Mengo Operation

Mengo Operation

Comred Mbwana Allyamtu

JF-Expert Member
Joined
Jun 28, 2016
Posts
351
Reaction score
887
"OPERATION STORMED MENGO", NI OPERATION ILIOSUKWA NA MILTON OBOTE KUTAMATISHA UTAWALA WA BAGANDA, NA KUMPINDUA EDWARD KABAKA MUTESA II.

Na. Comred Mbwana Allyamtu
Friday -25/1/2019
Marangu,Kilimanjaro-Tanzania

Miaka 50 iliyopita, yani tarehe 21 Novemba, 1969, Sir Fredrick Edward Kabaka Mutesa Rais wa kwanza wa Uganda alianguka ghafra nyumbani kwake, katika kitongoji cha Bormandsey, London na kupoteza maisha. Baada ya mwili wake kufanyiwa postmortem ilibainika kuwa kifo chake kilitokana na mwili wake kuwa na sumu nyingi mwilini mwake, ripoti hiyo ya kifo chake inasema sumu hiyo ilitokana na unywaji wa pombe kali alizokuwa akitumia alipo kuwa hai.

Huyu Edward Kabaka, alikuwa mtawala wa watu wa kabila la Baganda, huko nchini Uganda, lakini baada ya uhuru wa Uganda mwaka 1962, aliteuliwa kuwa rais asiyekuwa na mamlaka (ceremonial president) chini ya Waziri mkuu Dr, Apollo Militon Obote, Kabla ya kupinduliwa Juni 1966 na kukimbilia uhamishoni Uingeraza, ambako huko aliamua kuishi katika eneo la makazi ya watu maskini, katika kitongoji cha Bormandsey kusini jijini London nchini Uingeraza.

Turejee Uganda, tarehe aifahamiki vizuri, lakini ilikuwa ni miaka ya 1962,Wakati Uganda inapata uhuru Kabaka alikuwa amehitimu elimu yake Chuo kikuu cha Cambridge, Uingeraza na kutunikiwa cheo cha Luteni Kanali wa heshima katika kikosi maalumu cha walinzi wa malikia Elizabeth ll kilichoitwa Grenadier. Lakini mapema mwaka huo huo mara baada ya uhuru wa Uganda aliondolewa cheo hicho na malkia, lakin alibakizwa na cheo cha "Sir".

Wakati ule Uganda ilipopata uhuru 1962, utakumbuka kuwa ufalme wa Buganda ulikuwa ukijiendesha wenyewe ndani ya shirikisho la Uganda. Kulikuwa na serikali ya ubia ya chama cha Uganda Peoples Congress (UPC) cha Dr Milton Obote na kile cha Kabaka Mutesa kilichoitwa Yekka, cha rais wa nchi, Edward Kabaka Mutesa, ambapo vyama hivo viwili vilishilikiana kuunda serikali.

Ushirika wao ulikuwa wa lazima kufatia kuwa kabila la Baganda, walikuwa na ushawishi mkubwa katika uhuru wa Uganda kufatia himaya ya Baganda yenyewe. Ukiachilia mbali hilo Uingeraza iliwaamini sana viongozi wa kimila kutoka Baganda, nguvu kubwa ya chama cha Obote UPC, iliitaji ushiriki wa chama cha YEKKA katika kufanikisha kuunda serikali. Mivutano mikubwa baina yao hatimae waliunda serikali iliyokuwa na makandokando mengi.

Hiyo serikali ya mseto ilianguka 1964 kwa sababu ya mvutano baina ya Obote na Kabaka, baada ya mbunge wa chama cha Mutesa YEKKA aliyeitwa Daudi Ochieng kupelekwa muswada bungeni kuomba bunge liteue tume ya uchunguzi dhidi ya Obote. Obote katika kujibu mapigo akapanga kuidhofisha utawala wa Baganda, Obote alipanga kura ya maoni kuyauliza majimbo mawili ya Buganda iwapo yabaki ndani ya ufalme wa Buganda au yarejeshwe kwenye ufalme wa Bunyoro lengo la Obote ilikuwa ni kuipunguzia nguvu Ufalme wa Baganda ndani ya serikali yake. Kabaka aliipinga kura ya maoni. Obote alishikilia ifanywe. Ilipofanywa, yale majimbo mawili yaliamua yarejeshwe Bunyoro, hali hiyo ikachochea zaidi mgogoro wao.

