[h=1]MAMA RWAKATARE AUGUA GHAFLA[/h]
Na Mwandishi Wetu
MCHUNGAJI wa Kanisa la Mikocheni B Assemblies Of God,Dk. Getrude Rwakatare ameugua ghafla na kulazwa hospitalini jijini Dar es Salaam kutokana na kusumbuliwa na tatizo la shinikizo la damu.
Taarifa zilizopatikana kutoka kwa baadhi ya waumini wa kanisa lake ambao hawakupenda majina yao yatajwe gazetini, zinasema kulazwa kwa mchungaji huyo kunatokana na kupata shinikizo la damu kufuatia kupokea taarifa kuwa, baadhi ya vigogo wa vyama vya siasa na dini wameandaa mikakati ya kummaliza kidini na kisiasa.
Hata hivyo, waumini hao walikataa kata kata kutaja hospitali aliyolazwa mama huyo kwa madai ya usalama na kuhofia usumbufu kutoka kwa waandishi wa habari, waumini wake na watu wengine.
Hana hali mbaya sana japokuwa baadhi ya waumini walimiminika kumuona. Alipofika hospitalini kitu cha kwanza alichofanyiwa ni kutundikiwa dripu (chupa ya maji). Unajua huyu mama ana umri mkubwa hivyo, kama mtu ana jambo anapaswa amueleze hatua kwa hatua, vinginevyo, anaweza kumuua kwa presha, alisema mmoja wa waumini wa mchungaji huyo.
Hata tunapopata taarifa za msiba huwa tunamueleza kwa kumuanzia mbali, taratibu, tumekuwa tukifanya hivyo kuepuka mshituko unaoweza kumtokea, alisema muumini huyo.
Aidha, alifafanua kuwa kinachomsumbua mchungaji huyo ni makundi ndani ya vyama vya siasa kwani kuna baadhi ya wanachama aliochuana nao katika uchaguzi mkuu uliopita na kuwabwaga, bado inaonekana hawajavunja makundi yao na wanaendelea kuweka vikao na mbaya zaidi wanazungumzia miradi yake.
Hata hivyo, kundi hilo siyo kutoka Chama cha Mapinduzi tu bali kuna chama cha upinzani ambacho pia wamegawana majukumu ili kuhakikisha kwamba wanammaliza mama huyo, pia inaelezwa kuwa kuna baadhi ya viongozi wa dini ambao wamekuwa wakimfuatilia kwa lengo la kutaka kulisambaratisha kanisa lake ili waumini wake wahamie makanisa yao, alisema mmoja wa wachungaji wake ambaye aliomba jina lake lisichapishwe gazetini.
Aliendelea kusema kwamba, Mchungaji Rwakatare alikuwa akifuatwa siku nyingi na watu wabaya akitoa mfano wa kundi hilo lakini wamekuwa wakigonga ukuta kwani huwa anamuomba Mungu ili aepushe mambo hayo na amekuwa akifanikiwa.
Aliendelea kusema kwamba Mchungaji Rwakatare ni mtu wa watu na amekuwa akiisaidia jamii kiroho. Pia katika maendeleo amekuwa mmoja kati ya wanawake wanaowasaidia wananchi.
Waandishi wetu walimtafuta Mchungaji Rwakatare kwa njia ya simu, walipompata na kumuuliza kuhusu madai ya kuugua na kulazwa pamoja na kufuatwafuatwa, alikiri.
Ni kweli nilikuwa naumwa nikalazwa na kuwekewa drip lakini kwa sasa naendelea vizuri ila yote namuachia Mungu, alisema Mchungaji huyo kwa ufupi na kuomba aachwe apumzike.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa makundi yanayomtia presha Mchungaji Rwakatare yapo katika matabaka mawili ambayo ni wafanyabiashara na wale wanaojiita waumini wa dini za kilokole na ndiyo wanaodaiwa kutaka kummaliza kiongozi huyo.
Mchungaji Rwakatare aliteuliwa na Rais Kikwete kwa mara ya kwanza mwaka 2005 kuwa Mbunge wa Viti Maalum wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na mwaka huu aligombea na kufanikiwa kuwa Mbunge wa Viti Maalum kwa tiketi ya chama hicho.
Habari zinadai mara baada ya Mchungaji huyo kufanikiwa kuukwaa ubunge pamoja na wafuasi watano wa kanisa lake katika uchaguzi mkuu uliomalizika Oktoba mwaka huu, baadhi ya viongozi wa kisiasa kwa chuki zao hawakufurahia hatua hiyo.
Tuna ushahidi kwamba vikao vinafanyika kuwaundia kashfa walioshinda kwa kisingizio kwamba walisaidiwa na mchungaji kwa upendeleo na kwa udini jambo ambalo linadaiwa si la kweli, alisema mmoja wa wabunge hao walihojiwa na gazeti hili hivi karibuni.