Mgeni Wangu Uzee

Mzee Mwanakijiji

Platinum Member
Joined
Mar 10, 2006
Posts
33,771
Reaction score
41,027
Uzee kitu adhimu, huo ninauingia
Ujana sasa adimu, Shabani aliusia
Maungoni mwangu humu, uzee unanijia,
Na miye nakusalimu, mgeni wangu uzee!

Mbali ninamuachia, rafiki yangu ujana,
Miaka inakimbia, ya leo siyo ya jana,
Nabaki nakumbukia, nilipokuwa kijana
Na miye nakusalimu, mgeni wangu uzee!

Shabani aliandika, kaulilia ujana,
Ni vipi unamtoka, kashindwa kuung’ang’ana,
Meno yalimdondoka, na nguvu tena hamna,
Na miye nakusalimu, mgeni wangu uzee!

Taratibu waingia, uzee wabisha hodi,
Siwezi kuukimbia, hata niwe mkaidi
Hata nikitukania, ndivyo napigwa baridi,
Na miye nakusalimu, mgeni wangu uzee

Mvi sasa zanijia, nimejaribu kung’oa
Kidevu zasalimia, na miye nazichomoa,
Nikitoa zazidia, nami nazidi kutoa!
Na miye nakusalimu, mgeni wangu uzee!

Mapensi nayaachia, na macheni ya shingoni,
Hereni nilivalia, kwenye sikio jamani,
Mwendo nilibadilia, nilivyonesa njiani,
Na miye nakusalimu, mgeni wangu uzee!

Niliwapata mademu, tena wengine kwa zamu,
Nikaitwa mtaalamu, wa mambo yale matamu
Sasa yanitoka hamu, nanyimwa hata salamu!
Na miye nakusalimu, mgeni wangu uzee!

Nilenda nilipotaka, wasiponitaka nilenda,
Sikuwa na hata shaka, ati mtu kunidunda,
Leo naogopa paka, ninavutwa kama punda,
Na miye nakusalimu, mgeni wangu uzee!

Mwendo wa kudemadema, nikishika natetema,
Uso umenikunjama, natembea nikihema,
Magoti nayo yauma, uzee si lele mama!
Na miye nakusalimu, mgeni wangu uzee!

Kumbe maisha ni hivi, uzee haukwepeki,
Ninazikubali mvi, hata kama sizitaki,
Uzee siyo ugomvi, ujana haushikiki,
Na miye nakusalimu, mgeni wangu uzee!

Kweli nilifurahia, enzi zile za ujana,
Kamwe sintoyarudia, yalopita naagana,
Uzee nakumbatia, kwani lingine hakuna,
Na miye nakusalimu, mgeni wangu uzee!

Nasubiri wajukuu, nione na vitukuu,
Nakunja miguu juu, na mshukuru Mkuu
Kuona umri huu, enzi hizi ni nafuu,
Na miye nakusalimu, mgeni wangu uzee!

Na. M. M. Mwanakijiji (Sauti ya Kijiji a.k.a Vuvuzela Matata)
 
Mzee, tunakuombea kheri kichwani uendelee kuwa kijana. Maana wazee wa soku hizi ndio vinara wa kuharibu mambo.
 
Asante sana Mzee Mwanakijiji kuna mambo hapa duniani hayakwepeki lazima kuyapitia ..ni kujiandaa tu na hii fainali ua uzeeni
 
nakuombea uzee wenye neema mwanakijiji
 
Ujana maji ya moto, wahenga walishasema
Una mambo ya kitoto, wajua baba na mama
Iko pia mikong'oto, ujana si lelemama
Uzee kaukwepeki, ukabili kwa busara

Uwe ni mzee mwema , utushauri vijana
Tena tafuta hekima, kwako tuje kuzivuna
Uepuke kulalama, kama mzee mhina
Kila la heri mzee, na usitoke kijijini.
 
Mwanakijiji utenzi mzuri sana huu.. Ntajaribu kuja angalau na beti mbili
 
Uzee unaupenda, hilo nimeling'amua
ujana hukuupenda, hilo utalijutia
mgongo ukijipinda, mkojo ukikujia
ukatae nakuasa, kamwe usiukubali!

tangu enzi ulisema, uzee marhamu ya moyo
na kwa nguvu ukahema, kakataa ulonayo
kukimbilia hekima, japokuwa kibogoyo
ukatae nakuasa, kamwe usiukubali!

sikubali kuzeeka, hata we miaka mia
ujana sije ucheka, twakutaka Tanzania
chonde nakuomba kaka, badilisha dhahania
ukatae nakuasa, kamwe usiukubali!
 
Hata akiukataa, uzee aukwepeki
Na hata akikomaa, uzee haupingiki
lazima ataukwaa, aonje yake mikiki
Kubali tu yaishe, mzee mwanakijiji.
 
Yesterday 05:10 PM
Topic: Uzee wanijia

by kasimba123

Replies 2 Views 49

Uzee wanijia


Uzee kitu adhimu, huo ninauingia
Ujana sasa adimu, Shabani aliusia
Maungoni mwangu humu, uzee unanijia,
Na miye nakusalimu, mgeni wangu uzee!

Mbali ninamuachia, rafiki yangu ujana,
Miaka...
JANA KATIKA KUZUNGUKA HUMU JF,.HILI SHAIRI NILIANZA KULIONA HUMU,.LILIKUWA POSTED NA MZEE MKJJ,. baadaye nikaliona shairi hilo hilo jukwaa la michezo POSTED by KASIMBA
SASA WHO PLAGIARISED watunzi mtusaidie ,.lakini shairi ni zuri.,

 
Fainali uzeeni, asikuambie mtu!...........
MHHH..mistari haipandi nisiivamie fani.
Hongera mzee..Mwanakijiji!
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…