SoC02 Mimi na Mazingira

SoC02 Mimi na Mazingira

Stories of Change - 2022 Competition

MSABAHA RAYMOND

New Member
Joined
Aug 15, 2022
Posts
1
Reaction score
0
Mwandishi: RAYMOND NOEL Namba za simu: 0758659963

Asubuhi moja yenye baridi ilinikuta kwenye bonde dogo karibu na mtaa wetu, nilifika katika bonde hilo kwa lengo la kuchota maji katika chemchem maarufu inayopatikana hapo ambayo hutiririsha maji katika bonde kwa mwaka mzima, chemchem hiyo huwa ni mkombozi wa tatizo la maji linapotokea katika mtaa wetu.

Haikuwa mara yangu ya Kwanza au ya pili kufika hapo, kwa sababu nimeashafika eneo hilo mara nyingi tangu nikiwa mdogo, japokuwa sasa ilikuwa yapata miaka 7 toka nifike hapo kwa mara ya mwisho.

Kiufupi nilifurahi kufika hapo kwa mara nyingine tena. Nilianza kuchota maji safi na baridi katika chemchem ile, huku macho yangu yakipepesa huku na huko kushuhudia uzuri wa mazingira asili katika bonde hilo na pembeni ya chemchem, lakini nilishtushwa sana nilipobaini mabadiliko kadhaa katika bonde hili zuri; miti mingi mirefu na mizuri iliyounda msitu mdogo mahali hapa niliyokuwa nikiiona mara kadhaa kila nilipofika hapo ilikuwa imepungua kwa kiasi kikubwa sana na ilibaki michache tu, uoto katika bonde ulipungua mno huku makazi ya watu pamoja na mashamba yakichukua sehemu yake, hata maji katika chemchem ile hayakuwa mengi na yalitiririka kwa kasi ndogo mno tofauti na ilivyokuwa mara ya mwisho nilipofika hapa kabla ya leo. Pia, nilibaini kuwa ngedere waliokuwa wakipatikana hapa tuliofurahi kuwaona pindi tulipokuwa wadogo hawakuepo tena mahali hapa.

Nilisikitishwa sana na mabadiliko haya, hamu ya kufurahia bonde lile iliisha ghafla. Nilianza safari ya kurudi nyumbani kinyonge baada ya kumaliza kuchota maji, kichwani mwangu nikiwa ninajiuliza maswali mengi; Je, kwa nini binadamu tunaharibu mazingira vibaya kiasi hiki? Hatujui umuhimu wake? Mamlaka hisika hazibaini uharibifu huu? Au labda idadi ya watu imekuwa kubwa sana hivyo kuwa na mahitaji makubwa ya ardhi?. Nafikiri, swali langu la mwisho lilikuwa ni jibu la swali langu mojawapo kama sio yote kwa namna moja ama nyingine.

Nilipofika nyumbani, nikakaa chini kuendelea kutafakari kuhusu mabadiliko katika bonde lile, na hapo nikaazimia kwamba nitajitolea kwa namna yeyote kulitunza bonde lile na ikiwezekana kulifanya liwe na hali yake kama zamani na nitajitahidi kuelimisha watu kuhusu umuhimu wa kutunza mazingira katika bonde hilo.
Hivi sasa, nimeanza kukuza miti michache kwa lengo la kuipanda katika bonde ili kulirudishia uhalisia na uzuri wake. Pia nilifurahishwa sana siku moja pindi niliposikia tangazo redioni lililowataka wananchi kutunza mazingira yote yanayowazunguka na hasa katika eneo la bonde lile ambalo miti ilikuwa imebaki michache sana.

Hapa nikagundua kuwa katika "mapambano" haya siko peke yangu na nilifurahishwa zaidi kuona mamlaka husika zimeguswa na jambo hili. Natumaini siku moja bonde hili litarudia uzuri wake wa zamani na kurudisha mandhari ile pendwa ya " utotoni" kama watu wote watashorikiana katika kutunza mazingira haya.
TUYATUNZE NA KUYAPENDA MAZINGIRA YETU.
 
Upvote 0
Back
Top Bottom