Miaka 20 bila Nyerere: Machache kutoka historia ya safari ya kwanza ya Mwalimu Nyerere, Lindi 1955

Miaka 20 bila Nyerere: Machache kutoka historia ya safari ya kwanza ya Mwalimu Nyerere, Lindi 1955

Mohamed Said

JF-Expert Member
Joined
Nov 2, 2008
Posts
21,967
Reaction score
32,074
MIAKA 20 BILA NYERERE:
MACHACHE KUTOKA HISTORIA YA SAFARI YA KWANZA YA MWALIMU NYERERE LINDI 1955

Kumbukumbu ya Miaka 20 bila ya Baba wa Taifa imeadhimishwa leo mjini Lindi lakini si wengi wanaoijua historia hii kwa ukamilifu wake.

Hii ni fursa nzuri kwetu sisi kujikumbusha hali ya siasa ilikuwaje miaka ile Mwalimu Nyerere alipokanyaga Lindi mwaka wa 1955 katika harakati ya kukijenga chama cha TANU na kupigania uhuru wa Tanganyika.

Kisa ni kirefu lakini tutosheke na haya machache:

Nyerere na msafara wake wa Ali Mwinyi Tambwe na Rajab Diwani ulipokelewa na uongozi wa TANU wa Lindi huko Mbanji, kijiji kidogo nje ya mji.

Msafara wa Nyerere ulipowasili Mbanji ilikuwa kiasi cha saa moja jioni hivi na giza lilikuwa linaanza kutanda.

Mbali na Salum Mpunga na Ali Ibrahim Mnjawale wajumbe wawili waliokutana na Nyerere mjini Dar es Salaam kwenye mkutano wa mwaka wa TANU uliofanyika Ukumbi wa Hindu Mandal hakuna hata mtu kati ya umma ule uliokuja kupokea ujumbe kutoka makao makuu ya TANU aliyekuwa anajua Nyerere anafanana vipi.

Mpunga, dereva wa lori, alijibagua kutoka kwa lile kundi la watu akawa amesimama pembeni ili Nyerere apate kumuona. Baada ya Nyerere kumtia Mpunga machoni, Mpunga alimwendea kumsalimu Nyerere, Tambwe na Diwani; kisha aliligeukia lile kundi la watu kumtambulisha Nyerere kwa wananchi akilitaja jina lake kwa sauti kubwa.

Baada ya hapo aliutambulisha ule ujumbe wa Nyerere.

Nyerere na ujumbe wake ulisindikizwa kwa shangwe na kundi la watu hadi ofisi ya TANU kwenye nyumba ya Suleiman Masudi Mnonji Mtaa wa Makonde.

Kupakana na ofisi ya TANU ilikuwepo nyumba ya seremala mmoja mwanachama shupavu wa TANU, Issa bin Ali Naliwanda.

Hii ndiyo nyumba iliyochaguliwa alale Nyerere na ujumbe wake, si kwa sababu ilikuwa nzuri kupita zote.

Ilichaguliwa na kupewa heshima hii kwa sababu ilikuwa karibu sana na ofisi ya TANU na hivyo basi ilirahisishia TANU kazi ya ulinzi wa Nyerere.

Siku iliyofuata ilikuwa Jumapili na Nyerere aliwaomba wenyeji wake apelekwe kanisani kwa ajili ya ibada.

Kanisa Katoliki mjini Lindi ni jengo la fahari lililoko ufukweni katika Bahari ya Hindi.
Lindi ulikuwa mji wa Waislam.

Mbali na mlio wa kengele za kanisa hakuna mtu pale mjini aliyekuwa akishughulishwa na kile kilichokuwa kikifanyika kwenye viwanja vya kanisa.

Watu wachache waliokuwa wakienda kusali kanisani walikuwa Wakristo waliokuja Lindi kutoka sehemu nyingine za Tanganyika kufanya kazi katika ofisi za serikali.

Ghafla mahala hapa palipokuwa pweke, palipopuuzwa kwa miaka na Waislam wa mjini, pakawa muhimu kwa sababu rais wa TANU ambae alikuwa Mkatoliki alikuwa na haja ya kuhudhuria ibada pale kanisani.

Hakuna mtu katika uongozi wa TANU wa Lindi aliyejua ndani ya kanisa lile kulikuwa vipi wala hapakuwa na yoyote kati yao aliyewahi kuingia ndani ya kanisa, si Lindi wala mahali popote pale.

Uongozi wa TANU wa Waislam mjini Lindi haukumwamini Mkristo yoyote kumsindikiza Nyerere kanisani ili kumpa ulinzi. Baada ya kujadili suala hilo kwa urefu hatimaye iliamuliwa kuwa Mpunga na wanachama wachache Waislam wenye kuaminika lazima wamsindikize Nyerere kanisani na wengine wabakie nje kulinda mlango.

NYERERE MKUTANO WA TANU 1955 HINDU MANDAL HALL DAR.jpg

Picha: 1. Mkutano wa kwanza wa TANU wa mwaka 1955 Dar es Salaam

SALUM MPUNGA.jpg

2. Salum Mpunga​
 
Back
Top Bottom