Makanyaga
JF-Expert Member
- Sep 28, 2007
- 11,129
- 7,321
Kampuni moja ya chakula mjini San Francisco, nchini Marekani, imevumbua mfumo wa kukuza nyama ya kuku katika maabara, kutokana na seli ya unyoya wa kuku.
Ladha ya nyama hiyo ni sawa na ile ya kuku wa kawaida, tofauti ni kwamba hii imekuzwa kitaalamu katika maabara kutokana na seli ya mnyama.
Wanasayansi wanasema kuwa inachukua karibu siku mbili kutengeneza vipande vya nyama ya kuku katika maabara kwa kutumia protini ili kuiwezesha seli kupata umbo la nyama kadri inavyokuwa.
Ofisa mkuu mtendaji wa shirika linalojihushisha na mpango huo, Josh Tetrick, anasema majaribio ya kuuza nyama hiyo katika migahawa mikubwa duniani yataanza kufikia mwisho wa mwaka huu.
Mbali na hilo, Tetrick anasema wanatengeneza vitu kama mayai au barafu iliyo na krimu au siagi kutokana na mimea, sawa na jinsi wanavyo tengeneza nyama kutokana na nyama, hivyo hakuna haja ya kuangamiza wanyama.
Anasema walitoa nyama hiyo kwa migahawa maarufu duniani ya McDonalds au KFC, ili kuijaribu katika mapishi yao na matokeo yalikuwa mazuri sana.
Tetrick na wajasiriamali wengine wanaotengeneza nyama mbadala kwa kutumia njia ya kisayansi, wanasema lengo lao ni kusitisha uchinjaji wa wanyama na kuhifadhi mazingira.
Umoja wa Mataifa (UN) unasema kufuga wanyama kwa ajili ya chakula ni moja ya vitu vinavyochangia ongezeko la joto duniani pamoja na uharibifu wa mazingira.
Dk. Uma Valeti, mtaalamu wa magonjwa ya moyo ambaye pia ni mwanzilishi wa kampuni maarufu ya utengenezaji nyama ya Memphis, jijini California, anasema watu huchinja wanyama bilioni 70 kila mwaka ili kuwalisha watu bilioni saba.
Anasema ongezeko la mahitaji ya nyama duniani limefika kiwango cha juu, huku kukiwa na hofu kwamba watu watashindwa kufuga wanyama.
“Kile tunachoweza kufanya ni kukuza nyama ya aina yoyote katika maabara, iwe ni ya kuku au samaki moja kwa moja kutokana na seli ya wanyama hao,” anasema.
Wamarekani wengi wanasema hawali nyama lakini takwimu kutoka wizara ya kilimo nchini humo zinaashiria kuwa wanakula kilo 100 za nyama nyekundu na kuku zaidi ya jinsi walivyokula bidhaa hiyo miaka ya 1970.
Mwanasayansi Mark Post ambaye ni mwanzilishi wa bidhaa za kilimo zinazokuzwa kwa njia ya kisayansi nchini Ujerumani, anasema maabara yake ya kwanza iliunda hamburger, kwa gharama ya dola 300,000 sawa na (£228,000), mwaka 2013.
Anasema gharama hiyo ni ya juu sana hali ambayo inawatia hofu wanasayansi wengi kujiingiza katika biashara hiyo.
Kuna mataifa kadhaa ya Ulaya na Asia ambayo yameshauriana na Dk. Valeti kuhusiana na suala la kutengeneza nyama katika maabara.
Dk. Valeti anasema:
“Nadhani mataifa yanataka kuwekeza katika mfumo huu iwe ni kwa ajili ya kukabiliana na upungufu wa chakula au kuimarisha uchumi wao.”
Anasema siku zijazo anatazamia kutengeneza nyama hiyo katika viwanda vikubwa, badala ya maabara.
Huku mjadala kuhusiana na nyama inayokuzwa kupitia njia ya kisayansi ukiendelea kushika kasi, baadhi ya wafugaji wanahoji jinsi bidhaa hiyo itakavyouzwa.
Wanauliza kama ni nyama safi, ina protini safi au nyama ya kawaida tu! Wanauliza hivyo wakitafuta mantiki ya nyama bila mnyama kuchinjwa!
BBC