Miongozo ya Mwalimu Nyerere dhidi Ukoloni Mambo leo

Miongozo ya Mwalimu Nyerere dhidi Ukoloni Mambo leo

emaJenerali

Member
Joined
Mar 7, 2014
Posts
11
Reaction score
1
WAKATI Tanganyika inapata uhuru mwaka 1961 Mwalimu Nyerere alitangaza vita dhidi ya maadui watatu yaani Ujinga, Maradhi, na Umaskini. Hawa ni maadui ambao kwa wakati ule Mwalimu Nyerere aliwaita ni maadui wa Maendeleo.


Mapambano dhidi ya maadui hawa maradhi, ujinga, umaskini yalipita katika Miongozo mbalimbali ambayo Mwalimu Nyerere aliona kwamba Miongozo hiyo itafanikisha vita dhidi ya maadui hao.


Miongozo ambayo ingetatua changamoto za Maendeleo kwa haraka tena kwa muda mfupi hasa ukizingatia nchi ilikuwa imetoka mikononi mwa wakoloni kwa hiyo nguvu za ziada zilihitajika kuimarisha Uchumi.

Moja ya Miongozo ambayo Mwalimu Nyerere aliona inafaa kupambana na maadui hawa ni kujiweka huru bila kutegemea misaada kutoka kwa mabepari (Azimio la Arusha la mwaka 1967) ambalo lilikuwa na lengo la kuiweka Tanzania katika hali ya kujitegemea na kuondokana na unyonyaji. Hatua hii ilionekana ni dalili za Ukombozi kwa watanzania ambao walikuwa wanakabiliwa na maadui hawa watatu.


Nia ya Mwalimu katika Azimio hili ni tujitegemee kwa hali yoyote ile, tutumie rasilimali tulizonazo mfano ardhi, uoto wa asili, mbuga za wanyama, madini, nakadhalika kujiletea Maendeleo.


Tutumie rasilimali zetu bila kutegemea misaada pamoja na mikopo kutoka nchi za magharibi, hii ndiyo ilikuwa shabaha ya sera ya Ujamaa na kujitegemea.


Katika Azimio hili Mwalimu Nyerere anatambua kuwa nchi yetu si maskini kiasi cha kushindwa kutumia rasilimali tulizokuwa nazo na kujitawala (kujiletea maendeleo) na kwamba misaada, mikopo,uwekezaji, pamoja na ubinafsishaji ambao tunategemea kutoka kwenye nchi zilizoendelea hazitatutimizia kila kitu tunacho kihitaji bali itatuondolea uhuru wetu tulio kuwa nao.


Kwa kulidhihirisha hilo, Mwalimu Nyerere anaseama “tumepuuzwa kiasi cha kutosha. Unyonge wetu ndio uliotufanya tuonewe, tunyonywe na kupuuzwa. Sasa tunataka Mapinduzi, Mapinduzi ya kuondoa unyonge ili tusionewe tena na wala tusipuuzwe tena”


Maneno ambayo yaliupinga Ukoloni Mambo leo. Nyenzo kuu nne zilijengwa kuhakikisha Ukoloni mambo leo unapingwa vikali kwenye sera ya ujamaa na kujitegemea ambazo ni pamoja na umoja, mshikamano, upendo, pamoja na hari ya kufanya kazi kwa wananchi ili kuuendeleza Ujamaa.


Baada ya Azimio la Arusha la mwaka 1967, ilifuatiwa na Mwongozo wa mwaka 1971 ambao kilikuwa ni kipindi cha uzalendo uliozaliwa na itikadi ya umajumui wa Afrika (Pan- Africanism). Pia muda huo ulikuwa ni wakati wa kupalilia mapambano ya Waafrika dhidi ya Ukoloni (Ukoloni Mambo leo).
Kama ilivyoelezwa muuongozo huu ulikuwa mwendelezo wa Azimio la Arusha, kwa hiyo Shabaha ya Mwongozo huu ulikuwa ni kupambana na maadui watatu ujinga, maradhi, na umaskini ambao ulikuwa umeainishwa kwenye Azimio la Arusha.


Mwongozo huu wa mwaka 1971, ulipokelewa kwa hisia kali na wananchi hasa ukizingatia kwamba ulikuwa na misimamo ya kizalendo ya kulitumikia taifa pia Shabaha yake ya kupambana na ujinga, maradhi, na umaskini.
Misimamo ya Kizalendo ambayo imegusiwa kwenye mwongozo huu wa mwaka 1971, ni pamoja na swala la ulinzi wa ndani na wa nje ya nchi.


Kwa mfano, sera ya ulinzi na usalama ambayo ilitekelezwa mwaka 1971 iliibua hisia miongoni mwa wananchi na kupandikiza uzalendo ambao uliwafanya wafanyakazi wa sekta mbalimbali kujiunga na Jeshi la mgambo ambapo Jeshi hilo lililotumika kumwondoa Iddi Amin Dada wa Uganda dhidi ya uvamizi.


Bado msisitizo wa mwongozo huu unaendelea kuunga mkono Azimio la Arusha kwamba, maendeleo yenye maana ni yale yanayotuondolea kuonewa, kunyonywa, kunyanyaswa, na mawazo ya kufungwa na kutunyima uhuru na utu wetu.


