Samata apeleka huzuni Lyon Thursday, 03 February 2011 22:16
Sweetbert Lukonge
MABINGWA watetezi Simba wameamka usingizini na kuichapa African Lyon mabao 3-0 kwenye Uwanja wa Uhuru, huku kipa Juma Kaseja akiwa amekaa benchi kwa mara ya pili mfululizo.
Mshambuliaji chipukizi Mbwana Samatta alipachika mabao mawili dakika ya 46 na 82 dhidi ya timu yake ya zamani wa Lyon baada ya baada ya Amri Kiemba kufunga bao la mapema katika dakika ya 5.
Kocha Patrick Phiri alishindwa kumtumia Samatta kwenye mchezo wake wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Elan ya Comoro na kushuhudia washambuliaji wake wakongwe wakipoteza nafasi nyingi za kufunga kutokana na ubinafsi.
Phiri jana alimpumzisha mshambuliaji wa kimataifa wa Uganda, Emmanuel Okwi na kumuanzisha Samatta na Musa Mgosi mfungaji bora wa msimu uliopita.
Ilimlazimu MzambiaPhiri kusubiri hadi kipindi cha pili kuona matunda ya chipukizi huyo Samata aliyemsajili kutokea Lyon akipachika bao lake la kwanza kwa juhudi binafsi baada ya kuwalamba chenga mabeki kutokea katikati ya uwanja kabla ya kupiga shuti na kufunga bao hilo dakika 46, kabla ya kuunganisha krosi ya beki Haruna Shamte na kupachika bao la tatu dakika 82.
Awali winga Amri Kiemba alimalizia kwa umakini mpira uliokuwa umetemwa na kipa wa Lyon, Noel Lucas aliyepangua shuti la Jerry Santo dakika ya 5 na kuwapa Simba goli la mapema.
Simba iliyolazimishwa suluhu ugenini na Elan ya Comoro mwishoni mwa wiki kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa ilionyesha kubadilika jana wakati Lyon iliyojaa chipukizi na ilitawala mchezo huo.
KASEJA
Kipa namba moja wa Taifa Stars, Juma Kaseja kwa mara ya pili mfululizo alikuwa kwenye benchi na kumtazama Ally Mustapha akiendelea kuweka rekodi ya kutoruhusu goli katika mechi nyingine.
Kaseja tangu aliporuhusu mabao matatu kwenye mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Azam amejikuta kwenye wakati mgumu mbele ya mashabiki wa Simba pamoja na benchi la ufundi.
Hivi karibuni kocha Patrick Phiri alikaririwa akisema kuwa kipa huyo kipenzi cha Watanzania wengi amechoka na anahitaji kupumzika zaidi, jambo lililomfanya ashindwe kumtumia kwenye mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Elan ya Comoro mwishoni mwa wiki.
Mwamuzi wa mchezo huo,Oden Mbaga alilazimika kusimamisha mchezo kwa dakika tano baada ya kipa wa Lyon, Lucas kuumia kufutia kugongana na Kiemba katikati ya kipindi cha kwanza.
Pamoja na ushindi huo Simba imeendelea kubaki kwenye nafasi ya pili baada ya kufikisha pointi 30, wakiwa na mchezo moja mkononi, huku wapinzani wao Yanga wanaondamwa na migogoro kwa sasa wakiongoza kwa tofauti ya pointi moja.
Azam wao watakuwa kwenye mazingira mazuri ya kuota kutimiza ndoto yao ya kumaliza kwenye nafasi mbili za juu endapo watashinda leo dhidi ya Toto Afrika mchezo utaofanyika kwenye Uwanja wa Uhuru.
Mara baada ya mechi,kocha Phiri wa Simba alisema amefurahishwa na ushirikiano mzuri ulioonyeshwa kati ya Mgosi na Samata na ushindi huo ni ishara njema kwa timu yake.