Kufikia 1966, Obote alikabiliwa na mgogoro mwingine. Kulizuka mvutano ndani ya chama chake na mvutano huo ungeweza kumuondoa kwenye madaraka ya uwaziri mkuu kufatia tuhuma ya Obote kuhusika katika kushirikiana na waasi nchini Kongo DRC kuiba madini ya dhahabu. Baada ya kuona hali hiyo Obote akaamrisha viongozi watano wa chama chake waliokuwa na ushawishi, wakamatwe na kuwekwa kizuizini. Viongozi hao walikuwa ni Grace Ibingira, Balaki Kirya, Mathias Ngobi, G.B.K Magezi na Dr. Emmanuel Lumu. Halafu akaisimamisha katiba ya shirikisho kwa lengo la kumzulu Kabaka Ili aweze kujitangaza kuwa rais.

Hayo yalitokea Februari 1966. Kufika Mei 1966 bunge la Buganda nalo likajibu mapigo ya Obote ya kufuta katiba ya shirikisho, bunge hilo la Buganda lilipitisha azimio lililosema kwamba kwa kusimamishwa katiba ya shirikisho, Buganda haikuwa tena sehemu ya Uganda, yani likatangaza kujitenga na Uganda, na bunge hilo likaitaka serikali ya shirikisho, yani serikali ya Obote ijiondoe kutoka Kampala, mji mkuu, uliokuwa katika ufalme wa Buganda. Obote alijibu kwa kumpeleka Idi Amin kwenda kuishambulia kasri ya Mfalme, Kasri ya Mengo, akitumia silaha nzitonzito. Baada ya kufaulu mapinduzi hayo, mwaka 1967 Obote alitunga katiba mpya iliyozitengua tawala zote nne za kifalme nchini humo.

Mapinduzi hayo ya Mei, 24 1966, yalipewa jina la "Operation Stormed Mengo", mapinduzi haya yalilatibiwa na Mirton Obote, Waziri mkuu wa kwanza wa Uganda wakati huo pamoja na Iddi Amin Dada. Code name ya mapinduzi haya yaliitwa 'operation stormed mengo' kwa maana kwamba yalikuwa yanakwenda kuteketeza ikulu ya kabaka iliyoitwa "Mengo" iliyopo jijini Kampala, shabaha na uamuzi uliochagiza Obote kumuondoa Kabaka Mutesa kwa njia ya mapinduzi ilikuwa ni hofu yake juu ya mgogoro uliokuwepo baina yao, juu ya nani mwenye madaraka dhidi ya mwingine, kiukweli Obote aliyekuwa Waziri mkuu ndie aliyekuwa na nguvu kikatiba, lakini ushawishi wa Kabaka Mutesa uliotokana na Ufalme kutoka dola ya Buganda ilimpa wasiwasi na tishio sana Obote, pia hali ya kupendelewa kwa Kabaka Mutesa na Waingereza, kulizidi kumpa hofu zaidi Obote.

Kufatia hali hiyo Obote akaanza kulisogeza jeshi karibu, huku akiongeza uswahiba na Iddi Amini, mwanajeshi aliyekuwa na cheo cha kanali, kutokana na uhodari wa Amini ilimfanya Obote kupanga njama za kumuangusha Mutesa madarakani kwa kushirikiana na Amini. Baada ya Mipango na mikakati kukamilika Obote alimkabidhi kazi ya kumpindua Kabaka Mutesa, mkakati huo wa Operation Stormed Mengo ulilenga kumpindua Kabaka Mutesa pamoja na kumuua kabisa.

