Mwana Halisi washambuliwa
Saed Kubenea akiwa Muhimbili
na Happiness Katabazi
KATIKA tukio linaloweza kutafsiriwa kuwa jitihada za kutisha mhimili wa nne wa utawala, watumishi wawili wa gazeti la Mwana halisi, juzi walivamiwa na watu wasiojulikana, kutishwa, kushambuliwa na kujeruhiwa vibaya.
Katika tukio hilo la aina yake, watu hao watatu, walizivamia ofisi za gazeti hilo, na kuwakuta Mkurugenzi Mtendaji wa Hali Halisi Publishers, kampuni inayomiliki gazeti hilo na jingine la Mseto, Saed Kubenea na Mshauri wa habari wa gazeti hilo, Ndimara Tegambwage, wakiwa katika kazi ya kuandaa gazeti.
Katika mashambulizi yaliyofuatia uvamizi huo, watu hao waliojihami kwa mapanga na rungu, waliwamwagia tindikali waandishi hao na kusababisha Kubenea kujeruhiwa vibaya sehemu za usoni.
Tegambwage alijeruhiwa kwa panga wakati akipambana na wavamizi wawili.
Akizungumza na wanahabari waliofika kumjulia hali katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili katika wodi ya Sewahaji namba 19, Kubenea alisema tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa 2:30 usiku.
Akizungumza kwa taabu, alisema watu watatu wakiwa na panga, sime, rungu na chupa iliyokuwa na tindikali waliwavamia ofisini hapo na kuwajeruhi.
Katika kile kinachoonyesha masikitiko makubwa, Kubenea alieleza kuwa hivi sasa amepoteza uwezo wa kuona na hana uhakika iwapo ataweza kuona tena baada ya matibabu.
Kubenea alisema analihusisha tukio hilo na vitisho ambavyo amekuwa akivipata mara kwa mara kupitia simu yake ya kiganjani kutoka kwa watu wasiowafahamika.
Mmoja wa ndugu wa Kubenea, alisoma moja ya ujumbe huo wa vitisho uliokuwa ukimweleza Kubenea asingeumaliza mwaka jana akiwa hai.
"Nina uhakika kabisa kwamba tukio hili linatokana na simu na ujumbe mfupi niliokuwa naupokea kutoka kwa watu wasiojulikana. Mara kadhaa nimekuwa nikitoa taarifa Polisi Oysterbay, lakini hadi nakumbwa na tukio hili watu hao hawajawahi kutiwa mikononi mwa polisi.
"Mungu akinisaidia nikaweza kuona na endapo polisi watafanikiwa kuwakamata watu hao nina uwezo wa kuwatambua, ila kwa sasa siwezi kuwatambua kwa kuwa ndiyo hivyo tena sioni," alisema Kubenea.
Alisema hivi sasa familia na jamaa zake wanafanya kila liwezekanalo kumpeleka nchini India kwa matibabu zaidi.
Alisema juzi saa 6:45 usiku, baada ya kufikishwa hospitalini hapo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Jamal Rwambow na Kamanda wa Upelelezi wa wilaya hiyo, Damas Kasabi, walikwenda kumjulia hali, na aliwaeleza kwamba tukio hilo analihusisha na vitisho hivyo na waliahidi kulishughulikia.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Juma Duni Haji, ambaye alikuwepo hospitalini hapo, alisema tukio hilo ni kitisho kwa wanahabari, ili wasiendelee kufichua maovu.
"Wanahabari mpo vitani, wapiganaji wawili wamejeruhiwa
Kubenea ni mmoja wa vijana waliokuwa mstari wa mbele kuandika habari za ufisadi
hii ndiyo tabia ya dola, haitaki kukosolewa," alisema.
Wengine waliofika kumjulia hali Kubenea ni Mbunge wa Viti Maalumu, Halima Mdee (CHADEMA), waandishi kutoka vyombo vya habari, ndugu, jamaa na wapenzi wa magazeti ya Mwanahalisi.
Naye Tegambwage, ambaye alijeruhiwa kichwani kwa panga katika tukio hilo, akizungumza na gazeti hili nyumbani kwake Tegeta-Machakani, Mtaa wa Matumbini, alisema alipata jeraha hilo baada ya kukatwa na panga.
Akieleza tukio hilo, Tegambwage alisema wakiwa ofisi hapo na Kubenea, walisikia watu wakigonga mlango wakitaka wafungulie ndipo alipomtaka Kubenea akawafungulie.
"Kubenea alipofungua mlango watu hao walimtaka atoke nje, ndipo Kubenea alipofunga mlango, lakini watu hao walitumia nguvu kuufungua na kufanikiwa kuingia ndani na mmoja kati yao akamwambia Kubenea kwamba alikuwa amemfuata yeye na alikuwa akimtafuta kitambo," alisema Tegambwage.