"Tunataka kuitumia michezo yetu ya ligi kama sehemu ya maandalizi yetu ya mchezo wa marudiano dhidi ya Elan, unapoona wachezaji wamecheza kwa ushirikiano hivi ni jambo zuri."
Naye kocha wa Lyon, Jumanne Chale alisema lengo lake ni kuinusuru timu yake isishuke daraja msimu huu ili waweze kujipanga kwa msimu mpya.
"Kwa sasa tunapigana tutusishuke daraja, tumejipanga kuhakikisha tunashinda mechi zilizobakia ili kujinasua na balaa la kushuka daraja tu," alisema Chale.
Wasanii litumieni vema tamasha la Sauti za Busara
SIKU tano zijazo kisiwa cha Unguja kinatarajiwa kuanza kuhanikizwa kwa raha za aina yake pale tamasha la nane la Sauti za Busara kwa mwaka 2011 litakapozinduliwa rasmi.Tamasha hilo linalokusanya wasanii mbalimbali kutoka ndani na nje bara la Afrika, limepangwa kuanza kulindima kuanzia Jumatano ijayo, yaani Februari 9-13.Wakati tukielekea katika shamrashamra za tamasha hilo kubwa kuliko yote hapa nchini na Afrika Mashariki kwa ujumla, kuna baadhi ya mambo ambayo wasanii wetu wanatakiwa ama kupaswa kuyazingatia. Mojawapo ni kuhakikisha kuwa wanawasilisha kazi zao, ili nao waweze kushiriki kikamilifu, kwani jambo hilo sio tu kwamba litawawezesha kufikisha kazi zao kwa wapenzi na mashabiki wa burudani watakaohudhuria katika tamasha hilo kutoka ndani na nje ya nchi.Wasanii hao wanapaswa kufahamu kuwa wao ndio mabalozi wetu hivyo ni wajibu wao kuwasilisha kazi zao kwa mashabiki kutoka nje ambao watasaidia kuitangza sanaa ya Tanzania watakaporejea makwao. Pia uwepo huo wa mashabiki kutoka nje ya nchi, ni wazi kuwa utatoa fursa ya kipekee kwa wasanii wa Tanzania kuonyesha umahiri wao katika tungo, uwezo wa kuimba na hata unenguaji na ni mahali ambapo wanaweza kuutangaza na kuutambulisha utamaduni na mila za Watanzania, fursa ambayo kwa miaka mingi iliyopita ilikuwa haipatikani. Kadhalika, wasanii wetu wanapaswa kuonyesha uchangamfu, ukarimu mapenzi na dhamira ya kujifunza kutoka kwa wageni walio wasanii na hata mashabiki kwani daima kuna mengi wanaoweza kujifunza kupitia tamasha hilo. Tunasema hivi kwa kuwa tumeshuhudia mara kadhaa katika maonyesho yenu ya kawaida katika kumbi za hapa nyumbani, kila kukicha wasanii wengi wamekuwa wakituonyesha viroja na vituko vya ajabu hata wakiwa jukwaani. Hakuna haja wala ulazima wa kuvitaja viroja na vituko au mabaya yote waliyoyafanya kwa vile haitasaidia kujenga mwanzo wenye mafanikio kwa pande zote, kwao binafsi na taifa kwa ujumla. Nidhamu, kujiheshimu na kuheshimu kazi, uwajibikaji wa kweli pindi wanapokuwa jukwaani ni kati ya mambo ya msingi wanayopaswa kuwa nayo katika kipindi chote cha tamasha hilo. Zaidi ya hayo, tunalitakia kila la kheri tamasha hilo lililotokea kuvuta hisia za wengi kutokana na kujaa msisimko, lakini pia tukiamini litasaidia kuongeza kipato kwa wajasiriamali wengi wa viunga vya Zanzibar.
