SoC02 Mjue Nabii wa uongo

Stories of Change - 2022 Competition

Kasiano Muyenzi

JF-Expert Member
Joined
Feb 3, 2018
Posts
13,858
Reaction score
22,729
Manabii wa uongo wamekuwepo ulimwenguni pote tangu kuumbwa kwa ulimwengu hadi leo, ni ukweli usiojificha kabisa kuwa kuna watu hawajui kuwa kuna nabii wa uongo bali waliopo ni manabii wa kweli, hasa wale wanaotabiri na kuombea kwa jina la Yesu.

Nimeandaa hii mada ili iweze kukusaidia kumjua nabii wa uongo.

Nabii wa uongo ni mtumishi anayetumia karama ya kinabii kwa ajili ya kijiendeleza binafsi, kwa kudanganya watu.

Kuna swali pengine umewahi kujiuliza nalo ni hili : Kwa nini Mungu awaruhusu manabii wa uongo waingie ndani ya kanisa lake? Jibu la swali hilo linapatikana katika Biblia kitabu cha Kumbukumbu 13 :

"Kukizuka katikati yako nabii, au mwotaji wa ndoto, akikutolea ishara au ajabu, ikatukia ishara au hiyo ajabu aliyokuambia akisema, Na tuifuate miungu mingine usiyoijua, tuitumikie hiyo : wewe usiyasikilize maneno ya nabii yule, au yule mwotaji wa ndoto ; Kwa kuwa BWANA Mungu wenu, yuawajaribu, apate kujua kwamba mwampenda Bwana, Mungu wenu, kwa mioyo yenu yote na roho zenu zote " (Kum 13 :1-3)

Kutokana na mistari hiyo, hatujui tu kwamba manabii wa uongo wamo kanisani bali tunajua pia sababu ya kuwepo kwao. Wamo kwa ajili ya kujaribu mioyo ya wapendwa.

Watu wengi hawajui kuwa , nabii wa uongo atahukumiwa pamoja na wale aliowadanganya na wakamtii wote watahukumiwa

Mistari ifuatayo inatuthibitishia kuwa ;manabii wa uongo pamoja na wale wanaowatafuta na kuwaendeleza wote wataangamizwa.

"Wala msisikilize maneno ya manabii wawaambiayo ninyi, ya kwamba, Hamtamtumikia mfalme wa Babeli maana wanawatabiria uongo. Kwa maana mimi sikuwatuma, asema, bali wanatabiri uongo kwa jina langu ;nipate kuwatoeni nje, mkaangamie, ninyi, na Manabii hao wanao watabiria" (Yer 27:14-15)

Ni wazi na tunaona jinsi walivyo na ushawishi mkubwa kwa watu wenye matatizo ya kiafya na kiuchumi hivyo huweza kuwadanganya kirahisi watu wenye shida kama hizo. Ni kweli manabii wa uongo wanaweza kufanya muijiza kwa jina la Yesu Kristo. Yesu alitoa tahadhari mapema dhidi ya hao "watenda miujiza" wenye nguvu za kishetani maana huwa wanatumia uwezo ambao hautoki kwa Mungu. Uwezo na nguvu za manabii wa uongo hutoka katika uweza wa Shetani na mapepo.

Ni kweli, Yesu alilionya kanisa Lake katika karne zote kwamba watakuwepo manabii wa uongo katika kanisa ambao watatumia nguvu za Shetani katika kudanganya kanisa.

Manabii hao wa uongo watakuwepo hadi siku Yesu atakaporudi!

Lengo kubwa la hao manabii wa uongo ni kuwapoteza wale watu wasiijue kweli, kuwadanganya hata wapendwa wateule wasishike neno la kweli na badala yake washike hadithi za uongo.

Biblia inaonya ;

"Maana utakuja wakati watakayo yakataa mafundisho yenye uzima ;ila kwa kuzifuata njia zao wenyewe watajipatia waalimu makundi makundi, kwa kuwa wana masikio ya utafiti ;nao watajiepusha wasisikie yaliyo kweli, na kuzigeukia hadithi za uongo" (2 Tim 4:3-4).

Ni muhimu sana tena ni lazima kabisa kwamba tuwe macho kwa ajili ya manabii wa uongo na unabii wanaoutoa. Na mara tunapogundua kwamba tunakabiliana na nabii wa uongo, ni lazima kabisa tutumie mamlaka kuu ya Kristo katika kumshughurikia huyo nabii wa uongo.

