SoC03 Mimi na mama tutaizuru dunia kuinusuru Tanzania

SoC03 Mimi na mama tutaizuru dunia kuinusuru Tanzania

Stories of Change - 2023 Competition

Hamadi Hamisi

New Member
Joined
Aug 6, 2021
Posts
3
Reaction score
2
Mtembea bure si sawa na mkaa bure, kutembea nako ni kusoma na lengo la kusoma ni kupata maarifa,ujuzi,mbinu na mikakati kubadili hasi kuwa chanya. Nami nimeaandaa safari hii tukasome yote yaliyo mazuri ulimwenguni ikisha turudi majumbani tukiwa wapya wa fikra na kubadili mitazamo yetu kwa kesho iliyo bora kwetu na vizazi vijavyo.

Naamini itakua safari mzuri na sote tutafuarahia. Msione wivu mimi ndio nitapanga wapi twende na wapi tusiende na nitawaambia kwanini. Vilevile kuna maeneo haitotulazimu wote katika sisi tuwepo nitakuwa na Mama pamoja na kaka zetu hawa watatuletea mageuzi kwa watakayo yaona.

Kituo chetu cha kwanza Mama ni jijini Tokyo nchini Japani, hiki kituo ni muhimu sana kwa wote kufika bila ya udhuru, najua wote hatuwezi kutosha kwenye ndege zetu za ATCL ila wengine tuko radhi kupiga makasia hadi mboni za macho yetu zishuhudie milango ya jiji hili. Kwenye ardhi hii ndugu zangu kuna zaidi ya utajiri ambao lau kila mtu akiupata Tanzania yetu ya leo itakuwa tofauti kwa muda mfupi sana, ndio ni utajiri walio nao wajapani juu ya kuchunga wakati, uwajibikaji, uwazi na ukweli, ukarimu,kupendana na kuhurumiana kiasi ambacho kama utaangusha mfuko wenye punje za mtama na zikamwagika utasaidiwa kuokota hadi pale zote zitakapoisha na ukarejea kwenye amani.

Na zaidi wajapani ni makaroshi yani wako tayari kufa kwa kufanya kazi kwa bidii weledi na umakini mkubwa hawa ndio wajapani na ndivyo walivyofunzwa na kwasababu hizo kuwa miongoni mwa taifa lenye nguvu kazi ghali ulimwengu na kuzalisha bidhaa madhubuti tena wanazozipenda watu. Tunapotaka maendeleo ghali hatuna budi wenyewe kuwa ghali na adimu ulimwenguni, watanzania wote kwa ujumla wetu tuyaishi maisha ya wezetu hawa.

Mama tuelekee Pyongyang kwa Kaka Kiduku kuna jambo la kuchukua pale ila yale mengine muachie mwenyewe. Mwambie akuambie kwanini hana muhali na usimamizi wa maslahi na hadhi ya Taifa lake, najua atakusimulia ya Mjomba Putin ila mwambie hayo huyawezi kwa sasa chukua hilo moja tu ikisha turudi nalo hapa ili wakome wale wabadhirifu wa mali za umma, wakae pembeni wale wala rushwa na wakwamishaji wa maendeleo yetu.

Mama tusiache kupita pale Uchina kwa Anko Xi naye atupe machache namna alivyoweza kukuza kilimo kwa kumwaga mabilioni ya shilingi na nguvu kazi, atuambie vipi ameweza kukuza uchumi wake na kuwa tishio kwa waliokuwa watawala wake. Mama tukitoka kwa Anko Xi mabonde yetu yenye rutba yajue kuwa yako sehemu salama na wale vijana wanaomaliza pale Usuani ukiwakusanya na wale wakulima kule Kasulu na wote wanaotaka kilimo wajione wamechagua sehemu sahihi.

Mama tumchukue Kaka Masauni na Kaka Bashungwa hadi pale herufi mbili U.K waje wavieleze vikosi vya ulinzi na usalama kuwa raia ndio rasilimali ya kwanza inayotakiwa kulindwa na kuhakikishwa haitoweki wala kudhurika chini ya mikono yao. Wawaambie ni bora izame tani moja ya dhahabu raia zuke tena asibaguliwe kwa rangi yake au asili ya udongo wake.

Mama twende uzunguni tukaone kwanini wana mifumo bora ya elimu inayowapa wahitimu wake kuishi kile walichosoma na si kuanza kujitafuta kama wajasiriamali wetu wanaojiita mahaso, mama kule uhindini kwao Shahrukh Khan kwanini sanaa yao ya uigizaji iko juu sana kiasi cha Akshay kukamata eropleni kwa mkono wake mmoja Mama kwanini hawa wahindi wanasifiwa kufanikiwa kwenye afya au ni vile walivyoajiri sana na kuwekeza huko.