Mosha atangaza hali ya hatari Thursday, 03 February 2011 22:08
Mwandishi Wetu
MAKAMU mwenyekiti wa Yanga, David Mosha ametangaza hali ya tahadhari kwa viongozi na wachezaji wa klabu hiyo kufutia vitendo vya kihuni wanavyofanyiwa kwa sasa na watu wanaojiita wakereketwa wa Yanga.
Mosha ametoa kauli hiyo siku moja baada ya mashabiki wa timu hiyo kumfanyia fujo na kuvunja kioo cha nyuma cha gari yake juzi
kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam. Akizungumza na Mwananchi jana katika kituo cha polisi cha Chang'ombe, Mosha alisema hali ya usalama wa viongozi na wachezaji wa timu hiyo inazidi kuwa mbaya kutokana na vikundi
vya wanachama wa timu hiyo kufanya fujo kila mechi.
Akizungumzia aina ya kesi aliyoifungua katika kituo hicho alisema, "Mimi sijafungua kesi isipokuwa nimetoa taarifa ili serikali pamoja
na jeshi la polisi wafahamu kinachoendelea ndani ya timu,"alisema Mosha na kuongeza:
"Mimi kama Makamu Mwenyekiti siwezi kuvumilia hali hii wala siwezi kukaa kimya huku nikiona usalama wa viongozi na wachezaji ukizidi
kuzorota kutokana na vikundi vya watu wachache kwa sababu leo wanafanya fujo na kuharibu mali kesho yakitokea maafa itakuwaje
ninaiomba serikali na jeshi la polisi litizame suala hili kwa umakini zaidi."
Akitaja baadhi ya matukio yaliyowahi kutokea katika mechi za hivi karibuni alisema,"katika mechi ya Yanga na AFC ya Arusha aliyekuwa meneja wa timu hiyo Emanuel Mpangala aliondolewa uwanjani chini ya ulinzi wa polisi baada ya kunusurika kupigwa na
mashabiki.
Alisema mbali na Mpangala mchezaji wa timu hiyo Nsa Job pia alipigwa na mashabiki hao baada ya mechi ya kimataifa baina ya timu
hiyo na Dedebit ya Ethiopia.
Kuhusu watu waliovunja kioo cha gari lake alisema watu hao wanafahamika na tayari mmoja alikamatwa siku ya tukio na kuwataja wenzake pamoja na kumtaja aliyewatuma kufanya hivyo.
"Hao watu tayari wanafahamika,kwa sababu aliyekamatwa akivunja kioo cha gari langu aliwataja wenzake na kumtaja aliyewatuma
hivyo nimeamua kumsamehe kwa vile najua njaa zao ndio zilizopelekea wakafanya hivi, lakini polisi wataendelea na uchunguzi ili kubaini
sababu ya wao kutumwa na mtuhumiwa aliyetajwa,"alifafanua Mosha.
Hata hivyo RPC wa kituo hicho hakuweza kupatikana kuzungumzia suala hilo kwa madai kuwa yupo kwenye kikao nje ya ofisi.
