Mgombea urais wa Chama cha Wananchi (CUF), Gombo Samandito Gombo, ameahidi kwamba endapo atachaguliwa kuwa rais, atasimamia haki na kuhakikisha rasilimali za Taifa zinawanufaisha wananchi wote bila ubaguzi.
Gombo, ambaye aliambatana na mgombea mwenza wake Husna Mohammed Abdullah, amesema chama hicho kimejipanga kutenda haki kwa Watanzania wote ili wapate stahiki zao katika sekta muhimu kama afya, elimu na maji.
Soma pia:
Tuache masihara keki ya taifa ni tamu, nini kimewatoa makamu wa Rais na waziri mkuu ?
Akizungumza mara baada ya kuchukua fomu ya kugombea, Gombo amesema kwa sasa haki imekuwa ikipotea katika huduma hizo muhimu, na kwamba atakapopewa dhamana, kipaumbele chake cha kwanza kitakuwa kuhakikisha haki inapatikana kwa kila mmoja.
“Sisi kama CUF tunataka kulinda haki ya kupata huduma zote. Keki ya Taifa lazima itanufaishe Watanzania wote ili kuondoa malalamiko ya wananchi,” amesema.
Ameongeza kuwa kwa sasa kuna baadhi ya makundi ambayo yananufaika zaidi kuliko mengine, jambo linalosababisha malalamiko miongoni mwa wananchi, na CUF inakusudia kuondoa hali hiyo pindi ikishika dola.
Source: Nipashe digital