Kwa mantiki hiyo, Uliberali Mambo leo ulipingwa vikali na kuuona kwamba kuuruhusu ni kuendeleza unyonyaji, kuonewa, kunyanyaswa, na kufungwa kimawazo, pia itatunyima uhuru wetu.


Mwongozo huu wa Kizalendo ulidumu hadi mwaka 1981, ambapo baadae ulizaliwa Mwongozo mwingine mwaka huo huo ambao ulijulikana kama kipindi cha mpito kutoka muhula wa kizalendo na kuingia muhula wa Uliberali mambo leo.


Mambo yalibadilika kwenye Muhula huu wa Uliberali mambo leo, ikiwamo lile la kuzaliwa kwa chama cha mapinduzi baaada ya kuungana kuwa kitu kimoja TANU ya Tanzania Bara na ASP ya Zanzibar, pia kuundwa kwa Katiba Mpya ya mwaka 1977 pamoja na mambo mengine ya kiutawala yalibadilika.


Kwa mfano madaraka ya Umma kuanzia vijijini hadi Wilayani na Mijini, kuimarisha na kupanua demokrasia nchini kupitia uchaguzi ulio huru na wa haki, pia suala la haki za binadamu liliingizwa kwenye katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.


Hakika mwongozo huu wa, Uliberali mambo leo ulikinzana sana na mwongozo wa mwaka 1971 pia Azimio la Arusha uliokuwa ukijielekeza kwenye mapambano dhidi ya Ukoloni mambo leo na Ubeberu ambao ulikuwa umewekewa ulinzi dhidi ya uvamizi.


Tafsiri ya Mwalimu aliyo iongea kwenye Azimio la Arusha kwamba, tumenyonywa vya kutosha, pia tumepuuzwa vya kutosha na wakoloni vilioonekana havina msingi yoyote kwenye Mwongozo huu wa mwaka 1981.


Pia, mapambano dhidi ya ukoloni mambo leo yalionekana hayana maana yeyote kwenye nchi ambayo inataka maendeleo ya haraka kwa maana ya kuruhusu uwekezaji, ubinafsishaji, misaada kutoka kwa wahisani, mikopo kutoka benki ya dunia (WB), (IMF) na mashirika mengine ya mikopo kitu ambacho kimetuongezea maadui wa Maendeleo


Katika vita dhidi ya unyonge, kuonewa, kunyanyanyaswa dhidi ya Ukoloni Mambo leo, kitu ambacho sera ya ujamaa na kujitegemea imeeleza Misaada na mikopo vitahatarisha Uhuru wan chi yetu kama tutaviabudu na kuvisujudu kwa hali yoyote ile.


Sera Ujamaa na kujitegemea inasema, kujitawala hakuwezekani ikiwa taifa moja linategemea misaada na mikopo kutoka taifa jingine kwa maendeleo yake.


Aidha, hata kama pangetokea Taifa au Mataifa ambayo yako tayari kutupa fedha zote tunazohitaji kuendesha mipango yetu ya maendeleo isingekuwa sawa kwa nchi yetu kuipokea misaada hiyo bila kujiuliza matokeo yake yatakuwa ni nini kwa Uhuru wetu na uzima wetu.


Ni lazima kujiuliza maswali mara mbili, kwani fedha hizo wanazotaka kutupa wao hawazitaki? au hazikuwa na manufaa kwao?, kwa sababu hakuna taifa ambalo limeridhika kwa maendeleo yake.


Fikra ambazo hazijapata majibu ya uhakika za kulifanya Azimio la Arusha lipoteze maana kamili ya kuendelezwa na kutatua changamoto za maendeleo.


Baada ya Mwalimu Nyerere kung'atuka madarakani mwaka 1990 mwaka 1991 ulipitishwa mwongozo mwingine ujulikanao kama Azimio la Zanzibar chini ya Rais wa Awamu ya Pili Ally Hassan Mwinyi. Katika mwongozo huu baada ya ule wa mwaka 1981, ulikuwa na lengo la kuuzika rasmi Azimio la Arusha.


Katika hotuba yake Mwinyi kama Mwenyekiti wa Chama anasema kwa hali ya kipindi hicho (1991) hakiruhusu kuendelea kung'ang'ania Sera za Ujamaa na Kujitegemea kwa kuwa tayari kuna mabadiliko mengi ambayo hayaendani na mfumo wa sera ya Ujamaa na kujitegemea.


Katika Azimio hili Mwinyi anaonekana kuukubali kwa asilimia mia moja Ukoloni mambo leo lakini kwa upande wake Mwalimu Nyerere anasema bado anaamini kwamba Azimio la Arusha halina kasoro yoyote labda tu yafanyike mabadiliko ya Kiswahili ambayo kwa wakati huo yalikuwa yameboreshwa.


Baada ya kuuwawa kwa Azimio la Arusha hakuna mwongozo uliokuja na kubainisha mafanikio yaliyofikiwa baada ya kuingia kwa utandawazi, ubinafsishaji, uwekezaji, ambao ndio ulio karibisha ukoloni Mamboleo.
 
Back
Top Bottom