Ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipatia fursa hii ya kujibu swali lako.
Kuna maelekezo kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusiana na swali lako, amesema katika Hadithi iliyosimuliwa na Abdullah bin Amri (r.a) kuwa: Watu wa dini mbili tofauti hawatarithiana
(Abu Dauwd, Ibn Majah, Tirmidh).
Hivyo, ni wazi kuwa Muislamu hawezi kumrithi asiyekuwa Muislamu na kinyume chake pia. Kwa hivyo, ikiwa yule mzazi aliyekuwa ni Muislamu ndiyo aliyeaga dunia basi huyo kijana aliyekuwa si Muislamu hatamrithi mama yake kwa kuwa dini zao ni tofauti. Huyo mtoto atarithi tu ikiwa umri wake ni chini ya barekh, yaani bado kimawazo na kiuwezo (kiuwamuzi ambao kiserikali ni miaka 18 au 21 kwa nchi zingine), hapo atarithi. Lakini ikiwa mtoto ni mkubwa na ana uwezo wa kujitegemea, basi hatarithi na hata kama mtoto ndie aliyetangulia kufariki na umri wake ni mkubwa kwa maana anajitegemea na wazazi wake ni Waislam kinyume na imani ya mtoto wao nao hawatarithi.
Vile vile mtoto aliyezaliwa nje ya ndoa hana haki ya kumrithi baba aliyemzaa na baba hana haki katika mirathi yake. Mtoto atarithi kwa mama yake tu, na mama atarithi kwa mtoto wake.
Zingatia:
Lakini ikiwa Mzazi/Mtoto Muislamu ameacha wasia na amemtunukia kitu mfano baadhi ya mali, basi atapewa bila ya wasiwasi wowote, lakini hizo mali za usia hazitakiwi kuzidi zaidi ya theruthi moja (1/3).
Kwa ufupi ni kuwa Muislamu hamrithi hasiyekuwa Muislam mfano: Mkristo au Myahudi au Baniani na wao hawatamrithi Muislamu hata akiwa karibu naye kiasi gani katika nasaba.
Mirathi itakwenda kwa Wale watoto wake wawili na kiasi kidogo atarithi mume wake. Lakini kuangaliwa hapa kama mtoto bado mdogo, si barekh kwa maana yupo chini ya uangalizi wa mama yake au alikuwa chini ya uangalizi wake, huyu atarithi pamoja na nduguze wa mama mmoja.
Cha kuzingatiwa kabla ya kugawanywa kwa mirathi zitolewe pesa za maziko na madeni aliyonayo marehemu, pamoja na kutimiza usia wa marehemu.
May Allah guide you and set your affairs right.
Allahu A'lam