Herbalist Dr MziziMkavu
JF-Expert Member
- Feb 3, 2009
- 42,872
- 34,363
Maoni ya Katuni.
Juzi wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, walipandwa na hasira baada ya kuelezwa kwamba baadhi ya hoteli za kitalii zilizobinafsishwa hazilipi tozo mbalimbali ikiwamo ya utalii kwa miaka 10 sasa.
Pia ilbainika kwamba mikataba hiyo haijaweka bayana ukomo wake na inataka iwapo mgogoro utatokea baina ya serikali na mwekezaji, usuluhishi ukafanyike London katika Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa migogoro.
Wajumbe walisema kumekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa wafanyakazi, utendaji na uwekezaji duni wa mwekezaji ambaye ni kampuni ya Hotels & Lodges Limited inayomiliki hoteli kadhaa katika hifadhi ya Ngorongoro, Serengeti na Manyara.
Kwamba, inasikitisha kuona kuwa mikataba ikimpendelea zaidi mwekezaji huku ikiinyonya nchi bila kuwa na kikomo.
Walihoji ukomo wa mikataba hiyo na pia sababu za Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa) kutoruhusiwa kununua hoteli hizo wakati shirika hilo lina uwezo wa kuziendesha.
Mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo alisema taarifa ya Kampuni ya Mashirika Hodhi ya Umma (CHC), inaonyesha kwamba mikataba hiyo ni mibovu na hasa suala la kufanya usuluhishi nje ya nchi wakati Tanzania ina mahakama ikiwamo ya biashara.
Awali, Mwenyekiti wa Bodi ya CHC, Dk. Marcellina Chijoriga, alikiri kwamba mikataba ya kubinafsisha baadhi ya hoteli na mashirika ya umma ilikuwa mibovu na kwamba ni eneo ambalo serikali imejifunza.
Kuhusu kampuni ya Hotels & Lodges Limited ambayo ilimilikishwa hoteli za Lake Manyara, Lobo, Seronera na Ngorongoro, alisema aliuziwa kwa maelekezo ya Baraza la Mawaziri baada ya tathmini kufanyika.
Alisema kabla ya kuuzwa kwa hoteli hizo, serikali ilifanya tathmini na kujiridhisha kwamba zilikuwa na thamani ya Dola za Marekani milioni 15, lakini mwekezaji huyo aliuziwa kwa Dola za Marekani milioni 13.6.
Alisema kutokana na uamuzi huo, kampuni ya Hotels & Lodges, iliuziwa hoteli ya Lake Manyara kwa bei ya kutupa ya Dola za Marekani milioni 1.7 badala ya thamani yake halisi ambayo ilikuwa Dola milioni 3.8.
Alisema mwekezaji huyo alitakiwa kuwekeza Dola za Marekani milioni 3.2, lakini makubaliano hayo hayajafikiwa.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, alisema mikataba hiyo ni mibovu na kwamba inamnufaisha zaidi mwekezaji.
Alisema mwekezaji alikabidhiwa hoteli hizo mwaka 2003 na kutakiwa kuzikarabati na kuzifanya ziwe na hadhi ya kimataifa, lakini hadi sasa hajakamilisha makubaliano hayo.
Alisema mwekezaji huyo ameonekana ni mwenye kiburi na ambaye hataki kuhudhuria vikao halali na kwamba kwenda kusuluhisha mgogoro London siyo sahihi.
Kamati ya Bunge imeagiza mikataba hiyo ipitiwe na kuainisha vipengele vitakavyofanyiwa marekebisho kwa manufaa ya umma.
Hali hii inaonyesha wazi kwamba kuna tatizo kubwa katika usimamizi wa hoteli zilizobinafsishwa kwa wawekezaji wa nje.
Inashangaza kuona hata viongozi wa serikali wenye mamlaka ya kusimamia sekta hiyo kama Mwenyekiti wa CHC na Waziri Kagasheki, wanamlalamikia mwekezaji kwa kukiuka mkataba bila kuchukua hatua!
Kinachoonekana hapa ni kwamba mwekezaji huyo anakuwa na kiburi kwa kufahamu kuwa mikataba ya ubinafsishaji wa hoteli ilikuwa mibovu na inamnufaisha yeye.
Mikataba mibovu imeendelea kuitafuna nchi yetu kutokana na kila uchao wataalam wetu wa sheria kusaini mikataba ambayo baadaye inaipotezea nchi mabilioni ya fedha. Tunayo mifano mingi ya mikataba ya aina hiyo ambayo hatuwezi kuitaja yote hapa, lakini kwa kutaja michache ni Richmond, Dowans na IPTL.
Huko nyuma kuna baadhi ya viongozi wa serikali waliosema kuwa tunaingia katika mikataba mibovu kutokana na wataalam wetu kutokuwa na ujuzi katika mikataba.
Kauli hizo hazina ukweli kwa kuwa nchi yetu inao wasomi wengi waliobobea katika sheria. Tatizo lililoko ni kukosekana kwa uadilifu miongoni mwa watumishi wa umma ambao wanatanguliza mbele maslahi yao binafsi.
Kwa mfano, inakuwaje serikali inasaini mkataba na mwekezaji na kukubali kuwa kama litatokea tatizo usuluhishi ufanyike London katika Mahakama ya Usuluhishi wa migogoro wakati tunazo mahakama zetu nchini?
Kwa ujumla, mikataba hii ya ubinafsishaji hoteli imejaa utata mkubwa na tunakubaliana na Kamati ya Bunge kwamba ipitiwe upya ili nchi inufaike.
CHANZO: NIPASHE