Operation hiyo ilipangwa Enttebe siku ya tarehe 20, April 1966, mbele ya Obote na Iddi Amini, dulu zingine zinadai kuwa maelekezo ya Obote kumuondoa Kabaka Mutesa madarakani zilitoka Dar Es Salama, kwa Mwalimu Nyerere. Kwani Nyerere alionekana kuwa mtu wa karibu sana na Obote, huku Obote alionekana Kufuata maelekezo mengi Kutoka ikulu ya magogoni. Taarifa za siri zilizo elezwa na Brigadier General Sabama Opolot, ambae alikuwa mkuu wa jeshi la Uganda wakati huo, anasema walipokea maelekezo kutoka kwa Obote, ya kusajili siraha zote zilizotimika na askali walinzi wa rais Kabaka Mutesa, na mbinu hii inaelezwa kutoka nchini jirani, aliongeza kwa kusema "siku mbili Kabla ya mapinduzi ya Mutesa, Obote alipokea sm nyingi kutoka ikulu ya Dar Es Salaam, pia ubarozi wa Uingeraza mwaka 1987 ulisema kuwa tarehe 15, Mei 1966, ulinasa simu ya mazungumzo baina ya Nyerere na Obote, dhidi ya kupanga njama za kumdhibiti Mutesa.

Mipango ilipo kamilika, hatua za kumpindua Mutesa zikaanza, usiku wa Mei 23,1966 kikao kirefu kilifanyika kwenye kambi ya jeshi na polisi ya Kampala, Huku kikao hicho kikiongozwa na Obote, Amin na askali wapatao 62 hivi. Kikao hicho Obote aliwahaidi askali hao kuwapandisha vyeo iwapo wangefanikiwa operation hiyo, Ilipo fika asubuhi ya Mei 24, 1966 uvamizi kuelekea Mengo, makazi ya rais yakaanza, kutokea kwenye kambi ya jeshi ya Kampala Barracks 01 (ambayo kwa sasa ni kituo cha mafunzo ya jeshi Uganda -Uganda military academy)

Turudi katikati ya jiji la Kampala katika eneo la "Mengo" eneo yaliyopo makazi ya rais Mutesa, ilikuwa mapema asubuhi, Mei 24, mwaka 1966 wakati kikosi cha waziri mkuu wa Uganda Apollo Milton Obote yalipo vamia na kufanya shambulizi kwenye makazi ya bwana Fredrick Edward Kabaka Mutesa Rais wa kwanza wa Uganda kufuatia mapambano kati yao ya madaraka. Mkuu wa kikosi hicho alikuwa kanali Idi Amin Dada ,kabaka ambaye bado alikuwa anauchapa usingizi wakati milio ya bunduki iliposikika ghafla nje, akatoka mbio toka kitandani na kuvaa Nguo zake ,akaikimbilia bastola yake baada ya kujua nini kilichotokea.

Akatoka nje ya Ikulu mbio kuwaangalia walinzi wake waliokuwa wakirushiana risasi na kikosi cha Obote ,ingawa hawakuwa wamejiandaa na walizidiwa na wingi wa askali wa Obote, lakini walipambana vizuri. Mapambano yaliendelea kwa masaa kadhaa ,lakini kufika mchana hali ikaanza kuwa mbaya kwa Kabaka na askari wake , askari wake waliokuwa 500 sasa idadi yao ilishuka hadi askari 20.

Askari wa Kabaka walijishauri kama waendelee na mapambano na kufa au watorokee mahali Pengine ambapo watajipanga na kurudi kupambana, wote wakakubaliana wakimbie front, Ili wakajipange. Hivyo wakakimbia kwenye zizi la ng'ombe kupanga jinsi ya kutoroka kwa kuruka ukuta wa Ikulu. Wakati wanaanza kuelekea ukuta wenye urefu wa futi 12 risasi tatu za bunduki zikapigwa ,kabaka na watu wake wakasukumana na kukimbia kuepuka kifo.

Kabaka akapiga magoti na kusali kimya kimya kabla ya kuruka ukuta, akatua chini kwa nguvu na kuvunjika mfupa wake wa mgongoni. Watu wake wawili ,Kapteni Jehoash Katende na George Mallo wakafuatia hadi chini. Mpango wao wa kwanza ulikuwa kuingia Kenya lakini ulinzi na patroo ilikuwa Kali karibu na mpaka wa Kenya wakaamua kuelekea Kongo. Walikimbia kwa wiki mbili njiani huku wakila matunda na chakula walichopewa na wanavijiji kadhaa walio kutana nao njiani, mara wakaingia Bujumbura ,Burundi, kutokea Kongo, wakabaki huko Burundi waliko pewa hifadhi ya muda kwa muda mrefu na kupanga kutorokea London, Uingeraza, mwishoni mwa Juni ,1966.

