SoC04 Minong'ono ya uzalendo Nafsini Mwangu

SoC04 Minong'ono ya uzalendo Nafsini Mwangu

Tanzania Tuitakayo competition threads

Un tel homme

New Member
Joined
Jul 28, 2022
Posts
1
Reaction score
1

Kama ilivyo kwa vijana wengi, tuna hulka kuu ya kwenda kusoma nje ya nchi zetu, hasa kwa sababu ya scholarship au sponsorship ambapo japokuwa unasoma inakuwa ni sehemu ya kujiingizia kipato kwa namna fulani, kitaalamu tunasema unaua ndege wawili kwa jiwe moja yaani kupata elimu (vyeti) na mpunga juu.

Sasa bwana, nikiwa shule fulani huko kwa waluguru na wapogoro, kama mwalimu wa masomo ya lugha. Baada ya kuona maslahi si rafiki kwa maendeleo yangu, hasa ukizingatia sisi vijana tuna uchu wa kufanikiwa mapema ilhali muda upo mbio sana. Niliamua kutafuta scholarship. Wakenya wanasema Mungu si Kamau, mkeka ukatiki mwezi wa pili mwaka 2023, nikapangiwa kuenda kusomea masuala ya lugha na mawasiliano nchi fulani ya afrika ya kati huko. Ilikuwa jumanne jioni nikiwa nasakata kabumbu na wana kitaani, ndipo orodha ya majina ilitoka sambamba na maelezo kuwa tutume pasipoti tuandaliwe visa na tiketi kwa ajili ya safari.

Hapo ndipo kizungumkuti kilianza, patashika nguo kuchanika watu kuvaa magunia. Ukweli ni kuwa sikuwa na paspoti muda huo, na Scholarship ina mpunga wa kueleweka. Nikaanza sasa kufanya mchakato wa kutafuta pasipoti ili nitume. Kama ilivyo ada, nikaanza na kujaza fomu ya pasipoti mtandaoni. Mbuzi wa masikini hazai, kwa bahati mbaya nilikuwa nimepoteza cheti cha kuzaliwa, hivyo nilikuwa natumia nakala niliyokuwa nayo kwenye masuala yangu.

Baada ya kujaza fomu nikaipakua kutoka mtandaoni, kisha nikaambatanisha viambatanisho vyote, halafu nikaenda kwenye ofisi za uhamiaji za mkoa, kuenda pale nikaambiwa bwana, cheti cha kuzaliwa tunataka orijino, kwa sababu hii nakala yako kuna namna namba hazisomeki, nikajaribu kuongea nao kiume na kuwaeleza kuhusu mchakato mzima wakasema kijana lazima ukalete cheti halisi. Kumbuka cheti kimekataliwa muda huo, cha ajabu ni kuwa NIDA ina kila taarifa ambazo zimo katika cheti cha kuzaliwa, sasa kwa ile dharura, kwa nini wasitumie NIDA ambayo inaweza kuwa mbadala wa cheti cha kuzaliwa. Nikapiga moyo konde, kwa msaada wa bodaboda nikazitafuta ofisi za RITA pale mkoani nikafika. Baniani mbaya kiatu chake dawa, bwana naenda pale nikaambiwa nifuate ripoti ya upotevu kituo cha polisi ili wanishughulikie.

Maji ukiyavulia nguo sharti uyaoge, nikaenda kituoni, nikafanya mchakato huo na malipo, alhamdulillah, nikapata ile hati. Basi narudi ofisini mida ya saa tisa unusu hivi, Pamoja na kubembeleza, nikaambiwa muda wa kazi umeisha ila nikiangalia ubao wa matangazo imeandikwa mwisho wa kazi ni saa kumi. Nikaona isiwe taabu, nikalala, keshoye nimeenda pale RITA wakaangalia makaratasi yangu wakasema hawawezi kuchakata cheti pale, mpaka niende mkoa, na wilaya nilikozaliwa ndiko nikafuatilie hicho cheti. Nikarudi uhamiaji, wakati niko pale, wazo likanijia nikauliza nikiomba pasipoti leo nitaipata lini, nikawaambiwa ni baada ya wiki mbili kwa sababu, mpaka taarifa ziende Dar (makao makuu). Nikawaomba tena, zimwi likujualo halikuli ukakwisha, afisa akachukua fomu yangu akakagua akagundua kuna kosa badala ya kujaza sehemu nilikozaliwa nilijaza ninakoishi, akaniambia nikafanye marekebisho, ikumbukwe kufanya marakebisho unalipa 20,000/= kwa sababu ukishapakua fomu mtandaoni huruhusiwi kufanya marekebisho tena. Nikajisemea haina shida, nikarud kazini kwangu, nikijua nina muda wa kutosha nikajipange nianza mchakato upya baada ya kupoteza gharama zote hizo kwenye usafiri na malazi.

Kibarua nilichokuwa nacho ni kurudi mkoani kwangu kuchakata cheti, kisha nijaze fomu mpya kisha niende uhamiaji tena. Nimefika usiku kazini kwangu, sijakaa vyema ikaingia email nyingine inayonitahadharisha kuwa siku ya mwisho (deadline) ya kutuma ni ijumaa na muda huo kwangu ni Jumanne. Usiku huohuo nikachukua gari kurudi mkoani kwangu, nafika stendi sina hili wala lile “maafisa usafirishaji” wakanikatia tiketi kumbe ni magumashi wanakukatia halafu wanakaa kusubiri gari wakubambikizie humo ili wao wapige cha juu, wakanipakia kwenye basi sitalitaja jina, mbaya zaidi siti mule ndani zimejaa, basi nikasimama kutoka mikumi mpaka tulipofika uheheni, kuna mtu alishuka kwahiyo nikapata siti ili kuwahi unyakyusani. Nilifika jioni, moja kwa moja mpaka ofisini pale RITA nikawaelezea mkasa mzima, wakanipa fomu nikajaza kisha nikaambiwa, kupata cheti ni mpaka kesho yake, kumbuka hiyo ni Jumatano natakiwa niwe Dar Alhamisi, na ijumaa ndiyo siku ya mwisho. Kesho yake nimedamka asubuhi nimepewa cheti changu mara moja nikaanza kuenda Dar.

