SoC04 Miaka 10 ya giza kupisha nuru kutamalaki

SoC04 Miaka 10 ya giza kupisha nuru kutamalaki

Tanzania Tuitakayo competition threads

my nation

Member
Joined
Jul 15, 2021
Posts
71
Reaction score
96
Wanangu, ninaliona jasho lenu la kuusukuma huu ukuta lakini bado hausogei wala kutikisika na moyo wangu unajaa simanzi, nami ninajitahidi kuwaiteni kwa sauti kubwa lakini sauti yangu inaishia kwenye ombwe lililojaa kiza, najitahidi kutuma wajumbe lakini wanaishia kutafunwa na majitu katili waliojaa kwenye dunia ya kiza na wengine kujazwa sumu zinazoendelea kuwafarakanisha, moyo wangu unasononeka na nguvu kuniishia.

Wanangu sina budi kukupa hadithi hii ya kweli ili ujue kwanza pa kuanzia, usitembee kwenye ombwe la kiza lililojaa majitu wasije wakakumeza, mimi nguvu zimeniishia kwani hii minyororo nimefungwa na majitu katili ambao walisusia kuishi kwangu ila wakabeba mali zangu na kuzitumia kujenga kwao.

Wanangu hapo kale tulikuwa wamoja na tulitembeleana bila ya ubaguzi, njaa haikuwepo wala hatukuwa na kiu kwani tulijitosheleza. Wakati tunaumbwa tuligawiwa kulingana na kanda zetu hivyo hakukuwa na aliyepewa pungufu, kwani wote tulipewa sawasawa na haja ya mioyo yetu.

Wanangu kulizuka kizazi kilichojaa wana wenye tamaa na wengi wao walikuwa ndio majitu katili, hao hawakulidhika na mali walizozikuta kwao bali walianza kukusanya mali za wengine, majitu hayo yalikera sana, mwanzoni majitu hayo yalikuja na sura ya utu, uungwana, kugawa misaada na kuinjilisha, wanangu hiyo ndiyo iliyokuwa mitego ya kulainisha mioyo yetu ili wao kusambaza sumu zilizoendelea kuwatafuna wanangu na walivyofanikiwa kusambaza sumu zao walitugawa na hapo ndipo walipoonyesha sura zao halisi, hofu ilitanda moyoni mwangu kwani kiza kilitamalaki, wanangu waligawanyika wasisikilizane, walishindwa kunilinda mimi mama yao pamoja na mali nilizonazo.

Lakini sio wote walioathirika na sumu zao wapo waliosimama pamoja na mimi hadi kufa kwao ili kunitetea mimi pamoja na urithi niliokuwa ninawatunzia wanangu, vita ilitisha sana kwani wanangu waliogoma na kunipambania mimi pamoja na mali zangu dhidi ya hao majitu katili waliishia kunyongwa na kukatwa vichwa vyao ambavyo walivisafirisha hadi kwao ila nashukuru baadhi yenu walipambana na kuvirejesha.

Wanangu mnaotokwa na jasho jingi sana kuusukuma ukuta huu ili kuuangusha kuna moja muhimu ambalo linawakwamisha, hata hivyo siwastaajabii kwa sababu ya kiza kinachowazunguka na kuwafanya mshindwe kuona nyuma ya ukuta huu, wanangu kwa kuwa mna kiu na shauku ya kuona nyuma ya ukuta huu mimi mama yenu ni vema niwaeleze kilichopo kwani kabla ya kuujenga ukuta huu nalikuwapo na kuyaona mazuri mengi, mkifanikiwa kuuangusha ukuta huu mtagubikwa na nuru iliyojaa mema yote niliyowatunzia na mtasahau taabu zote zilizowakumba ntangu kuzaliwa kwenu.

Wanangu ukuta huu nyuma yake umejengewa nguzo zinazoushikilia hivyo ni muhimu nguzo hizo mzing’oe kwanza ili kuweza kuuangusha ukuta huo na kuweza kunufaishwa na mema yaliyozuiliwa na ukuta huu, lakini ni nani wa kuweza kuzing’oa nguzo hizo? Nguzo hizo zinazoushikilia ukuta huu zimejengwa kwa elimu yao iliyojaa ubaguzi wa rangi, kabila, jinsia, dini, kisiasa, kiuchumi, kijamii, kikanda ndio unaowafanya mshindwe kuuangusha ukuta huu.