Kabaka akabakia ukimbizini, London, hadi kifo chake mwaka 1969. Sababu ya kifo chake Kulingana na Ripoti ya mchunguzi wa maiti yake, ilisema kuwa chanzo cha kifo chake Ilikuwa ni sumu Kali ya pombe, pia Daktari alisema kwamba kiwango cha ulevi ilikuwa juu sana, kwani ilikuwa miligramu 380 kwenye damu ya kabaka na kuwa hali ilikuwa mbaya sababu ya Sumu ilipolinganishwa na uzito wake wa mwili wa kg 63 na urefu wake wa futi 5.6, ilionesha kuwa kiwango hicho cha sumu ilikuwa kali kupindukia.

Habari za kifo cha Kabaka zilitangazwa redioni katika habari za asubuhi kupitia Radio ya Uganda. Kufatia uhasama na Obote, Serikali ya Obote ikakataa kusimamia mazishi na ombi la kulejeshwa mwili wa kabaka kuzikwa Uganda, Mwili wake serikali ya Uingeraza iliamua kuuzika huko huko Uingeraza, mwili wa kabaka ulizikwa katika makaburi ya "Kensal Green" London kwa miaka miwili mpaka mwaka 1971, wakati wa utawala wa Iddi Amin maiti yake ilifukuliwa na kurudishwa Kampala, Uganda na kupewa mazishi ya kitaifa chini ya amri ya Idi Amini.

Baada ya mwili wake kurejeshwa Uganda kwa mazishi upya, matangazo yalitolewa kwa kuwaomba watu kushiriki katika kutoa heshima kwa kabaka, mamia ya wanaume na wanawake walioomboleza kwa kusanyika nje ya jengo la Kasubi ambapo mazishi ya Wafalme wa Buganda hufanyika, pia mahali hapo panajulikana kama "eneo la kumbukumbu la makaburi ya Kasubi". Karibu ofisi zote zilifungwa mjini Kampala, maduka yalifungwa kuonesha ishara ya heshima, pia mechi ya mpira wa miguu Kati ya timu ya taifa Uganda iliyokuwa ikicheza na timu ya Cameron katika uwanja wa "Kampala Stadium" ilifutwa kupisha mazishi ya kabaka.

Kabaka Mutesa aliwaacha wanawake kadhaa (zaidi ya wanne) na watoto karibu tisa, watoto watatu kati yao waliishi nchini Uingeraza na kusoma elimu yao huko huko nchini Uingereza.Pia aliacha nyuma kumbukumbu zake kadhaa Ikiwa ni pamoja na vitabu kadhaa alivyo jaribu kuchapisha pamoja na vingine vilivyo kuja kuchapishwa baadae, lakini pia vitabu vingine hukuweza kuvichapisha kwa kukosa fedha.

Wakati wa utawala wa Yoweri Kaguta Museveni alitangaza kumpatia heshima ya kitaifa, kwa kumtangaza Mutesa kama kiongozi shujaa wa uhuru, katika jiji la Kampala na miji mingine nchini Uganda, mitaa kadhaa imepewa jina lake. Huku eneo la Mengo limehifadhiwa kama makumbusho ya kitaifa, kaburi lake la Kasubi ni eneo la makaburi ya heshima ndani ya himaya ya Baganda na Uganda Pia.


Email- mbwanaallyamtu990@gmail.com
FB_IMG_1557210051455.jpeg
FB_IMG_1557210056239.jpeg
FB_IMG_1557210078432.jpeg
FB_IMG_1557210070770.jpeg
FB_IMG_1557210074222.jpeg
FB_IMG_1557210084765.jpeg
FB_IMG_1557210091220.jpeg
 
Back
Top Bottom