JamiiTalks
JF Advocacy Team
- Aug 7, 2018
- 685
- 1,124
Swala la mimba za utotoni limekuwa ni jambo lenye utata kwenye jamii nyingi ndani nanje ya Afrika. Utafiti wa shirika la afya duniani (WHO) unaonyesha kwamba wasichana milioni 16 wenye umri kati ya miaka 15 hadi 19, na wasichana milioni 1 wenye umri wa chini ya miaka 15 huwa wahanga wa mimba za utotoni kila mwaka.
Asilimia kubwa ya wasichana hawa inatoka kwenye jamii zenye uchumi wa chini. Kutokana na kutotarajiwa kwa mimba hizi, wasichana milioni 3 hutoa mimba katika mazingira hatarishi kila mwaka. Tatizo la mimba utotoni linaenda sambamba na uwepo wa asilimia kubwa ya ndoa za utotoni.
Ni muhimu kufahamu kwamba; hili si janga la nchi masikini peke yake. Ile dhana ya „bora kuwa mbwa ulaya kuliko kuwa mwana wa nchi“ haina makali katika swala la mimba katika umri mdogo. Tatizo hili lipo pia kwenye nchi kubwa kiuchumi kama Marekani. Mwaka 2015, zaidi ya watoto laki mbili walizaliwa na mabinti wenye umri mdogo nchini humo. Wakati huohuo, mabinti wanne kati ya 10 waliathiriwa na tatizo hili.
Nchini kwetu Tanzania, utafiti wa demografia na afya wa mwaka 2016 unaonyesha kwamba; watoto 36 kati ya 100 wanaolewa kabla ya kufikisha miaka 18, wakati watoto 27 kati ya 100 wanapata ujauzito kabla ya kufikisha miaka 18. Takwimu hizi zinaonyesha kwamba tatizo hili si dogo kwani linamgusa mtoto wa kike ulimwenguni kote na hivyo linahitaji kuzungumziwa.
Mimba za utotoni ni nini?
Mimba za utotoni ni pale binti au kigori anapopata mimba kabla ya kutimiza miaka 18.Wataalamu wa afya ya uzazi wanashauri ili kuepukana na matatizo ya kiafya ni vyema kupata mimba baada ya kufikisha umri wa miaka 18. Inatajwa kwamba, chini ya miaka 18 wasichana bado hawajakomaa kiakili na kimwili. Nyonga zao huwa changa na nyembamba hivyo kutoweza kustahimili kubeba kiumbe.
Wembamba huu wa nyonga unaweza pia kumkwamisha mtoto katika njia ya uzazi wakati wa kujifungua. Hii inaweza kupelekea kifo cha mtoto anayezaliwa kutokana na kukosa hewa. Pia, mimba za utotoni zinaweza kuleta madhara ya kiafya kama fistula (kutokwa na haja ndogo na kubwa bila ya kuweza kujizuia), Kutokwa na damu nyingi wakati wa kujifungua, Kupata maambukizi ya bakteria katika njia ya uzazi, kifafa cha mimba na athari za kisaikolojia
Visababishi na vichocheo vya mimba za utotoni
Sababu zinazotajwa kuchangia kuwepo kwa tatizo la mimba za utotoni zinatofautiana kulingana na mazingira. Lakini zipo pia sababu ambazo zinaendana kimataifa.- Mawasiliano hafifu wakati wa balehe
Siku hizi balehe inaanza mapema sana. Kati ya miaka 9 hadi 12 wasichana wanaanza kupevuka. Wakati wa balehe mwili huzalisha homoni nyingi zaidi zinazosababisha mabadiliko ya kimwili. Homoni hizi huleta pia mabadiliko ya hisia ya mara kwa mara; kuwa na furaha, huzuni na hasira. Pamoja na mabadiliko mengine ya mwili, maumivu makali wakati wa hedhi na kupanda na kushuka kwa hisia husababisha kuchanganyikiwa kwa wasichana. Hali hii hupelekea wale wanaobalehe kujiuliza maswali mengi na kupatwa na wasiwasi jinsi wanavyoonekana kwa watu wengine. Na hivyo kuwafanya wapatwe na msongo wa mawazo.
- Shinikizo rika (Peer pressure)
Vyombo vya habari na internet pamoja na kuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya jamii pia vimekuja na changamoto ya mashinikizo ya tabia hatarishi kwa vijana. Upana na uhuru wa internet unampa fursa kijana kufuatilia mambo ambayo ni mwiko kwenye jamii yake.
Na kutokana na kukosa mwongozo juu ya mambo hayo, kuna hatari kubwa ya kushawishika kuiga baadhi ya mambo bila ya kuyaelewa. Hali hii inaweza kupelekea matumizi mabaya ya internet; kama kuangalia ponografia na kurusha picha za utupu mtandaoni. Hizi ni njia zinazowafanya mabinti pia kushawishiwa kimapenzi na watu waliowazidi umri.
- Kutotuwepo kwa elimu ya afya ya uzazi
Hata hivyo mada ya “reproduction” inayotajwa kama sehemu ya elimu ya uzazi hufundishwa kidato cha tatu katika shule ya sekondari. Hiki ni kipindi ambacho mabinti wengi huwa wameshaathiriwa na mimba za utotoni. Vilevile mada hii pekee haikidhi mahitaji ya elimu ya uzazi na jinsia.
- Ukatili wa kijinsia
Wazazi wengi huridhia kufanya makubaliano nje ya mahakama kwani baadhi ya wahalifu ni ndugu wa familia au ukoo. Hivyo wengi huridhia kumuozesha binti yao au kulipa adhabu fulani nje ya mahakama.
- Umasikini
Huu ni uhalisia unaoumiza sana ukiufikiria kwa makini. Katika mazingira haya: mzazi yuko tayari kumuozesha binti yake mapema kwa kuogopa kwamba atapata mimba kabla ya kuolewa na kumkosesha pesa ya mahari. Na wakati mwingine, mabinti huozeshwa ili mahari yao itumike kwa minajili ya kumsomesha mtoto wa kiume.
Katika maeneo ya vijijini, si nadra kuona msichana ananyimwa haki ya elimu na kulazimishwa kuolewa. Haya ni matokeo ya imani potufu kuwa mtoto wa kike hawezi kuisaidia familia yake kama mtoto wa kiume. Ni wazi kwamba elimu inahitajika ili jamii ielewe umuhimu wa elimu na madhara ya kumuozesha binti kabla ya kufikisha umri unaofaa.
Upvote
0