Labda niwaulize wanangu mko wote hapo? Mbona hamna ushirikiano, mbona wanaume mko wengi kuliko wanawake usawa uko wapi? Jana walijitokeza wengi wanawake mbona leo hawajatokea! Au unadhani sijui!, mhuu!! Niliwaona jinsi mlivyowazuia wasishiriki eti kwa sababu tu ni wake na mabinti zenu, lakini fahamu ya kwamba mmewanyima haki ya kushiriki mapambano ya kuuangusha ukuta ili muweze kula mema ya nchi. Wengine hapa mnajiliwaza huku mkiwa mmewatelekeza watoto wenu, mliwazaa wenyewe lakini mmewaachia mama zao eti tu kwa sababu ninyi mnapambana kuuangusha ukuta, mmejawa na laana za kuzitelekeza familia zenu ndio maana mnatoa jasho la kushindwa badala ya jasho la kufanikiwa, wanangu zilejeeni familia zenu na mzitunze vyema ili hao wana wa kiume na wa kike wakue vyema na kuziunganisha nguvu zao ili kwa umoja wenu muunganishe nguvu kuweza kuuangusha ukuta huu.

Wanangu mnanisikitisha sana mbona hamna lenu moja, mmeamua kuunda vyama ili kumpata kiongozi wa kuhakikisha mnafikia malengo yenu ya kuuangusha ukuta huu, lakini mnakosa umoja, mimi niwashauri nyote ni wanangu msipandikize sera zenye chuki, baba zenu walipambana na kufanikiwa kukata mnyororo mkuu niliokuwa nimefungwa nao kiasi cha kukosa uhuru na wakaazimia kuwa na umoja na mshikamano ili kuangusha ukuta huu ulio salia, lakini ninyi mwajikanyaga wenyewe mpaka nashindwa kuwaelewa mnanipambania hivi ili mpate hayo mema kwa ajili yenu tu na matumbo yenu au ni kwa ajli yenu nyote na wale mliowatelekeza? Wanangu wosia huu niwapatieni ninyi ili mtoke gizani na kuipata nuru iliyojawa na mema ambayo wazee wenu waliipambania tangu mwanzo na kuwachia mapambano hayo mnayoendelea nayo na leo nitawapatia njia nzuri ya kuzing’oa hizo nguzo zilizo nyuma ya ukuta huu zinazowafanya mchelewe kuuangusha ukuta huu na kushindwa kula mema ya nchi niliyowatunzieni ninyi ntangu kuumbwa kwangu.

Wanangu ngoja niwaibie siri ambayo nimekaa nayo kwa muda mrefu sana, niliwatunzia mali nyingi zinazoonekana na zile zisizonekana, labda niendelee kuwafumbua macho yenu japo mpo gizani mali zinazoonekana mfano wake ni kama bahari, maziwa, mito, milima mikubwa mnayoiona kwa upande wenu, hifadhi za wanyama na misitu ya kuvutia na hayo ni machache tu lakini mali zisizoonekana mfano wake ni madini mbalimbali, gesi asilia na mafuta, hayo yote ni mema ambayo nimewahifadhia wanangu.

Wanangu kwa kuwa huo ukuta umejengwa na majitu katili na kuuwekea sumu, mmekuwa mkifarakana ninyi kwa ninyi na kushindwa kufikia lengo lenu hivyo ni mhimu kufahamu ukuta huo umejengwa kwa elimu yao ambayo sisi ndio tunawafundishia wanetu mashuleni ni lazima tuupitie mfumo wa elimu mnao wafundishia wana wenu ili kung’oa baadhi ya mizizi inayowachelewesha kufikia malengo na kuweka baadhi ya mitaala ya kale itakayo saidia kuwajenga wana wenu.

Hakikisheni ndani ya miaka hii kumi mnakuwa na umoja na mshikamano ili kuhakikisha mnashikamana katika kuuangusha ukuta huu,
ondoeni kati yenu ubaguzi wa kijinsia ili kuhakikisha wanaume na wanawake, watoto wenu wa kike na wakiume mnashikamana vyema katika kuzing’oa nguzo na vigingi vya kuwakwamisha kuuangusaha ukuta huu, vyama vyote vya siasa mlivyoviunda hakikisheni mnasikilizana na kupeana mbinu ili kuhakikisha nyote mnashiriki kuusukuma ukuta na kuzing’oa hizo nguzo ili nyote muangaziwe na hiyo nuru iliyojaa mema ya nchi.

Wanangu ninyi ni watoto wasikivu na watiifu, kwa haya yote na mbinu zote nilizowapeni ni hakika baada ya miaka hii kumi kupita mtaangaziwa na nuru iliyojaa mema ya nchi na kwa umoja wenu ninyi nyote na watoto wenu mtanufaika nayo, niwatakieni kila lakheri kwenye mapambano yenu ya kuuangusha ukuta huu ili mtoe jasho lenye mafanikio, ni mimi mama yenu TANZANIA.​
 
Upvote 5
Back
Top Bottom