Miss Unsinkable: Mhudumu wa Titanic aliyenusurika kifo mara nne kimiujiza

Miss Unsinkable: Mhudumu wa Titanic aliyenusurika kifo mara nne kimiujiza

Hashpower7113

JF-Expert Member
Joined
Sep 26, 2011
Posts
1,353
Reaction score
2,142
Kunusurika kwenye ajali, siyo jambo jepesi na ni wale wenye bahati ya kipekee tu ndiyo wanaoweza kunusurika, yaani ajali mbaya imetokea, watu kibao wamepoteza maisha lakini wewe ukatoka ukiwa hai, ni Mungu tu!

Ukijaribu kuwasikiliza watu waliowahi kunusurika kwenye ajali, ambao wengi huwa wamenusurika kwenye ajali moja, watakueleza jinsi walivyokuwa na bahati ya mtende kutoka salama kwenye mdomo wa mauti na jinsi wanavyomshukuru Mungu.

Lakini hebu fikiria, mtu ananusurika kufa kwa maradhi, baadaye anakuja kunusurika kwenye ajali kubwa ya kwanza iliyosababisha vifo vya watu kibao, miaka michache akaja kunsurika tena kwenye ajali mbaya kuliko ile ya kwanza, maisha yakaendelea! Baadaye akaja kunusurika kwa mara ya tatu kwenye ajali mbaya zaidi! Ni jambo la ajabu si ndiyo?

Basi kwa taarifa yako, Violet Constance Jessop au Miss Unsinkable aliyezaliwa Oktoba 2, 1887, anaingia kwenye rekodi ya aina yake duniani, baada ya kunusurika kufa kwa maradhi na baadaye kunusurika kwenye ajali kubwa tatu za meli, ikiwemo ajali ya meli ya Titanic.

1125381

Jessop alikuwa mhudumu wa kwenye meli (stewardness) na nesi aliyekuwa akiwahudumia abiria na manahodha. Kabla hajaanza kazi hiyo, kwa mara ya kwanza akiwa na umri mdogo, Jessop alianza kuugua ugonjwa hatari wa kifua kikuu (TB), madaktari wakamueleza yeye na wazazi wake kwamba asingeweza kupona!

Hata hivyo, katika hali ambayo hakuna aliyeitegemea, alipona maradhi hayo, maisha yakaendelea.

Baadaye, baba yake alifariki yeye akiwa na umri wa miaka 16 tu, akalazimika kuanza kusaidiana na mama yake kuwalea wadogo zake. Mama yake alikuwa akifanya kazi ya uhudumu kwenye meli, kwa hiyo muda mwingi alikuwa akisafiri na kumuacha awaangalie wadogo zake.

Hata hivyo, miaka michache baadaye, mama yake naye alifariki na kumuachia jukumu la kuwalea wadogo zake. Akalazimika kutafuta ajira na hapo ndipo alipopata kazi kama aliyokuwa akiifanya mama yake, ya uhudumu kwenye meli.

Akiwa na umri wa miaka 21, aliianza kazi hiyo kwa kuajiriwa kwenye meli ya Royal Mail Line, hiyo ilikuwa ni mwaka 1908. Miaka mitatu baadaye, alihamishiwa kwenye meli kubwa na ya kifahari kwa wakati huo, RMS Olympic.

Mwaka huohuo, Septemba 20, 1911, meli hiyo ilipata ajali mbaya baada ya kugongana na meli ya kivita, HMS Hawke. Violet alinusurika katika ajali hiyo.

Mwaka mmoja baadaye, April 10, 1912, Jessop alikuwa miongoni mwa watu waliokuwa ndani ya meli kubwa ya RMS Titanic wakati ikianza safari yake. Siku nne baadaye, meli hiyo iligonga mwamba kwenye bahari ya North Atlantic na kuzama.

1125382
Zaidi ya abiria 1,517 walipoteza maisha lakini kwa mara nyingine, mwanadada huyo alitoka salama huku akifanya kazi kubwa ya kusaidia kuwaokoa watu wengine. Asubuhi iliyofuatia, Jessop na wenzake waliokolewa na meli ya RMS Carpathia.

Miaka michache baadaye, wakati vita ya kwanza ya dunia ikiendelea, kwa mara nyingine Jessop alikuwa kwenye meli kubwa ya HMHS Britannic, wakati meli hiyo ambayo sasa ilikuwa ikitumika kama hospitali, kuwasaidia majeruhi wa vita ya dunia, ilipopigwa bomu na kulipuka kisha kuzama.

Muujiza mwingine ukatokea, Jessop akawa miongoni mwa watu waliosalimika. Hata hivyo, katika ajali hii, Jessop alipata majeraha makubwa kichwani ambapo alipigwa na ‘propellers’ za boti ya uokozi wakati akijaribu kujiokoa kutoka kwenye meli iliyokuwa inawaka moto.

Hata hivyo, baadaye alipatiwa matibabu na kupona, kwa jinsi alivyokuwa akiipenda kazi yake, baada ya kupona, alirejea kazini na maisha yakaendelea lakini tayari matukio yake ya kunusurika kwenye ajali hizo kubwakubwa, yalimfanya apate umaarufu mkubwa, akabatizwa jina la Miss Unsinkable, ikiwa na maana mrembo asiyezama.

Jessop alifariki dunia mwaka 1971 baada ya kuugua maradhi ya moyo, akiwa na umri wa miaka 83.

Hashpower7113
 
Back
Top Bottom