Alitokea mchawi, kawaroga watu hawa.
Akawapa ukiziwi, na magonjwa yaso dawa.
Kawafanya wawe kiwi, ndege wasio na mbawa.
Mchawa alipania, kuwatesa si kuua.
Kawaroga mashujaa, kafanya wawe wanyonge.
Kawaroga wenye njaa, kwa uchawi wa matonge.
Karoga saa na taa, kuvizuzua viringe.
Mchawi alipania, kuwatesa si kuua.
Kawafisha kiurongo, kawafanya mizukule.
Amewaroga ubongo, kwa wao akili nywele.
Karoga jino na pengo, vya kumung'unya ndo wale.
Mchawi alipania, kuwatesa si kuua.
Kawatupia majini, mengi ya'so na idadi.
Akawatenda kihuni, hata kipofu shahidi.
Wanaenda hawaoni, karoga kichwa na bodi.
Mchawi alipania, kuwatesa si kuua.
Anga za malenga.