SoC03 Misingi ya Utawala Bora

SoC03 Misingi ya Utawala Bora

Stories of Change - 2023 Competition

SanPedro

Member
Joined
Apr 4, 2019
Posts
41
Reaction score
89
Utawala bora ni utekelezaji wa sera kwa njia ya uwazi, ufanisi, ushirikishwaji wa wananchi, uadilifu na uwajibikaji kwa kufuata misingi ya katiba na utawala wa sheria ili kulinda rasilimali za umma.

Katika ngazi zote za utawala, kuanzia serikali kuu mpaka serikali za mitaa ili kufikia dhana ya utawala bora ni lazima misingi na nguzo za utawala bora zifuatwe. Misingi ya utawala bora ni uwazi, ushirikishwaji, uwajibikaji, ufanisi, maridhiano, utawala wa sheria na uadilifu. Nguzo kuu za utawala bora ni; katiba ya kidemokrasia, mgawanyo wa madaraka, uhuru wa kujieleza, uhuru wa vyombo vya habari, uhuru wa mahakama na ulinzi, ukuzaji na uzingatiaji wa haki za binadamu.

Kwa mujibu wa ibara ya 129(1) ya katiba ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, kama ilivyorekebishwa na sheria nambari (3) ya mwaka 2000, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), iliundwa ikiwa ni idara huru yenye majukumu ya; Kuhamasisha hifadhi ya haki za binadamu, kupokea malalamiko ya uvunjwaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora, kufanya utafiti, kutoa na kueneza elimu kwa umma kuhusu haki za binadamu na utawala bora. Kadharika, kushirikiana na mashirika na taasisi za kimataifa, kikanda na kitaifa zenye uzoefu na uhodari katika ukuzaji na ulinzi wa haki za binadamu na utawala bora.

Licha ya uwepo wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), bado dhana ya utawala bora haijaweza kufikiwa kutokana na sababu zifuatazo.

Kutoheshimiwa kwa uhuru wa habari na vyombo vya habari. Utawala bora unaheshimu uhuru wa watu kuwa na mazingira ya kuzungumza na kupeana habari. Vilevile utawala bora unaheshimu haki ya watu kupata habari kutoka katika vyombo huru vya umma na binafsi, vyenye uwezo wa kutafuta, kuandika, kuhariri na kusambaza habari kwa watu, pasipo kuingiliwa na serikali ili kuweza kusambaza habari ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.

Kutoheshimiwa kwa uhuru wa kupashana habari kumepelekea kukosekana kwa uhusiano mzuri kati ya waandishi wa habari na jeshi la polisi. Kwa mfano, Semptemba 2, 2012, mwandishi wa habari wa kituo cha televisheni (Channel Ten) Daudi Mwangosi, aliweza kuuliwa na jeshi la polisi kijijini Nyororo, mkoani Iringa akiwa katika utekelezaji wa majukumu yake wakati wa maandamano ya wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Kucheleweshwa kwa haki bila sababu ya msingi. Kumekuwa na utaratibu wa watu kukamatwa na jeshi la polisi kwa tuhuma mbalimbali na kuwekwa rumande au mahabusu kwa mda mrefu pasipo kupewa nafasi ya kusikilizwa au kufunguliwa kesi mahakamani. Kwa mfano, George Sanga, aliyekuwa katibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) jimbo la Njombe mjini na wenzake, Optatus Nkwera na Goodluck Mfuse kwa pamoja wameweza kunyimwa haki ya kupelekwa mbele ya mahakama kujibu tuhuma dhidi yao na kusalia mahabusu kwa zaidi ya miaka miwili sasa. Watuhumumiwa walishtakiwa kwa kuhusika na mauaji ya mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Emmanuel Mlelwa mnamo Semptemba 21, 2020.

Kukosekana kwa uhuru wa mahakama.
Ili kufikia dhana ya utawala bora ni lazima uhuru wa mahakama uheshimiwe. Kwa mujibu wa ibara ya 107B ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, kila jaji au hakimu yupo huru kuamua kesi iliyopo mbele yake kwa mujibu wa sheria na ushahidi ulioletwa mbele yake bila kushinikizwa na mtu au chombo chochote, ikiwemo bunge na serikali.

Katika uongozi wa awamu ya tano chini ya aliyekuwa raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hayati Daktari John Pombe Magufuli uhuru wa mahakama ulibinywa. Kwa mara kadhaa raisi alisimama na kutoa kauli zinazokiuka katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977 na kuingilia uhuru wa mhimili wa mahakama. Kwa mfano; Katika maadhimisho ya siku ya sheria duniani tarehe 4, februari 2016, alisema "Kuna kesi zaidi ya 400 zilizopo mahakamani ambazo kama zikiendeshwa ipasavyo, serikali itapata pesa taslimu shilingi trilioni moja kama fidia kutoka kwa wadau". Raisi alitoa kauli hiyo akiahidi kuwapatia mahakama kiasi cha shilingi bilioni mia mbili.

Kwa mujibu wa ibara ya 13(6) (a) na 107B ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, watu wote ni sawa mbele ya sheria na wanayo haki bila ubaguzi wowote, kulindwa na kupata haki sawa mbele ya sheria. Hivyo basi, kauli yake inaingilia uhuru wa mahakama, kwani hakuna wakili anayeweza fika mahakamani akijua mteja wake atashindwa kesi. Hali kadharika kutokana na kauli hiyo, hakuna jaji atakayeweza kutoa hukumu dhidi ya serikali ukizingatia kuwa jaji ni mteuliwa wa huyo raisi.

Ukiukwaji wa haki za binadamu. Haki za binadamu ni stahili alizonazo kila binadamu kutokana na asili ya utu alionao, kama vile; haki ya kuwa hai, haki ya uhuru wa mtu binafsi, haki ya uhuru wa maoni na haki ya kushiriki shughuri za umma.

Utawala bora unaofuata misingi ya utawala wa sheria husaidia kukuza hifadhi ya haki za binadamu. Hali kadharika ukiukwaji wa nguzo na misingi ya utawala bora huchochea ukiukwaji wa haki za binadamu. Nchini Tanzania ukiukwaji wa haki za binadamu umeweza kujidhihirisha katika mambo mbalimbali yanayofanywa na watendaji wa serikali. Kwa mfano; Mchakato wa kuwaondoa watu wa jamii ya wamasai huko Loliondo ili kupisha shughuri za utalii na hifadhi ya wanyamapori ulikuwa kinyume na haki za binadamu, kwani wananchi walinyimwa fursa ya kushirikishwa kufanya maamuzi juu ya mambo yanayohusu maisha yao. Na mnamo, juni 8, 2022 askari walivamia vijiji na kuondoa watu kwa nguvu, jambo lililoleta mvutano mkubwa kati ya wananchi na serikali.

Utawala bora ni chachu ya kukuza maendeleo ya nchi, kwani huchangia katika kuleta ustawi wa wananchi kwa kuimarisha utoaji wa huduma bora. Hivyo, nitoe wito kwa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), kuwajibika ipasavyo kutekeleza majukumu yake bila kulegalega ili taifa liwe na jamii yenye utamaduni wa kuheshimu misingi ya utawala bora na haki za binadamu. Kadharika, tume iwekeze vya kutosha katika kufanya uchunguzi juu ya uvunjwaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora, pasi na shaka kufungua mashauri mahakamani ili kuzuia vitendo vya uvunjaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora.
 
Upvote 3
Mdau piga kura yako ..
Andiko hili liweze kuifikia Tume ya Haki za Binadamu & Utawara Bora ..
 
Back
Top Bottom