Safari ya usiku nikaamkia Uhamiaji House pale, nikawasilisha viambatanisho, lakini maafisa wakadai kuwa vinatakiwa vipigwe muhuri na mwanasheria ndipo nivilete (changamoto nyingine hiyo, mwanasheria nae akataka 5000/= kwa kila cheti, na ninavyo kama kumi: 50,000/=). Nikaongea naye kishikaji yule Mama nikalipa 20000/= akanirekebishia. Nikarudi kisha nikawaelekeza kuwa nina dharura ya siku ya mwisho leo. Wakasema haiwezekani kwa sababu pasipoti zinakamilika baada ya wiki moja. Chukulia kwa mfano ningekuwa mgonjwa, yaani unakufa huku unajiona. Sikuwa na namna zaidi ya kukubali matokeo kwamba baada yay a jitihada, sadaka na gharama zote hizo, matokeo ni sifuri, fursa imenipotea na nirudi mzigoni kwangu. Kwa mara ya kwanza nilipata hasira na chuki kwa nchi yangu, uzalendo ulinishuka ghafula. Lakini, apangalo mungu binadamu hawezi kulipangua, nikiwa kwenye daladala nikapata wazo kuwa niwaandikie wale jamaa email ya delay. Kweli bwana, nikaandika email nikaelezea hali halisi ilivyo si unajua mbongo ukimpa nafasi ya kujitetea. Wakanielewa na wakaniongezea wiki moja. Mambo yakaenda kama alivyopanga Mola. Ila ukitafakari kwa kina unaona shida kubwa, madudu na uzembe kwenye mifumo na ofisi za umma, hakuna utaratibu maalaumu, uwajibikaji upo chini mno.

Kwa mikasa hiyo, Tanzania ninayoinong'ona ni:

Tanzania ambayo ninaweza kuchakata cheti cha kuzaliwa ofisi yoyote, si lazima mpaka nilikozaliwa kwa sababu mfumo ni uleule mmoja kwa RITA.

Tanzania ambayo kila ofisi ya uhamiaji mikoani ina uwezo wa kutayarisha pasipoti kwa wakati, hususani wakati wa dharura.

Tanzania ambayo mifumo yake ya ujazaji fomu mitandaoni inaruhusu kuhariri kama kuna makosa na kuyarekebisha bila kulipa tena kwa mara nyingine ili kuepushs gharama zisizo na mantiki.

Tanzania ambayo, ukitaka lost report huna haja ya kufika kituoni, unaingia mtandaoni unajaza taarifa, unafanya malipo na kisha unapakua ripoti yako na kuendelea na michakato mingine.

Tanzania yenye utaratibu madhubuti wa utayarishaji wa vyeti papo kwa papo, kungerahisisha maisha hasa wakati wa dharura.

Tanzania ambayo makampuni ya usafirishaji yana mifumo imara, yenye utaratibu tusingekuwa na utapeli na mateso wakati wa kusafiri.

Tanzania ambayo kitambulsiho cha NIDA kina uwezo wa kutumika kama mbadala wa cheti cha kuzaliwa hasa wakati wa dharura, kusingekuwa na mihangaiko isiyo ya msingi.

Tanzania ambayo kuna ofisi au mamlaka fulani ya kushughulikia uhakiki wa vyeti na ugongwaji mihuri wa nyaraka nje na utegemezi wa asasi za wanasheria binafsi, ama Tanzania ambayo nyaraka zake zote zinatolewa zikiwa tayari zimeshahakikiwa na mwanasheria, kungepunguza milolongo na gharama zisizo na maana yoyote.
 
Upvote 2
Mambo yakaenda kama alivyopanga Mola. Ila ukitafakari kwa kina unaona shida kubwa, madudu na uzembe kwenye mifumo na ofisi za umma, hakuna utaratibu maalaumu, uwajibikaji upo chini mno
Dah, pole sana. Ila vizuri mwishowe ulikamilisha mchakato. Haiya twende kazi.


Tanzania ambayo kitambulsiho cha NIDA kina uwezo wa kutumika kama mbadala wa cheti cha kuzaliwa hasa wakati wa dharura, kusingekuwa na mihangaiko isiyo ya msingi.
Exactly


Tanzania ambayo kuna ofisi au mamlaka fulani ya kushughulikia uhakiki wa vyeti na ugongwaji mihuri wa nyaraka nje na utegemezi wa asasi za wanasheria binafsi, ama Tanzania ambayo nyaraka zake zote zinatolewa zikiwa tayari zimeshahakikiwa na mwanasheria, kungepunguza milolongo na gharama zisizo na maana yoyote.
Kuna mambo kama haya ni sheria tu na nyingine zinapitwa na wakati. Ni kama ile ya kuzima simu ukifika petroli station. Sheria iliyotungwa enzi mabetri yanalipuka kirahisi lakini hadi leo utakuta📵📵.
Ndio kama mambo ya kuhakiki vyeti, yalianza enzi hizo mifumo hakuna, watu wanafoji vyeti na huwezi kuhakiki online. Yaani bro utashangaa hadi wanaoenda kufanya usaili RITA bado wakaomba cheti chako cha kuzaliwa na wanataka kipigwe muhuri na mwanasheria kwamba ni nakala halisi whaaaat?🤯🤯🤯
 
Back
Top Bottom