Herbalist Dr MziziMkavu
JF-Expert Member
- Feb 3, 2009
- 42,872
- 34,363
KWA UFUPI
Mbali na Marwa, ambaye amesoma kozi ya urubani, mshtakiwa mwingine katika kesi hiyo ni Peter Charles Mayalla, ambaye ni mshtakiwa wa pili katika kesi hiyo.
Dar es Salaam. Salimu Mohamed Marwa (25) ni mshtakiwa wa kwanza katika kesi ya mauaji ya mfanyabiashara wa magari, raia wa Ghana, Jose ph Opong.
Mbali na Marwa, ambaye amesoma kozi ya urubani, mshtakiwa mwingine katika kesi hiyo ni Peter Charles Mayalla, ambaye ni mshtakiwa wa pili katika kesi hiyo.
Washtakiwa hawa hao, ambao wote ni wakazi wa Bagamoyo mkoani Pwani wanakabiliwa na kesi hiyo katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, inayosikilizwa na Jaji Njengafibili Mwaikugile.
Wanadaiwa kuwa Septemba 10, 2010, walimuua kwa makusudi Opong, kwa kumkatakata sehemu mbalimbali za mwili, baada ya kumlewesha kwa dawa za kulevya na kisha kwenda kumzika katika msitu wa Kaole.
Awali Marwa, alitiwa mbaroni kwa tuhuma za kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu, baada kukamatwa akiwa na nyaraka za magari ya marehemu Opong katika harakati za kuyauza magari hayo yaliyokuwa Bandarini.
Alikamatwa baada ya mke wa marehemu Opong kutoa taarifa Kituo Kikuu cha Polisi, Septemba 22, kuwa mumewe alikuwa hajaonekana tangu Septemba 9, na kwamba aliondoka kwenda kushughulikia magari yake yaliyokuwa bandarini.
Baada ya taarifa hizo, Polisi walitoa taarifa bandarini kuwa mtu yeyote atakayefika kutaka kutoa magari hayo asiruhusiwe, na Septemba 28, ndipo Salim alipokamatwa akiwa na nyaraka za magari hayo, mkataba wa mauziano na kitambulisho cha marehemu Opong.
Kwanza alipoulizwa kuhusu mahali alipozipata nyaraka hizo alisema kuwa ameuziwa na Joseph Opong, lakini alipoulizwa mahali alikokuwa Opong alijibu kuwa hajui na kwamba baada ya kuuziana, waliachana.
Kuhusu kitambulisho ambacho kilikuwa na jina la Opong lakini kikiwa na picha yake, alishindwa kueleza lolote.
Hivyo kesho yake Septemba 29, timu ya Upelelezi kutoka Polisi Kanda ya Dar es Salaam ikiongozwa na Inspekta (Mkaguzi wa Polisi), Saidi Mohamed Mwagara ilikwenda na mtuhumiwa nyumbani kwake Bagamoyo, kufanya ukaguzi ambao ungewezesha kubaini alikokuwa Opong.
Inspekta Mwagara alidai kuwa hata hivyo katika ukaguzi wao hawakuweza kupata kielelezo chochote cha kuwasaidia, na kwamba wakati wakiwa kwa mtuhumiwa huyo, alimtaka mtuhumiwa awaeleze ukweli kwa kuwa walikuwa wameshachoka.
Alidai kuwa mshtakiwa huyo alisema naye ameshachoka kuzunguka na kwamba sasa anataka awaeleze ukweli, na ndipo akasema kuwa Opong tayari wameshamuua, na kwamba yuko tayari kwenda kuwaonyesha walikomzika.
Aliongeza kuwa kutokana na maelezo hayo kwa kuwa ilikuwa jioni, waliondoka na kwenda katika Kituo cha Polisi Bagamoyo ambapo mshtakiwa aliwaelezea kuhusu tukio hilo na kwamba baadaye usiku aliwapeleka katika Msitu wa Kaole na kuwaonyesha mahali walikokuwa wamemzika Opong.
Inspekta Mwagara aliendelea kudai kuwa waliweka alama katika eneo hilo na kwamba waliweza hata kupata mapanga mawili yaliyotumika kumuulia Opong, kisha wakarudi kituoni.
Alidai kuwa kutokana na maelezo hayo ya mshtakiwa walitoa taarifa kwa viongozi wake kisha wakaomba kibali kutoka kwa Korona (Hakimu wa Wilaya) wakaenda kufukua mahali pale Marwa alipowaonyesha kuwa ndipo walipomzika Opong.
Aliongeza kuwa walipochimba mahali hapo kweli walikuta mwili wa mtu ukiwa ndani ya mfuko mkubwa wa kubebea nguo wenye zipu.
Aliendelea kuwa waliifungua zipu ile wakakuta mwili wa mtu ukiwa umekunjwakunjwa huku ukiwa umekatwakatwa sehemu mbalimbali za mwili, ukiwa umeshaharibika, kisha wakaupeleka katika Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo kwa uchunguzi ndipo ukatambulika kuwa ni wa Opong.
Baada ya tukio hilo alimwagiza Ditektvu Koplo Elia aandike maelezo ya onyo ya mshtakiwa, ambayo mahakama imeyapokea kuwa kielelezo cha ushahidi wa upande wa mashtaka.
Katika maelezo hayo ambayo yalisomwa mahakamani hapo, mshtakiwa Marwa alieleza namna alivyokutana na kufahamiana na Opong, njama na mipango ya kumuua, lengo la kumuua na jinsi walivyofanikiwa kutekeleza mauaji hayo.
Kwa mujibu wa maelezo hayo, Septemba 2, 2010, saa 15.00, mshtakiwa huyo akiwa na rafiki zake Sudi na Abdallah, wakitokea Mwenge wakienda kuuza madini yao, walikutana na mtu ambaye hakuwa akimjua, eneo la Kinondoni Moroko jijini Dar es Salaam.
Mtu huyo alimuuliza mshtakiwa Marwa kwa Kiingereza kama anajua kuongea Kiingereza naye akamjibu kuwa anajua .
Mtu huyo alijitambulisha kuwa anaitwa Joseph Opong na kwamba alikuwa anataka kwenda Bagamoyo lakini alikuwa amesahau kituo cha mabasi ya kwenda huko kwa kuwa alikuwa na muda mrefu tangu alipotoka huko kwa mara ya mwisho.
Mshtakiwa Marwa alimwambia Opong kuwa asiwe na wasiwasi amefika kwa kuwa na yeye ni mkazi wa Bagamoyo. Hivyo alimuuliza kuwa alitaka kwenda kumwona nani na Opong akamjibu kuwa kuna ndugu yake ambaye ni maarufu kwa jina la Mghana.
Mshtakiwa Marwa alisema kuwa alimwambia Opong kuwa anamjua Mghana kwa kuwa anakaa naye jirani na kwamba kutoka kwake hadi kwa ndugu yake huyo ni nyumba ya tatu tu.
​Mghana alivyouawa kinyama Bagamoyo - Habari Ya Ndani - mwananchi.co.tz