Ila nimekumbuka chenchi anazo Kaka Mwigulu za kufanya yote hayo yawe bora. Mama twende na kaka Mwigulu hadi pale uhispania ya weusi hawa waliomtwanga mnyama kwenye robo fainali kule kwenye ubingwa watueleze na Kaka mwigulu ahifadhi atakachosikia mana hachelewi kufanya biashara zake za kwenye buku wakati uhalisia wa wamiliki magoli pale KO wanalia nyau mitaji inaangamia, watuambie wamewezaje kuinua uchumi kwa kodi ndogo na rafiki kwa watu wao, kwanini wameweza kuboresha mazingira kwa uwekezaji huku wakizisaidia sekta binafsi kuchuana na kuongeza ushindani wa soko la ndani hali inayoleya ahueni ya maisha kwa watu wao. Lakini watueleze pia kwanini shilingi yao inayoingia wanaidhibiti na kila mwanafamilia anaifaidi.

Mama kuna hizi kelele za DP Ulimwengu twende hadi pale Abudhabi, nitavaa kile kiremba cha kahawia na kanzu yangu nyeupe Maprof tusiwaache nyuma, Sheikh atueleze namna bora walizozitumia kuibadilisha Dubai kutoka jangwa hadi kuwa kitovu kikubwa cha biashara ulimwenguni. Watuambie na sisi tufanye vipi tukusanye mapesa mengi na ndani ya miaka kumi tu Tulibadishe pori la kigoma kuwa kama Accra Ghana. Mama ila kwa ilivyo Dubai naomba uniache kwanza nile bata napia nifurahie namna familia zilivyopewa kipaumbele, hapa ndio kuna maana halisi ya mume, mke, mtoto, baba, mama, babu na bibi hakika wamefanikiwa hapa na huu ndo mwanzo wa kuipata jamii bora kwani familia zao ni bora pia.

Mama tupite kule Sirte Libya yalikokuwa makazi ya Babu Gadafi dikteta aliyeshibisha raia wake hadi wakasaza, naamini tutapata kurasa chache za kitabu alichowaandikia watu wake kwa karibu nusu karne, hasa yale maneno yake yakishujaa aliyoysema kwenye ile hotuba yake aliyokua akihesabu masaa ya pumzi zake, namnukuu "..Wakati wengine walipokuwa wanajenga majumba makubwa na kifahari mimi niliishi kwenye nyumba ya kawaida na kwenye mahema. Siwezi kusahau maisha yangu ya utoto kule Sirte. Sikutapanya rasilimali za nchi yangu,... nilichukua kidogo kwa ajili yangu na sehemu kubwa niliwapa wananchi." Mwisho wa kunukuu.(Chanzo: Ukurasa wa Tujuze Facebook). Mama usia na mwisho wa Babu ni ponyo na indhari kwetu.

Mama tutafanya vibaya ikiwa hatutokwenda Burkinafaso kwenye Kaburi la Kapteni Sankara, mwana mageuzi wa kweli aliebadilisha maisha ya Yako kwa pumzi chache alizojaaliwa madarakani. Hakupenda makuu wala kujitweza kwa maslahi binafsi bali alitamani kila raia wake aone ladha ya uwepo wake ulimwenguni.

Mama nilitaka tupite Zaire kwa babu Mobutu ila nakhofu unaweza kuvaa ile kofia yake yenye vumbi, mama ile kofia haikufai kwanza ni ndogo sana na haina nuru ya kuliangaza taifa letu tukufu,si unamkumbuka Babu alivyotumia bakora yake kufanya watu wake wanyonge na waone ardhi yao ni ya moto mithli ya shaba na chungu kuliko shubiri kisha akawatweza wale weupe waliompa mrija wa kunywea pumzi za watu wake, Mama huku mie sitaki twende.

Mliokuwa hamuitaki safari naona mnatabasamu naamini tumevipenda vituo vya safari yetu. Mama hawezi kukwamisha tutakwenda huko na Mabro watatuhurumia pia. Tunalipenda taifa letu mazuri ya wezentu tuyafanyie kazi na mabaya tuwaachie na yale yetu bora tuyaendeleze. Udhibiti wa rasilimali zetu kiwe kipaumbele kwani ndio msingi wa maisha ya Tanzania ijayo na kizazi chake na hayo yoye ni katika kukumbushana namna wezetu walivyotumia utawala bora na uwajibikaji kufanya mageuzi wanayofurahia leo ndio mana nasema MIMI NA MAMA TUTAIZURU DUNIA KUINUSURU TANZANIA.
 
Upvote 1
Back
Top Bottom