Nimeipata hii kutoka gazeti la raia mwema:
Mgogoro wa nani ana haki ya kuchinja umekuwa ukifukuta Mkoani Mwanza tangu Mei mwaka jana baada ya kulipuka wakati wa mazishi ya mzee Kamuli ambaye alikuwa muumini wa Kanisa la AICT Nyehunge. Katika msiba huo mchungaji wake, James Lutambi, alichinja ng'ombe kwa ajili ya kitoweo msibani.
Waislamu waliohudhuria msiba walihoji nani aliyekuwa amechinja wakaambiwa ni mchungaji. Wakataka kujua kwanini amechinja, yakatokea majibizano kidogo kabla ya waislamu kuondoka na kisha wakamwandikia Mtendaji wa Kijiji barua ya kutangaza kujitenga kushirikiana na wakristo katika misiba na sherehe.
Baada ya tangazo hilo, wakristo nao wakaamua kuwa na bucha yao. Baada ya kushughulikiwa katika ngazi mbalimbali za uongozi tangu katika kata hadi wilaya na kutopatikana suluhu, ndipo alipolazimika kwenda Mkuu wa Mkoa ambaye ni kama alikwenda kuuwasha moto zaidi badala ya kuutuliza.
Inaelezwa na baadhi ya wananchi wa Nyehunge kwamba Desemba 31, 2012 mchungaji Paul Range wa kanisa la EAGT alikamatwa na polisi na kuwekwa mahabusu kwa kosa la kuchinja ng'ombe machinjioni. Pamoja naye, mmiliki wa ngombe huyo naye aliwekwa mahabusu kwa kosa hilo hilo, tukio hilo lilisababisha pia Mkuu wa mkoa wa Mwanza kuamuru mtendaji wa kijiji cha Nyehunge kufukuzwa kazi kwa kushindwa kudhibiti uchinjaji huo.
Source: Raia Mwema