Nairobi, Kenya. Mwanaharakati mashuhuri wa muungano wa National Super Alliance (Nasa) aliyefukuzwa hivi karibuni Miguna Miguna anasema inafanyika mipango ya kurudi Kenya na kwamba suala la muda tu kabla ya kukanyaga mguu wake nchini.
Miguna aliliambia gazeti la Nation katika mahojiano maalum kutoka Canada kwamba tayari amewaagiza wanasheria wake kupeleka mahakamani ombi la kuitaka mahakama iamuru amri ya serikali itenguliwe na arejeshewe hati yake ya kusafiria.
Miguna anashutumiwa kwa kushiriki katika mkutano haramu wa "kumwapisha" kiongozi wa Nasa Raila Odinga kuwa "rais wa watu" katika bustani ya Uhuru Park Januari 30.
Mwanasheria huyo machachari alisema kuwa hakuna chochote kitakachomzuia kurudi nyumbani kwa kuwa ni raia halali wa Kenya na Katiba iko wazi juu ya utaifa wake.
"Najua mke wangu hatafurahi kusikia hilo lakini baadhi ya vitu hivi unapaswa kuamua jinsi unavyotaka kuishi maisha yako na urithi unaotaka kuacha nyuma.
"Hivi tunavyozungumza, tayari wanasheria wangu wameshawasilisha maombi leo katika mahakama kuu wakitaka uamuzi wa kupokonywa uraia wangu ufutwe.
"Ujumbe wangu kwa Uhuru Kenyatta na William Ruto ni huu, "Kenya si mali yenu nitarudi. Samahani!" alisema.
Serikali inadai kwamba alipoteza uraia baada ya kupata pasipoti ya Canada mwaka 1988 baada ya maombi yake kupewa hati ya Kenya kukataliwa Septemba 1987, muda mfupi baada ya kufukuzwa kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi.
Hata hivyo, alikanusha madai kwamba aliukana uraia wa Kenya, akisema uraia wake wa kuzaliwa ni haki isiyoweza kupokonywa.
"Hakuna mtu anayeweza kubatilisha uraia wa Mkenya aliyezaliwa nchini Kenya. Uraia pekee ambao mtu anaweza kupoteza hata akiwa Kenya ni ule wa kuasili. Kwa hali yoyote, sihitaji idhini ya mtu yeyote kurudi nchini kwangu, "alisema.
Habari kwa hisani ya gazeti la mwananchi