CHAMA cha Waandishi wa Habari za Sanaa Tanzania (CAJA) na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Aprili mwaka jana walizindua jukwaa la sanaa wakiwa na lengo la kuwakutanisha wadau hao, ikiwa ni njia pekee ya kuwakutanisha. Lengo la Jukwaa hilo lilitokana na baada ya michakato ambayo ilitokana na malalamiko mengi kutoka kwa pande hizo kuhusu upashanaji habari, jambo ambalo linawapa wakati mgumu wadau hao. Waandishi wa habari walilalama kwamba wanapata wakati mgumu wa kuwapata wasanii kwa wakati unaofaa ili kubadilishana mawazo kati ya pande hizo. Mara nyingi Mwenyekiti wa Simba, Alhaj Ismail Aden Rage, hupenda kutoa kauli kwamba umuhimu kati ya waandishi wa habari na wadau wake wakiwemo wanamichezo na wanasanaa unafananishwa na kuku na Yai. Bila kujali, yai na kuku ni kipi kilichoanza lakini katika suala la maendeleo ni vitu ambavyo vinategemeana kwa sababu kila kimoja ni muhimu kwa mwenzake. Sasa kwa umuhimu huo inatakiwa wasanii hapa nchini wanatakiwa kuhudhuria katika jukwaa ambalo ndio kimbilio lao la kufikisha ujumbe kwa jamii ambayo inahitaji chakula ambacho wanacho, kazi ya sanaa. Ukiachilia mbali kufikisha ujumbe kwa jamii katika jukwaa hilo ambalo hufanyika kila Jumatatu, hukutanisha wasanii wenye elimu mbalimbali kutoka kona za Tanzania ambao wanatoa elimu murua ya tasnia hiyo ambayo inapigiwa kelele kila uchao. Cha kusikitisha zaidi watoa mada wanaowasilisha mada katika majukwaa tofauti ni wasomi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na wengine ambao si wasomi, lakini ni mguso kwa jamii ambao kwa asilimia kubwa ndio kimbilio letu katika kusaka namna ya kuendeleza tasnia ya sanaa. Wasomi hao hutoa elimu ambayo kama wasanii wanaofanya kazi za sanaa wangejitokeza ingekuwa ni mojawapo ya elimu ambayo hutolewa vyuoni, lakini walaji wenyewe ambao ni wasanii wanajificha. Hali ya wasanii kutohudhuria majukwaa ya sanaa BASATA kila Jumatatu, inaonyesha dhahiri kwamba maendeleo yanayofanywa na Serikali wakati huu ambazo inatakiwa wasanii wazifanyie kazi ambazo wanaendelea kutekeleza kelele za wasanii zilizopigwa muda mrefu. Serikali inaendelea kujenga majumba makubwa ya sanaa, mfano mmoja wapo ni jumba linalomaliziwa kujengwa zilipo ofisi za BASATA na lingine linatarajiwa kujengwa katika maeneo ya Kiromo Bagamoyo. Sasa wasanii kelele zilizokuwa zikipigwa muda mrefu inatakiwa muanze kuzifanyia kazi na kuleta changamoto miongoni mwenu kwa kuhudhuria katika majukwaa na kutoa michango yenu ambayo itasaidia na kufanikisha maendeleo ya sanaa hapa nchini. Cha kusikitisha zaidi utakuta siku nyingine kuna mada muhimu zinazotolewa katika Jukwaa la sanaa, lakini muitikio wa wadau wenyewe wa sanaa ni mdogo hadi unaogopa kwamba kwa mwendo unaofanywa na wasanii hao. Asilimia kubwa ya wenye asili ya ngozi nyeusi tuna tabia ya kutopenda kujifunza zaidi hasa ukizingatia ameshapata maendeleo, mambo mengine anayaweka pembeni badala ya kuendelea kusaka mipangilio ya kuiboresha kazi yake. Watanzania tuna kawaida ya kujikweza pindi kazi mojawapo inapofanya vizuri badala ya kuongeza ufanisi ili kuendelea kufanya vizuri zaidi, matokeo yake ile kazi moja ndiyo inakuwa mwisho wa msanii. Wenzetu walioendelea, mara zote wanajifunza zaidi, ndiyo maana wanapata nafasi ya kujifunza kazi zetu na kuzifanyia kazi ipasavyo jambo ambalo wanazidi kuchuma kazi zetu ambazo tumezibuni sisi wenyewe. Inatakiwa tuache ‘Upedeshee' ambao hautusaidii katika kusaka maendeleo ambayo tunayapigia kelele bila ya kupata ufumbuzi ambao unatakiwa wasanii wenyewe kujitambua na kusaka namna ya kufanikisha maendeleo hayo. Lakini malalamiko yanayoishia hewani bila ya kupata ufumbuzi ambao inatakiwa wasanii kutokana na nguvu waliyonayo kufanikisha maendeleo yao, badala yake wamekubali kuwa chini. BASATA ambao wanasaka namna ya kuwakomboa wasanii, Agosti mwaka jana waliazimia kuunda mashrikisho manne ambayo yatawakutanisha ili kusaka namna ya kufikia maendeleo wanayopigia kelele. Wasanii hudhurieni katika majukwaa ili mpate chakula chenu ambacho ni kupata ladha za watu tofauti ambazo ndani yake inapatikana elimu, burudani na maendeleo mengine ambayo ni muhimu kwao na jamii. Lakini tukiendelea kulaumiana bila ya kusogeleana, ufumbuzi hautapatikana hadi dunia inakwisha, tujitokeze katika majukwaa ili kuondoa wingu ambalo limetanda katika nyanja ya sanaa na burudani ambalo limedumu kwa miaka mingi na wa kuliondosha ni sisi, shime tushirikiane.