Ukimtambua nabii wa uongo alivyo na tabia zake zilivyo unaweza kukabiliana naye asikudanganye.
Jambo la kusikitisha kuna mtindo umezuka siku hizi kila anapoibuka nabii ama mtumishi yeyote mpya watu wengi badala ya kumchunguza na kumfahamu kiundani kama ni nabii wa kweli ama lah, wao hukimbilia kumsimanga ama kumsifia pasipo kuchukua hatua zozote za kukabiliana naye kwa kutumia mamlaka ya Yesu, na matokeo yake akiwa nabii wa uongo husonga mbele kwa kuwa huwa hana mpinzani mwenye nguvu wala mamlaka ya Yesu bali hupigiwa kelele na walopokaji wapendwa walopokaji tu wasio weza kubatilisha huduma yake ya unabii wa uongo.

UTAMTAMBUAJE NABII WA UONGO?

Nabii halisi wa uongo ni yule ambaye hawezi kamwe kufundishwa wala kusahihishwa.

1. Hakubali kutii mamlaka yoyote, anaamini kwamba mtu yeyote asiyekubaliana na yeye amekosea na hatimaye humfanya kuwa "adui"

2. Hutoa unabii kwa ajili ya kujinufaisha kama ni upande wa fedha, utawala, cheo, au lolote analolitafuta kwa ajili ya faida yake binafsi.

3. Huwa na kiburi kikubwa kabisa. Na mara nyingi ana dhambi kubwa ya binafsi maishani mwake ya kiburi na anasa .

4. Hutumia nguvu za kiroho (nguvu za Shetani) kutoa unabii wake kwa mambo yajayo, sambamba na kutumia njia za siri, za udanganyifu na werevu ili awatawale watu wengine.

5. Hupenda kutoa unabii kwa ajili ya mtu mmoja binafsi na hutumia maneno kama haya ".... Hakuna mtu mwingine atakayeweza kufahamu neno hili. Ni la kwako peke yako. Usimwambie mtu mtu mwingine yeyote neno hili"!

Werevu huo humfanya ajipatie mapato (sadaka) kutoka kwa mtu binafsi anayempatia unabii binafsi wa uongo.

6. Hupenda sana kusifiwa na watu. Na mara nyingi huonyesha unyenyekevu wa uongo

7. Hakubali kushindwa, ni mbishi

8. Anaitika kwa ukali na ushupavu pale anapovumbuliwa.

9. Anatafuta 'kondoo wasiopevuka' na kuwapendeza.

10. Anajiepusha na viongozi waliopevuka wa kweli.

#Mungu anatuambia kwamba tumkatae nabii wa uongo. Ukiwa kama kiongozi wa kanisa ama kikundi cha waabudio halisi, ni vyema kumkabili kwa ujasiri nabii wa uongo na kumshughulikia kwa nguvu na mamlaka ya Yesu ili ashindwe kuendeleza huduma yake ya unabii wa uongo aitumiayo kudanganya watu.

Hao manabii huwa wanaweka hadharani namba zao za simu ili wawasiliane na wenye kuhitaji unabii. Wakati mwingine huwa wanapita majumbani na, maofisini ama kwenye biashara za watu ili wafikishe unabii huko.

Nina jambo la kukushauri ;
ikiwa nabii atakutembelea popote ulipo ili kukuhudumia binafsi, ni vyema ujifunze yote uwezayo kuhusu historia yake. Ni muhimu sana kufahamu angalau historia ya ujumla ya mtu yeyote anayetoa unabii kwako. Unaweza kufanya hivyo kwa kumuuliza maswali yafuatayo ;
1. Ulikuwa katika kanisa gani kabla hujaja hapa?

2. Je ulikuwa msharika wa kanisa lile kwa muda gani?

3. Je umehusiana na makanisa gani mengine mbali ya hilo ulilopo sasa ?
4. Baba yako wa kiimani ni nani na yupo wapi?

Hayo ni baadhi tu ya maswali (nimetoa mfano) Ila unaweza kuwa na maswali yako mengi muulize yote.
Endapo hutaridhika na majibu ya "nabii" basi wasiliana na baba yake wa imani na umuulize kuhusu cheo cha huyo mwanae wa kiimani katika kanisa alilomlelea.
Kwa kufanya hivyo utakuwa umejifunza mengi kuhusu historia ya nabii huyo kama ni nabii wa uongo utajua tu kulingana na sifa zake kama nilizozielezea.

Kumbuka si kila nabii hutoka kwa MUNGU
 
Upvote 0
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…