba ambacho kilimuwezesha kukaa ama kulala, kichumba hicho kilikuwa na mfumo wa kuzalisha hewa mpya. Lakini pia aliunganishwa na mfumo uliomuwezesha kula, kunywa maji na kumsafisha.
Licha ya mbwa Laika kufika kwenye anga la mbali na kuizunguka dunia lakini hakufanikiwa kurudi duniani, alifia hukohuko kwa sababu kifaa kilichompeleka hakikutengenezwa kwa ajili ya kurudi salama kulingana na teknolojia ya wakati huo.
Kwa mujibu wa Russian space web inadaiwa kuwa mbwa Laika alifanikiwa kuishi kwa siku nne tu wakati chombo hiko kikiwa hiko, lakini vyanzo vingine vinadai kuwa mbwa Laika aliishi kati ya masaa matano hadi sita ya safari kutokana na joto kali lililokuwepo kwenye chombo hiko.
credits: RCS Energia
NASA wameeleza kuwa tarehe 10/11/1957 satelaiti iliishiwa betri na hivyo kupelekea upokeaji wa data kutoka kwenye jaribio hilo ukakoma. Miaka kadhaa baadaye wanyama wengine walipelekwa angani lakini awamu hii walirudi salama na hiyo ikawa ni hatua muhimu ya kuandaa safari itakayomuhusisha binadamu kwenda anga la mbali.
Mnamo mwaka wa 2008, sanamu la kumbukumbu la Laika liliwekwa nje ya Star City, kwenye kituo cha kijeshi nchini Urusi alipopewa mafunzo kabla ya safari yake. Sanamu hiyo inafanana na chombo kilichounganishwa kwenye mkono kilichompeleka Laika kwenye anga la mbali.
Credit: Universe today