Uhaba wa mashabiki ukumbini tuwasaidieje wasanii wetu?
Khadija Kalili
TAKRIBAN miaka minne nyuma sasa ambako kumekuwa na mfumuko wa kuasisiwa bendi nyingi mpya lakini ambazo zimekuwa hazileti tija katika tasnia hii ikiwa ni uhaba wa mashabiki kwenye kumbi wanazopiga kiasi cha kupoteza hamasa ya wasanii wake vinara licha ya kuwa na majina makubwa. Mfano mzuri ni kwa msanii Ally Choki ‘Rwambow', Ramadhan Masanja ‘Banza Stone' na Mwinjuma Muumin ‘Kocha wa Dunia' na wengineo wengi ambao ni maarufu hapa nchini walioweza kuanzisha bendi zao lakini mashabiki katika maonyesho yao wamekuwa ni wa kusuasua bila ya kujua nini tatizo. Umaarufu wa wasanii hao unatokana na namna walivyo wakali na wabunifu katika tungo zao nyingi na zenye kuvuta hisia za mashabiki na wapenzi wengi wa miondoko ya muziki wa dansi nchini. Binafsi nimeshindwa kufahamu tatizo linalowaandama nyota hawa waliowahi kufahamika jina la ‘Mafahari Watatu' ikiwa na maana kuwa wao pekee ndiyo wanaotamba katika muziki wa dansi nchini. Sitaki kuamini kuwa, mfumuko wa bendi na kushuka kwa nyota zao hasa Banza na Muumini kwani kama wao ni mafahari kwanini hizo bendi zilizofumuka ghafla zisiwe chini yao. Pia sitomuunga mkono shabiki au mdau yeyote yule ambaye ataibuka na kusema kuwa eti huenda ikawa wakali hao wamechokwa, kutokana na ukongwe wao, hivyo hiyo ndiyo iwe sababu ya wao kushuka kisanii kiasi cha maonyesho yao kutojaza mashabiki kama ilivyo katika bendi nyingine. Ukweli ni kwamba Banza, Choki na Muumin hawana ukongwe wa kufikia kuwekewa mashaka ya kuwa labda wameshachokwa na mashabiki pamoja na wapenzi wa muziki wa dansi kwa ujumla. Nasema hivyo kwa sababu majina yao hayajavuma kwa zaidi ya muongo mmoja. Kwa sababu zipo bendi na waimbaji wakongwe wengi ambao wako kwenye fani kwa miaka zaidi ya 33 sasa, lakini hawajachuja hivyo kwa nini wao wachuje hivyo jamani ? Wakongwe wengi waliowatangulia kwa kila kitu, ambao wapo kwenye gemu hadi leo na wanapopanda jukwaani, mashabiki huomba wasishuke ambao kama vile wale wa bendi za The Kilimanjaro, Msondo, Sikinde. Hapo ndipo ninapojiuliza nini tatizo kwa Muumin, Choki na Banza ili kama wadau na mashabiki wao watakuwa wanalijua tatizo basi wajitokeze kuwasaidia wasimame kama walivyokuwa zamani. Hivi sasa wanapopiga kwenye kumbi hali ni tete sana hata kwenye kumbi wanazotumbuiza ambako mara kwa mara maonyesho yao yanahudhuriwa na mashabiki wachache sana hivi chanzo hasa ni nini! Hata hivyo, binafsi nachukua fursa hii kuwashauri