SoC02 Mimi ni nani?

SoC02 Mimi ni nani?

Stories of Change - 2022 Competition

Captain Donor

Member
Joined
Jul 24, 2022
Posts
13
Reaction score
19
Hatimaye!, usiku wa deni haukawii kukucha. Ujumbe kutoka kwa Raisi wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kumsihi kila mtazania mwenye simu ya mkononi kushiriki sensa kikamilifu umenifikia. Nipo tayari kuhesabiwa.

Lakini wakati nikiwa namsubiri karani wa sensa atakayepita kwenye kaya niliyoamkia leo, fikra zangu zinakijita katika swali mimi ni nani? Nikiwa naendelea kujiuliza swali hili kwanza kabisa napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia pumzi mpaka wakati huu na kwa kunichagua kuwa ni miongoni mwa watu na raia wa taifa hili. Ni ukweli usiopingika kwamba watanzania tumebarikiwa na Mungu mengi yaliyo mazuri.

Swali mimi ni nani ndio msingi muhimu wa stadi zote za maisha; stadi kwaajili ya kujitambua, stadi za kifikra kwaajili ya kufikiri na stadi kwaajili ya mahusiano. Tunapozungumzia stadi za maisha tunakusudia ule ujuzi au maarifa yanayomsaidia mtu kuishi vizuri katika mazingira yake yanayomzunguka.

Ni wachache miongoni mwa wengi tuliobahatika kusoma somo la stadi za kazi kwa vitendo tulipokuwa shule ya msingi. Walau tuliambua machache katika mengi kwa kujifunza stadi za maisha kwani kupitia somo la stadi za kazi ilitujengea ukaribu na maelewano zaidi mimi na wanafunzi wenzangu ambao hata baada ya miaka takribani kumi na nne baada ya kuhitimu darasa la saba bado tunawasiliana, hilo limewezekana kutokana na kujengewa na walimu wetu stadi ya kimahusiano baina yetu.

Swali mimi ni nani hutuwezesha kuianza safari ya kujitambua, swali hili ni chachu na hatua ya mwanzo kuanza kubaini sisi ni wakina nani kama wanadamu na kipi tunapaswa tufanye maishani.

Si hivyo tu bali kujitambua kunamuwezesha mtu kujua ni lipi lengo lake kuu la maisha, kutimiza wajibu wake wa kila siku pamoja na kukubaliana na majukumu anayokabiliwa nayo kwenye familia, jamii inayowazunguka na taifa kwa ujumla.

Ninapozungumzia kukubaliana na majukumu nakusudia mtu kuchukua dhima ya kuondosha matatizo au shari dhidi yake ama jamii yake kwa kutafuta suluhisho bora iwe ni kwa kubadilika binafsi ili kuondokana na lawama au shutuma dhidi yake au kwa kufanya mabadiliko ili kuyaondosha matatizo na kero fulani katika jamii yake.

Swali mimi ni nani lina mchango mkubwa kwa kila mmoja wetu pindi atapolijibu vizuri, kwani kwa kufanya hivyo utakuwa ni mfano mzuri wa kuigwa kutokana na matokeo baada ya kujiuliza swali hili kwa mtu binafsi na jamii inayomzunguka. Ni dhahiri kuwa mtu akiweza kulijibu swali hili vizuri basi ataitunza afya yake vizuri kwaajili ya ustawi wake binafsi wa kiakili, kiroho, kisaikolojia na kimahusiano na atajitahidi kutoshiriki kwa namna yoyote ile kuiangamiza nafsi yake yeye mwenyewe kwa kujiingiza kwenye shughuli zisizo halali na kwa kutokufanya yale yote ambayo hayamfalii chochote katika maisha yake.

Matumizi ya vitu kama bangi na mfano wake siyo suluhisho la kuyasahau au kuyakimbia matatizo bali ndiyo chanzo cha kuyazidisha na kuharibikiwa zaidi na kupelekea kuongezeka kwa watu tegemzi na mizigo kwa jamii zao jambo ambalo ni hasara kwa taifa kwa kupoteza nguvu kazi.

Swali mimi ni nani linatukumbusha kila mmoja wetu kuwa na mshikamano na wengine katika kupambana dhidi ya adui; umasikini, ujinga na maradhi. Ni wajibu wa kila Mtanzania kumpiga vita adui umasikini kwani ni kikwazo kikubwa cha haki, wengi wamenyang'anywa haki zao kutokana na umasikini, lakini pia tumpige vita vikali adui ujinga kwani ni wengi wamepoteza maisha kutokana na adui huyu akishirikiana na adui maradhi na wengine wamepoteza viungo vyao kwa kukosa uwajibikaji na kumuendekeza adui ujinga. Tuna kila sababu ya kujifunga mkanda wa uwajibikaji leo zaidi ya ilivyokuwa jana ili kuwashinda maadui hawa.

Hitimisho
Ni dhahiri kuwa unajua wewe ni nani, unafahamu jina lako la kwanza na la mwisho, unajua ni wapi umezaliwa na tarehe yako ya kuzaliwa na pengine unaweza kuzitaja tarakimu zote za kitambulisho chako cha uraia kwa kichwa.

Lakini hayo pekee hayatoi picha kamili unapojiuliza mimi ni nani. Kuna mengi zaidi ya jina lako, vitambulisho vyako na chimbuko au asili ya kule utakapo. Ni fikra zako, imani na misimamo yako, ndoto na malengo yako, historia yako ya kipekee na jumla ya uzoefu wote uliopitia maishani ndio vinatoa picha kamili ya wewe ni nani.

Mimi ni kijana wa kitanzania, ninajitambua na nina ndoto maishani mwangu. Nipo tayari kuwa wakala wa mabadiliko chanya kwenye familia yangu, jamii inayonizunguka na kuwa balozi mzuri wa maendeleo na mazuri yote ya nchi yangu Tanzania.
 
Upvote 0
Back
Top Bottom