Alisema mtu huyo alikuwa amebeba chupa yenye kemikali ambayo anadhani ni tindikali, alimmwagia usoni Kubenea. Alisema walimmwagia na yeye lakini macho yake yalisalimika kwa sababu alikuwa amevaa miwani hivyo kemikali hiyo kumwagikia puani na mdomoni.
Alisema walivyoingia, Kubenea wakati anapambana na mtu huyo, mtu mwingine alimrushia panga ambalo alilikwepa na mwingine alimrushia panga jingine ambalo alilipangua na kufanikiwa kuwakamata mashati watu hao wawili hadi kuanguka nao chini.
"Baada ya kuwashinda nguvu ndipo yule aliyekuwa anakabiliana na Kubenea akanipiga panga la kichwa ambapo nyama ilikuwa ikining'inia
wale wenzake wakavua mashati niliyokuwa nimeyashikilia, wakakimbia," alisema Tegambwage.
Alisema watu hao waliacha pia silaha zao, ikiwemo chupa iliyokuwa na tindikali.
Alisema baada ya watu hao kuondoka hawakuwa wakihisi maumivu, licha ya kuamua kwenda kupata huduma ya kwanza katika hospitali binafsi ya Dk. Mvungi iliyopo Kinondoni, ambako alishonwa nyuzi 15 kwenye jeraha alilolipata na wakati huo Kubenea alikuwa akiona kwa taabu.
Baadaye walishauriwa na madaktari kwenda Hospitali ya Muhimbili, ambapo yeye alipelekwa MOI, ambapo alipigwa X-ray na kuruhusiwa.
Tegambwage, ambaye ni mchambuzi mahiri wa mada kupitia vyombo vya habari, alisema anaamini tukio hilo ni mchezo mchafu unaochezwa na baadhi ya watu woga ambao inawezekana wameguswa na uandishi wa magazeti hayo, hivyo kuamua kutumia dhiki za vijana kutenda unyama wa kiwango kile.
"Ninachoelewa vijana wale hawana sababu ya kutujeruhi au kutaka kutuua, isipokuwa wametumwa kutekeleza matakwa ya watu wengine.
"Tendo hili limetokana na uandishi wa habari, hakuna sababu ya kukataa kuwa shujaa
wanahabari wote waendelee na mtindo huo huo, waandike," alisema Tegambwage.
Hata hivyo, alisema waliotumwa kutenda tukio hilo ndio wanaotetewa na vyombo vya habari na waliowatuma wanataka kuangamiza uhuru wa kila mmoja na si wanahabari peke yake.
Hii ni mara ya tatu kwa Kubenea kukumbwa na matatizo, kwani katikati ya mwaka jana watu wasiofahamika walichoma gari lake aina ya Suzuki Escudo.
Katika tukio la pili, akiwa nyumbani kwake Kinondoni akitembea kandokando mwa barabara, aligongwa na gari lisilofahamika na kuanguka chini na baada ya gari hilo kumgonga lilikimbia.
Naye Meneja Utalawa wa magazeti hayo, Yusuf Aboud, aliwaambia waandishi wa habari hospitali hapo kwamba mapema mwezi uliopita kijana mmoja alifika katika ofisi zao na kumuulizia Kubenea ambaye alimtaka atoke nje ya ofisi, kwani alikuwa ameleta habari.
Hata hivyo, Kubenea aligoma kutoka nje na kumtaka mwandishi wake, Iddy Mkwama, aende kuzungumza na kijana huyo.
"Pamoja na Iddy kwenda kumsikiliza kijana yule alisisitiza kumwona Kubenea, kwani alitaka kumweleza kuwa alikuwa kwenye kijiwe kimoja aliwasikia baadhi ya vijana wakipanga njama za kutaka kumdhuru," alisema Aboud.
"Baada ya kijana kusema hivyo, Iddy alirudi kumwita tena Kubenea na walipotoka nje walimuona kijana huyo akikimbia na kuingia kwenye gari aina baloon lililokuwa limebeba watu wengine watatu na kuondoka kwa kasi," alisema Aboud.
Katika hatua nyingine, Katibu wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Mbeya, Christopher Nyenyembe, alilaani tukio hilo, na kubainisha kuwa lina lengo la kuzika uhuru wa habari. Aliwataka waandishi wa habari na wanaharakati kote nchini kuungana kulaani kitendo hicho.
Wakati huo huo, Jukwaa la Wahariri leo limeitisha mkutano na waandishi wa habari utakaofanyika katika Ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) kwa ajili ya kutoa tamko kuhusiana na tukio hilo.
news from Tanzania Daima