KERO Mgao mkali wa Maji katika Mtaa wa PPF, Kata ya Kiseke – Ilemela Mwanza

Hii ni kero ambayo mwananchi ameiwasilisha JF akitaka wahusika kuchukua hatua
A

Anonymous

Guest
Naomba kuwasilisha kilio cha wananchi wa Mtaa wa PPF, Kata ya Kiseke ndani ya Manispaa ya Ilemela kuhusu tatizo kubwa la ukosefu wa maji ambalo limekuwa likiendelea kwa muda mrefu sasa.

Kwa sasa eneo hili hupata maji mara moja tu kwa wiki, mara nyingi siku ya Jumatano pekee. Wakati mwingine hata wiki nzima hupita bila maji kupatikana kabisa. Hali hii imekuwa ikiwasababishia wananchi mateso makubwa na maisha kuwa magumu sana.

Kutokana na ukosefu huo wa maji, wananchi hulazimika kununua maji kwa gharama kubwa kati ya Tshs 500 hadi 1,000 kwa dumu moja, jambo ambalo ni mzigo mkubwa hasa kwa wananchi wenye kipato cha chini. Wengine hulazimika kutegemea maji ya visima vilivyo mbali na maeneo yao, hali inayohatarisha afya pamoja na kuongeza usumbufu mkubwa wa maisha ya kila siku.

Cha kusikitisha zaidi ni kwamba wakati mwingine huduma ya maji hupatikana chini ya mara nne kwa mwezi mzima. Mfano, katika miezi ya Machi na Aprili, eneo hili lilipata maji kwa siku mbili pekee ndani ya mwezi mzima. Hii ni hali ya kusikitisha sana kwa wananchi wanaolipa huduma na kuendelea kuhitaji maji kwa matumizi ya kila siku.

Kata ya Kiseke ipo karibu na Jiji la Mwanza pamoja na miundombinu muhimu ya Serikali, lakini bado wananchi wanaendelea kupata shida kubwa ya maji kana kwamba eneo hili halitambuliki kabisa katika huduma za msingi.

Tunaomba mamlaka husika zisikie kilio cha wananchi wa Mtaa wa PPF na maeneo ya jirani kwa kuchukua hatua za haraka na za kudumu kuhakikisha huduma ya maji inapatikana kwa uhakika kama ilivyo haki ya msingi kwa kila mwananchi.

Naomba kuwasilisha.

Pia soma: MWAUWASA: Kukosekana kwa huduma Uzalishaji na Usambazaji wa Maji Mwanza imetokana na hitilafu ya umeme
 
Mwanza kua na mgao ni swala lisilosameeka.
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…