JanguKamaJangu
JF-Expert Member
- Feb 7, 2022
- 2,780
- 6,607
Serikali kupitia Wizara ya afya imesema kuwa Mpaka sasa hakuna mgonjwa aliyetambulika na kuthibitika kuwa na ugonjwa homa ya nyani (Monkeypox) hapa nchini.
Kauli hiyo imebainishwa na Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Aifello Sichalwe leo Mkoani Manyara wakati akitoa taarfa kuhusu Ugonjwa wa Homa ya Nyani (MonkeyPox) ambapo hivi karibuni Shirika la afya Duniani (WHO) lilitangaza kuwepo kwa ugonjwa huo katika baadhi ya nchi Duniani.
Amesema, Ugonjwa huo unaoambukizwa na virusi vya Monkeypox na dalili za ugonjwa huu mara nyingi huonekana kuanzia wastani wa siku 5 hadi 21 tangu mtu apate maambukizi.
Aliendelea kusema kuwa, dalili kuu za ugonjwa huu ni pamoja na vipele ambavyo vinaweza kuwa na majimaji au usaha, kichwa kuuma, homa, mwili kuchoka, na wakati mwingine inaweza kupelekea kifo hasa kwa watoto wachanga na upungufu wa kinga mwilini.
Mara nyingi ugonjwa huwa si mkali na wakati mwingine hufanana na tetekuwanga, na hupona bila dawa ndani ya wiki chache. Amesisitiza Dkt. Sichalwe.
Aidha, Dkt. Sichalwe amesema, kuwa ugonjwa huu unaambukizwa toka kwa wanyama jamii ya nyani, panya na kindi ambao hubeba virusi vya ugonjwa wa monkeypox, huku akiweka wazi kuwa, mtu mwenye maambukizi anaweza kuambukiza watu wengine pale anapokuwa na dalili.
“Hivyo ni vyema wananchi wakaondoa hofu maana Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wanaendelea kufuatilia hali ya ugonjwa huu katika nchi unakotokea.” amesema Dkt. Sichalwe.
Sambamba na hilo Dkt. Sichalwe amesema, madhara ya ugonjwa huu ni pamoja na kifo (case fatality rate), huku akiondoa hofu kuwa, madhara ya kifo sio makubwa na kusema wakiugua wagonjwa 100, watatu hadi sita ndiyo wanaweza kufariki na mara nyingi ugonjwa hupona wenyewe.
Aidha, ameeleza hatua ambazo Wizara ya Afya imechukua tangu kuanza kwa visa vya ugonjwa huo maeneo mbalimbali ya dunia hasa DRC na Ulaya ikiwemo kuandaa mpango ndani ya saa 72 wa kukabiliana na ugonjwa huu kama utatokea na kuandaa mwongozo wa matibabu ambapo utatumika iwapo mgonjwa akitokea.