wasikate tamaa kwa sababu muziki ni sawa na bidhaa ambayo hutegemea msimu huenda hali ikageuka kulingana na wakati husika. Kadhalika nawapa pongezi kwa kutokata tamaa na kuendeleza gurudumu la kutoa burudani na kufanya ziara katika mikoa mbalimbali licha ya kupata mashabiki wachache ipo siku nao watakula neema na kufurahia matunda ya kazi zao kama ilivyo kwa wasanii wengine. Kama hiyo haitoshi nawasihi msikate tamaa kwani mkiwa na inani ipo siku mtarudi tena katika chati na kuwa kama mlivyokuwa miaka sita au mitano nyuma. Bila kuficha kitu, wasanii hawa walikuwa juu na kufanikiwa kutingisha medani ya muziki hasa kutokana na tungo zao pamoja na nakshi zilizokuwa zikipatikana katika vibao vyao hata vile walivyoshirikishwa tu ambavyo vimetungwa na wasanii wengine. Yaani hivi sasa hata kama serikali itapiga marufuku nyimbo za bendi nyingine zote na kuziacha za nguli hawa pekee bado mashabiki wa muziki wa dansi watakavyopata raha. Nasema hivyo kwa sababu ikiwa wewe ni shabiki wa miondoko ya muziki wa dansi, huwezi kubaki kitini au kukaa bila kutikisa kichwa pale kibao cha mmoja wao kitakapopigwa. Ushahidi katika jambo hili ni vibao kama ‘Kiu ya Mapenzi', Tunda Special', ‘Mgumba', ‘Kilio cha Yatima', ‘Ugumu wa Maisha' na ‘Nyumba ya Urithi' vyote vya Muumin. Ama vile vya Banza Stone kama ‘Aungurumapo Simba', ‘Mtaji wa Maskini', ‘Elimu ya Mjinga', ‘Euro 2000', ‘Mtu Pesa', ‘Hujafa Hujasifiwa' na ‘Mimi Niseme'. Au za rafiki yangu Choki zikiwamo ‘Jirani', ‘Chuki Binafsi', ‘Busu la Kufunga na Kufungua Mwaka', ‘Password', ‘Umbea Hauna Posho', ‘Mtaa wa Kwanza' na ‘Mjini Mipango'. Hawa niliowataja hapa ni baadhi ya wanamuziki ambao kwa hakika kujikusanyia kwao mashabiki kulitokana na juhudi zao za dhati za kuhakikisha wanawaandalia kitu roho yao inapenda. Ila cha kushangaza, licha ya kuendelea kufanya mambo ya uhakika, katika siku za hivi karibuni wanamuziki hao wameonekana kupoteza makali yao kwa wapenzi na mashabiki. Wote watatu wangali wapo katika makundi yanayorindimisha muziki, ambako Banza Stone yuko katika bendi ya Rufita Connection. Hali kadhalika, Choki yuko katika bendi yake ya Extra Bongo huku Muumin akiwa analiongoza jahazi la Bwagamoyo Sound International ‘Wana Gusa Unase'. Wote huko waliko bado wanapakua vibao ambavyo kwakweli ukitulia na kuvisikiliza kwa makini, huwezi kukwepa kumshukuru Mungu kwa kuwashusha nguli hawa wa muziki nchini Tanzania. Kwa leo naomba nikunje busati langu huku nikiwatakia wote wikiendi njema.